loader
Makaa ya mawe Ruvuma yaajiri Watanzania 700

Makaa ya mawe Ruvuma yaajiri Watanzania 700

MAKAA ya mawe yanayochimbwa mkoani Ruvuma yameingiza zaidi ya Sh bilioni 400 na kutengeneza zaidi ya 700 kwa Watanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme alisema kiasi hicho cha fedha kimepatikana kutokana na mauzo ya madini ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 3.3 yaliyouzwa kuanzia Agosti 2017 hadi Oktoba 2020.

Alisema uchimbaji wa makaa ya mawe unafanyika katika wilaya za Songea, Mbinga na Nyasa na kwamba Mkoa wa Ruvuma una hazina kubwa ya mashapo ya makaa ya mawe yaliyofanyiwa utafiti na kampuni tatu kubwa za uchimbaji.

“Kwa mujibu wa utafiti unaoendelea kufanyika, Mkoa wa Ruvuma una mashapo ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 457, mashapo hayo tulionayo tunaweza kufanya uchimbaji kwa miaka 718 bila kumaliza hazina hii,”alisisitiza Mndeme.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa huyo alisema katika kipindi cha mwaka 2019/2020 zaidi ya tani 636,000 za makaa ya mawe yaliyochimbwa mkoani Ruvuma ziliuzwa ndani na nje ya nchi.

Alisema Mkoa wa Ruvuma una aina mbalimbali za madini yakiwemo ya dhahabu na vito vya thamani  yanayochimbwa kwa wingi katika wilaya za Tunduru, Songea, Mbinga na Nyasa.

Mndeme alisema katika Mkoa wa Ruvuma kuanzia Mei 2019 yalifunguliwa masoko ya madini ya vito na dhahabu  katika wilaya za Songea na Tunduru. Hadi sasa kupitia masoko hayo, zimeuzwa gramu zaidi ya milioni moja zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 7.7.

Alisema Watanzania zaidi ya 1,000 wamepata ajira za uchimbaji kwenye madini hayo mkoani Ruvuma.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huyo, tayari limejengwa jengo kubwa la kituo cha umahiri cha madini la mkoa litakalotumika kutoa elimu kuhusu madini kwa wachimbaji wadogo, elimu ya upatikanaji wa masoko ya madini na elimu ya utambuzi wa madini.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Songea

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi