loader
Dstv Habarileo  Mobile
Dk Mwinyi: Zanzibar ni kubwa kuliko tofauti zetu

Dk Mwinyi: Zanzibar ni kubwa kuliko tofauti zetu

“Zanzibar mpya itajengwa na sisi wenyewe bila kujali itikadi zetu, Zanzibar ni kubwa kuliko tofauti zetu, nipo tayari kuendeleza maridhiano na kushirikiana kujenga Zanzibar yetu,” amesema Dk Hussein Ali Mwinyi mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Zanzibar.

Aidha Rais Mwinyi mara baada ya kuapishwa amesema atafanya kazi kwa uwazi, uwajibikaji na usawa bila ubaguzi.

“Serikali nitakayoiunda itakuwa ya uwazi, uwajibikaji na usawa bila kubagua mtu kwa rangi au eneo analotoka ambayo itakayokuwa ikizingatia nidhamu kwa watumishi, itakayokuwa na kasi kwa kuimarisha huduma za kijamii.”amesema Rais Mwinyi

Sambamba na hivyo amesema taswira kamili ya Serikali atakayoiongoza ataitoa hivi karibuni atakapokwenda kuzindua Baraza la Wawakilishi.

Pia Rais Mwinyi amesema yuko tayari kuendeleza maridhiano na mshikamano wa Wazanzibar ulioanzishwa na watangulizi wake akiwemo Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mahamed Shein.

 “Nasimama mbele yenu kwa mara ya kwanza nikiwa Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nimekula kiapo kuwa Rais wa nane wa Zanzibar,” amesema Rais Mwinyi huku akishangiliwa kwa nguvu na umati wa watu waliojitokeza kwenye uwanja wa Amani wakishuhudia akila kiapo.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya kuifikia leo, natambua wajibu ulioko mbele yangu wa kuwaongoza Wazanzibar bila kujali dini, ukabili au maeneo wanayotoka…

“…niwapongeza na kuwashukuru sana wananchi kwa kusherekea ushindi kwa nidhamu na utulivu, hongereni sana kwa hilo. Uchaguzi ni jambo la muhimu, kwani uchaguzi ni mchakato na amani ya kudumu ni msingi wa kudumu,” amesema na kuongeza

“Nawapongeza wagombea wenzangu kwa nafasi ya urais kwa kuyapokea matokeo na kuyakubali na ninaahidi kushirikiana nao katika Serikali nitakayoiunda ili kujenga Zanzibar mpya, Zanzibar itajengwa na sisi wenyewe bila kujali itikadi zetu, Zanzibar ni kubwa kuliko tofauti zetu hivyo nipo tayari kuendeleza maridhiano na kuijenga Zanzibar yetu,” amesema

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi alimshukuru Rais Mteule wa Tanzania, John Magufuli kwa ushirikiano wake na kwamba alipenda kushiriki kushuhudia kiapo chake lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake ameshindwa kufanya hivyo.

Akitoa salama za Rais Mteule Magufuli, Rais Mwinyi amesema “Rais Magufuli anawashukuru  Wazanzibar wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwachagua viongozi, kujitokeza kwa wingi Oktoba  28, 2020 ni ukomavu wenu kwamba uchaguzi ni njia sahihi ya kuwapata viongozi watakaoiongoza nchi hii kwa miaka mitano.”

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi