loader
Dstv Habarileo  Mobile
Corona na mafunzo chanya Dodoma

Corona na mafunzo chanya Dodoma

“HAPA shuleni mara kadhaa tumepewa elimu juu ya kujikinga na ugonjwa wa Covid- 19, tumejua ulipoanzia, unavyoambukiza na namna ya kulinda afya zetu.”

Hayo ni maneno ya Flora William, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Kalenga iliyopo Kata ya Mpwayungu, Wilaya ya Chamwino, Dodoma.

Anasema baada ya likizo ya Covid- 19, shule yao iliweka utaratibu wa kunawa mikono kabla ya kuingia darasani.

“Ilikuwa ni lazima kunawa mikono. Mwanzoni tulikuwa tunaona taabu kidogo kwa vile tulikuwa hatujazoea, lakini sasa kwetu ni jambo la kawaida kwani hata nyumbani kuna kibuyu chirizi, ukifika unanawa mikono kabla ya kuingia ndani,” anasema, binti huyo mkazi wa Kijiji cha Mchichi.

Anasema ni vyema kama utaratibu wa kunawa mikono ukaendelea kwani utawaepusha wanafunzi na magonjwa mbalimbali kama ya matumbo na kuhara.

“Hata ukifika kijijini, nyumba karibu zote zina vibuyu chirizi kwa ajili ya kunawa mikono, hali inayoonesha elimu imewanufaisha wananchi walio wengi,” anasema.

Mwanafunzi mwingine, Amos Godfrey, wa Shule ya Msingi Kalenga anasema elimu waliyoipata shuleni ya jinsi ya kujikinga na virusi vya Corona wanaifikisha majumbani kwa wazazi na wadogo zao.

“Sasa hivi imekuwa kama kanuni, ukitoka chooni lazima unawe mikono hata ile tabia ya kusalimiana salimiana na watu ovyo imepungua na hata tunapokuwa uwanjani tunacheza mpira kumekuwa na uangalifu mkubwa,” anasema.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Lusinde iliyopo Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Naimu Saburi anasema: “Baada ya likizo ya Covid -19 shule zilifunguliwa kwa tahadhari kubwa na tahadhari hizo bado zinaendelea. Mwitikio wa kunawa mikono ulikuwa mzuri na hata sasa imesaidia kuwajengea wanafunzi tabia ya kunawa mikono kitu ambacho hapo kabla hakikuwepo.”

Mratibu wa Kampeni ya Usafi wa Mazingira na Ofisa Afya wa Wilaya ya Chamwino, Asha Msengwa, anasema jamii inaendelea kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto juu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona hasa kwa kuendeleza utamaduni wa kunawa mikono.

Anasema jamii imekuwa ikizingatia maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya na hata katika maeneo ya vijijini nyumba nyingi zimefungwa vibuyu chirizi kwa ajili ya kunawa mikono hali inayoonesha elimu inayotolewa kwa jamii inaleta tija na kubadilisha mitazamo ya wananchi kuwa kunawa mikono si wakati wa kula tu.

Hata hivyo, anasema kulikuwa na bado kuna changamoto kwenye vilabu vya pombe za kienyeji kutokana na baadhi ya wanywaji kupokezana kikombe kimoja.

“Hapo ndipo kuna shida, akinywa pombe akiinuka kwenda kujisaidia akirudi hakumbuki kunawa mikono anaendelea kunywa pombe na chombo kile kile anafuta mate ya mwenzie lakini anasiliba na kinyesi,” anasema.

Anawataka waelimisha rika waliopo katika jamii kuwa mfano wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kushawishi jamii kuchukua tahadhari na kutoa ushirikiano.

“Wananchi wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari. Mwitikio wa kunawa mikono umekuwa mzuri sana hata kwa maeneo ya vijijini, kila nyumba utakayopita utaona kuna vibuyu chirizi kwa ajili ya kunawia mikono,” anasema.

Mtendaji wa Kijiji cha Manchali B, Laudislaus Loboto, anasema wao viongozi wanaendelea kutoa elimu kwa jamii.

“Bado kuna changamoto kwenye misiba. Baada ya mazishi ukiwaambia watu watawanyike kwao ni kama kikwazo, lakini tumeweka mikakati kuhakikisha mazishi yakimalizika watu wanatawanyika,” anasema.

Shida Kilindi ambaye ni muelimisha rika kutoka Kijiji cha Mlowa Barabarani anasema kwenye vilabu vya pombe za kienyeji watu wanaendelea na maisha kama kawaida.

“Wakati ule tunatoa elimu ya kuhamasisha watu kujikinga na maambukizi ya corona unapokwenda kwenye kilabu cha pombe utakuta kina milango sita ya kuingilia na kutokea lakini kina ndoo moja ya kunawa mikono au hakuna ndoo kabisa.

“Walikuwa wakisema corona iko kwenye Ofisi ya Mtendaji, zahanati, mahakamani, vituo vya afya yaani sehemu zote ambazo wanahimiza hawawezi kuingia bila kuvaa barakoa ndizo walidhani kuwa zina corona,” anasema.

Muelimisha rika kutoka Kijiji cha Kawawa, George Lugano, anasema utamaduni wa kunawa mikono umekuwa wa kudumu kwani wengi sasa ni utaratibu kwenye nyumba zao.

“Sasa hivi watoto hata wanapokuwa nyumbani wamejijengea utaratibu wa kunawa mikono bila kuambiwa tofauti na zamani mtoto ananawa baada ya kumaliza kula chakula,” anasema.

Mkazi wa kitongoji cha Minyinga, Kata ya Manchali, Eva Mhando, anasema baada ya ugonjwa wa corona kuingia nchini viongozi waliwahamasisha juu ya matumizi ya vibuyu chirizi.
"Mimi nilianza kutumia kibuyu chirizi kabla hata ya Corona kuingia ila nilikiweka nyuma ya nyumba karibu na chooni, lakini baadaye nikaona kwa nini nisiweke kingine mbele ya nyumba ili tuweze kunawa kwa urahisi na hata wageni wanapofika hapa nyumbani wanawe mikono kabla ya kuingia ndani na kulikuwa hakuna kupeana mikono," anasema.

Helena Lesilija anasema aliweka ndoo ya kunawa mikono na sabuni baada ya kupata elimu kutoka kwa maofisa afya.
"Watu wanazingatia sana suala la kunawa mikono ila wengine wanakuwa wagumu. Tunashukuru tulipata elimu kutoka kwa serikali na kwenye mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na wakati mwingine tulipata elimu kwa njia ya vipeperushi vya namna ya kujikinga na virusi vya corona," anasema.

Mkazi wa kitongoji cha Sokoine, Kata ya Manchali, Mosses Manyagi, anasema alikuwa hana uwezo wala ujuzi wa kuwekea kibuyu chirizi lakini sasa si tatizo tena kwake.

"Nashukuru kwa elimu tuliyopata ya kuwekewa kibuyu chirizi hapa
nyumbani kwangu, nitakuwa mjumbe wa kutoa elimu katika jamii
yangu. Hapa kijijini kila nyumba ina kibuyu chirizi na kinatumika na wananchi wanaona fahari kuwa navyo,” anasema.

Msafiri Mhwani ambaye ni muelimisha rika wa shirila lisilokuwa la kiserikali la Woman Wake Up (WOWAP) katika Kijiji
cha Chalinze anasema alikuwa akitoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na virusi vya corona na alikuwa akizunguka kwenye kaya
kuhamasisha matumizi ya vibuyu chirizi.

Mwenyeki wa Kijiji cha Chalinze, Hamisi John anasema wananchi wamekuwa wakichukua tahadhari za kutosha katika suala zima la kujilinda na corona.
Shirika la WOWAP lilitekeleza mradi wa Covid -19 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino lengo likiwa ni kufanya hamasa kuhakikisha kuwa wanawake na watoto wanakuwa sehemu ya kujikinga na maambukizi ya maradhi hayo kwa kupata uelewa wa namna gani maradhi hayo yanaenezwa na kuchukua hatua za katika kujikinga.

Mratibu wa shirika hilo, Nasra Suleiman anasema mradi huo pia ulitekelezwa katika shule za wilaya hiyo ikiwamo Chilanjililo, Chikoti, Mlowa, Azimio, Juhudi, Nzali, Mapinduzi, Matembe, Kalenga na Nagulo.

Anasema walitoa elimu juu ya kujikinga na maambukizi yanayosababishwa na virusi vya corona na baadhi ya shule ziligawiwa vifaa vikiwamo, ndoo, sabuni, vipeperushi na mabango.

“Shule zilipokea vizuri mradi tulifanya kazi na wanafunzi, walimu, maofisa elimu wa kata walitusaidia kufanya kazi yetu vizuri sana,” anasema.

Walifanya pia kikao cha wadau ili kupata elimu waliyotoa kwenye jamii katika Wilaya ya Chamwino. Wadau hao ni pamoja na maofisa afya, watendaji ngazi za kata na vijiji.

“Mafunzo hayo yameonekana kuwa na tija kubwa katika jamii,” anasema.

Anasema kwa kiasi kikubwa jamii imebadilika na imekuwa na utamaduni wa kunawa mikono.

“Katika shule nyingi mpaka sasa unawaji mikono umekuwa endelevu na wanafunzi wanafurahia kunawa mikono,” anasema.

Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana hivi karibuni kupitia polisi Wilaya ya Chamwino zinaonesha kwamba kuna jumla ya kesi za mimba 58 zilizoripotiwa ambapo 53 ni za wanafunzi wa shule za sekondari na watano ni wa shule za msingi.

Idadi hiyo ya wanafunzi waliopata ujauzito inatajwa kuwa ni kubwa na jamii inatakiwa kushirikiana ili kuhakikisha watoto wanalindwa na kila aina ya ukatili ili waweze kumaliza masomo bila kupata madhila za mimba na ndoa za utotoni. Inadhaniwa kwamba likizo ya corona inaweza kuwa imechangia mimba hizo pale wazazi walipolegalega katika kuwaangalia watoto wao.

 

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8213b65e4d43ec08d7ebad9b47549f62.jpg

Mteja anayetaka kutuma mzigo nje au kupitishia ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi