loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kwaheri Sir Sean Connery muasisi wa sinema za kijasusi za James Bond

WAKATI dunia inatoka kuadhimisha siku ya James  Bond, Oktoba 5 mwaka huu na  huku wakisubiri toleo jingine la filamu ya  James Bond ya No Time To Die,  muigizaji wa sinema za mwanzo za James Bond,  Muingereza mwenye asili ya Scotland, Sean Connery amefariki dunia juzi mjini Nassau , Bahamas akiwa na umri wa miaka 90.

Oktoba 5,1962  ndio siku ambayo sinema ya kwanza katika mtiririko wa sinema za James Bond, Dr. No ilizinduliwa rasmi. Sinema ya No Time To Die ambayo ilitakiwa kutoka mwezi huu, inatarajiwa kutoka Aprili mwakani na inamzungumzia Bond akiwa katika heka heka za kumuokoa mwanasayansi, ambapo katika pilikapilika hizo anakumbana na  dhiki kubwa na kujua mambo mengine zaidi kuliko alichotumwa.

Kwenye sinema hii ya No Time To Die  ambayo James Bond wake ni Graig, anaonekana akiwa ameshastaafu kazi na anaishi katika visiwa vya Jamaica, akiwa huko anajikuta akipata simu kutoka kwa rafiki yake wa CIA, Felix Leiter kwamba anahitaji kumrejesha mwanasayansi huyo.

Hiyo ni sinema ambayo ndiyo ambayo ilitarajiwa kuamsha dunia tena na wakati wa maandalizi haya hakuna hata mtu mmoja ambaye alifikiri kwamba mwanzilishi wa maigizo haya katika  sinema aliyeshiriki sinema ya kwanza ya  James Bond ya Dr No, atafariki dunia.

Sir Sean Connery (huyu ni knighthood) alicheza  sinema ya kwanza ya James Bond ya Dr. No mwaka 1962, kisha akaigiza From Russia With Love, Goldfinger, Thunderball, You Only Live Twice na Diamonds Are Forever .Lakini pia aliigiza moja isiyokuwa rasmi ya Never Say Never Again (1983).

Katika maandiko ya historia ya sinema hizi imeandikwa kwamba mwaka  1961, projuza wa Marekani Albert R. ‘Cubby’ Broccoli alitaka kuingiza simulizi za Ian Fleming za James Bond katika sinema. Baada ya mazungumzo na makubaliano, Mmarekani huyo aliungana na projuza wa Canada, Harry Saltzman, aliyetaka hisa na katika sinema hii ya kwanza Broccoli alipata fedha kutoka United Artists; akiwa na Dola za Marekani milioni 1 aliipeleka 007 katika sinema.

Awali, Broccoli na Saltzman walitaka  Thunderball kuwa filamu ya kwanza katika vitabu vya Bond lakini kutokana na matatizo ya hatimiliki waliamua kuichukua Dr No ambacho kilikuwa kitabu cha sita katika simulizi za Bond, ambayo ilikuwa ni simulizi la anga za juu

Sinema ya kwanza ilianza kufanyiwa kazi  nchini Jamaica, Januari 16 1962 na ikamaliziwa kwenye studio za Pinewood kwa kazi za ndani . Ukiangalia filamu hii unakutana na  mambo mengi ambayo baadaye yalikuwa ndio elementi za James Bond.

Dr. No ilizinduliwa nchini Uingereza Oktoba 5, 1962  kwa kishindo kikubwa, huku wapenzi wa sinema wakisema kwamba  mbabe mpya wa sinema ameingia kitaani na ndio maana kila Oktoba 5 wapenzi wa sinema huadhimisha ‘James Bond Day’.

Katika sinema hii James Bond (Sean Connery) anapelekwa Jamaica kuchunguza mauaji ya mpelelezi mwingine. Bond, akisaidiwa na  mpelelezi wa  CIA Felix Leiter (Jack Lord) na mwanakijiji Quarrel (John Kitzmuller), wanafuatilia mambo mpaka wanakutana na mwanasayansi Dr. No (Joseph Wiseman). Wakiwa ndani ya kisiwa binafsi cha  Dr. No cha Crab Key, Bond anakutana na Honey Ryder.

Wawili hao wanakamatwa na jeshi binafsi la Dr. No na Bond  anapata ufahamu wa anachopanga mwanasayansi huyo kuimaliza Marekani kwa kuangamiza mpango wake wa kutawala anga za juu. Katika hekaheka za kuwania maisha Bond anambabatiza Dr. No ambaye anasukumwa katika kinu cha nyukilia na kisha anamwokoa Honey kabla ya kisiwa hakijalipuka.

Katika waigizaji wote wa Bond, Connery ambaye awali alitamba na Action Of The Tiger, alikuwa anafiti  maelezo na umahiri wa wapelelezi wa Uingereza.

Akitangaza kifo cha  Sean projuza Michael G. Wilson na Barbara Broccoli walisema: “ Tunasikitishwa na habari kwamba  Sean Connery amefariki dunia. Atakumbukwa siku zote kwamba yeye ndiye mwanzilishi kiasili wa James Bond, ambaye ubabe na utamu wa sinema  kwa sasa ulianzishwa na maneno yake matano yaisyosahaulika “ Jina langu ni Bond... James Bond (The name’s Bond… James Bond”) —yeye alifanya mabadiliko makubwa katika sinema za kijasusi akiwa  jasusi ambaye ana sifa zote, mwenye mvuto wa aina yake na kasi ya aina yake katika kufikiri na kufanya mashambulizi.

“Hakika pasi shaka alikuwa ndio ufunguo mkubwa wa mafanikio wa sinema  za James Bond, hatutamsahau kwa hilo.”

Naye  muigizaji wa sasa wa nafasi hiyo ya James Bond, Daniel Craig alisema:  “Nina huzuni kubwa kusikia kifo cha mmoja wa watu mashuhuri wa kweli katika sinema. Sir Sean Connery atakumbukwa kama Bond na zaidi ya hapo.

Aliweza kupambanua, kujua wakati na kuweka staili. Umaridadi na mvuto wake aliouweka katika sinema hakika ulisaidia kutengeneza sinema zenye hadhi kubwa za James Bond. Ataendelea kuwa mmoja wa washawishi katika sinema za aina hii kwa miaka mingi ijayo.  Mawazo yangu yote yapo kwa familia yake na wapenzi wake. Ni matumaini yangu kuwa popote alipo pana uwanja wa gofu na anaendelea kuucheza.”

Kiukweli ni Sean Connery aliyeleta staili na mvuto katika sinema za 007 , staili ambazo mpaka leo ndio zinaendesha sinema  hizi. Bond ni mpenda totoz, ana wiski na anayejitumbukiza katika utata mwenyewe kisha kujinasua.

Akiwa amezaliwa Fountainbridge, Scotland kabla ya kuanza kazi hii ya kuigiza, alikuwa amejiunga na  kikosi cha maji cha Uingereza akitarajia kuiona dunia yote ambako kikosi hicho kipo.

Alikuwa ndani ya jeshi hilo kwa miaka mitatu, ndani ya melivita kisha akaacha na kuamua kuanza mambo mengi lakini si kabla ya kushiriki katika Mr Universe mwaka 1953. Alipata medali ya shaba katika uzito wake. 

Alipokuwa na miaka 23 alikuwa na tatizo la kuchagua kuwa mwanasoka  achezee Manchester United  au kuwa mwigizaji, akaamua kuwa muigizaji. Sinema yake ya kwanza ilikuwa No Road Back ( 1957), ikifuatiwa na na vipande kadhaa katika programu  na sinema kwa ajili ya televisheni  kama Requiem For A Heavyweight (1957), Anna Christie (1957), Another Time, Another Place (1958), Darby O’Gill And The Little People (1959), Macbeth (1961) na Anna Karenina (1961).

Wakati wa majira ya kiangazi 1961 Connery aliingia katika mitaa ambapo  ofisi za Mayfair za Albert R Broccoli na Patna wake Broccoli, Harry Saltzman  na Ofisa Mtendaji  Mkuu wa  United Artists ,  Bud Ornstein walikuwepo. Walimuona Connery akitembea katika mitaa wakampenda. Wakaona chaguo lifaalo la James Bond.Ndipo walipomuingiza kucheza sinema ya Dr No.

Alipewa tuzo ya  Knighthood mwaka 2000.  Na mwaka 2006 Taasisi ya filamu ya Marekani (American Film Institute) ilimpatia tuzo ya mafanikio katika uigizaji  na anatambulika kama waigizaji  wenye mafanikio makubwa.

James Bond katika sinema hizi ni kamanda wa kikosi cha maji. Kiukweli kati ya wagizaji wote waliofanyakazi katika sinema hizi aliyekuwa kwenye melivita kama mpiganaji  wa kweli ni huyu Sean.

Ukiachia mbabe huyo Sean Connery aliyeigiza  katika miaka ya 1962–1967, 1971 na 1983,wengine walioigiza kama  James Bond  ni David Niven (1967) George Lazenby (1969) Roger Moore (1973–1985) Timothy Dalton (1987–1989) Pierce Brosnan (1995–2002) na Daniel Craig (2006–hadi sasa ).

Pamoja na  kuigiza sinema za James Bond katika uhai wake pia alishiriki sinema zingine na mwaka  1988 alipata tuzo kwa ushiriki wake ndani ya sinema ya The Untouchables. Picha nyingine alizoshiriki ni The Hunt for Red October, Highlander, Indiana Jones and the Last Crusade na  The Rock.

Mtoto wake Jason Connery alisema kwamba baba yake alifariki katika visiwa vya Bahamas katika mji wake wa Nassau akiwa amezungukwa na  familia yake. Alisema baba yake hakuwa katika afya njema katika siku za karibuni.

Msemaji wake Nancy Seltzer alisema kwamba kutakuwa na mazishi na maziko binafsi. Amemuacha mke Micheline na watoto Jason na Stephane.

Imeandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya mtandao

 

Swali: Nia ya kufunga ...

foto
Mwandishi: Beda Msimbe

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi