loader
Kaze azidi kuijenga Yanga

Kaze azidi kuijenga Yanga

LICHA ya timu yake kuendele kukusanya pointi tatu kwenye viwanja vya ugenini kocha mkuu wa Yanga Cedric Kaze, amesema bado hajaridhishwa na soka ambalo linaonyeshwa na vijana wake.

Chini ya Kaze Yanga imekusanya pointi tisa, sita kati ya hizo ikizipata ugenini dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na nyingine ilizipata Uwanja wa Karume mkoani Mara kwa kuvunja mwiko kwa kuifunga Biashara United bao 1-0,  juzi Jumamosi.

Akizungumza juzi Kaze, alisema kwa mbali ameanza kuona mwanga wa kile ambacho anataka wachezaji wake wakifanye  na hilo linampa matumaini ingawa matokeo ya kukusanya pointi tatu katika kila mechi nalo ni jambo ambalo analifurahia.

“Najua ni kwanini wachezaji wangu wanashindwa kufuata ipasavyo maelekezo ninayowapa, kwanza ni presha ya kutaka kushinda mechi hilo ndio linasababisha wacheze kwa hofu ukizingatia ligi ya Tanzania inaushindani mkubwa sana,  lakini hili sina wasiwasi nalo taratibu watashika na watafanya ninavyotaka,” alisema Kaze.

Kocha huyo aliyebeba imani na matumaini ya Wanayanga  msimu huu wakiamini atawapa mataji kutokana na uweoz wake alisema kwa namna kazi yake inavyokwenda anaamini hadi kufikia katikakti ya mzunguko wa kwanza mashabiki tayari wataanza kukiona kile alichowaahidi ambacho ni soka la kuvutia.

Alisema uwajibikaji wa wachezaji mazoezini na hata kwenye mechi ni moja ya vitu ambavyo vinamvutia mno, hivyo ni kazi yake yeye kuhakikisha anawaunganisha na kupandikiza mfumo ambayo utawasaidia kucheza kwa malengo na kupata kile ambacho wamekikusudia ifikapo mwishoni mwa msimu huu.

Aidha, kocha huyo alisema mwenendo wanaokwenda nao mpaka sasa unampa matumaini ya kufanya vizuri huko mbeleni kwasababu wachezaji wake tayari watakuwa wameshika kwa ufasaha mifumo anayowataka kuitumia, hivyo mashabiki wa timu hiyo waendelee kuwapa sapoti  ili kuwatia moyo wachezaji wao.

Yanga itamaliza ziara ya Kanda ya Ziwa kwa kumenyana na Gwambina FC ya Misungwi  mchezo  utakaopigwa kesho Jumanne kwenye dimba la Gwambina Complex nje kidogo ya Jiji la Mwanza na endapo itashinda itakuwa imevuna pointi 12 kutoka Kanda ya Ziwa msimu huu.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/edf9e3e10afd246113b7040d3613b5f3.jpg

TAASISI ya Mama Ongea ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi