loader
Dstv Habarileo  Mobile
​​​​​​​Udhibiti wa corona ulivyompaisha JPM

​​​​​​​Udhibiti wa corona ulivyompaisha JPM

TANGU Desemba mwaka jana kuliibuka ugonjwa wa ajabu unaosambaa kwa kasi duniani, ambao hadi hivi karibuni ulisambaa na kuambukiza watu takribani milioni 46.96, kuua watu milioni 1.2 na watu waliopata maambukizi na kupona walifikia milioni 33.85.

Ugonjwa huo unaotokana na virusi vya corona ulioanzia nchini China katika Mji wa Wuhan ulipewa jina na Shirika la Afya Duniani (WHO) la Covid-19.

Aina hiyo ya virusi vya corona mwanzoni iliitwa 2019 Novel Coronavirus (2019-nCoV) na hatimaye ikapewa jina la SARS-Cov-2 na kisha Covid-19.

Kwa mujibu wa Wikipedia, virusi vya corona huwa na uwezo wa kubadilika na aina nyingi husababisha magonjwa yasiyo hatari sana upande wa binadamu.

Hata hivyo, kutokana na kudhoofika kwa mwili kutokana na mashambulio ya virusi kunafungua milango kwa bakteria wabaya kuvamia na kusababisha maambukizi ya mfumo wa upumuaji kama mafua au homa ya mafua (influenza), yanayoisha kwa kawaida baada ya siku kadhaa.

Lakini kuna pia maambukizi ya hatari kama nimonia inayoweza kusababisha kifo.

Hadi sasa hakuna chanjo au dawa ya kudhibiti virusi vya aina hiyo. Kwa hiyo uponyaji hutegemea mara kwa mara nguvu ya kinga mwilini kwa kila mtu. Hii inamaanisha virusi hivi huleta hatari hasa kwa watu wenye kinga za mwili zilizodhoofika.

Aina hizo za virusi zina uwezo wa kubadilika, miaka ya nyuma ulikuwa na mabadiliko kadhaa yaliyosababisha vifo vya watu na kuenea haraka kimataifa, hivyo kusababisha hofu za epidemiki au hata pandemia.

Kwa sasa kirusi hicho, kinashambulia zaidi nchi za magharibi, ambako nchini Marekani inaongoza kwa kuwa na waathirika wengi wanaofikia milioni 9.56 na vifo vinavyofikia 237,009 ikifuatiwa na India ambayo ina maambukizi yanayofikia milioni 8.26 na vifo 123,139.

Hata hivyo, tangu Aprili 29, mwaka huu, Tanzania ilipotoa takwimu za maambukizi ya watu 509 na vifo vya watu 21, hadi leo hakuna taaifa ya mtu yeyote mwenye maambukizi ya ugonjwa huo wala kupoteza maisha.

Na kuanzia kipindi hicho vituo vyote vya dharura kwa ajili ya wagonjwa wenye maambukizi ya ugonjwa huo vilifungwa ikiwamo Hospitali ya Rufaa ya Amana jijini Dar es Sakaam iliyokuwa maalumu kwa ajili ya ugonjwa huo.

Mafanikio hayo ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo hadi leo yamekuwa gumzo duniani kutokana na ujasiri na uthubutu wa Rais John Magufuli wa kuhakikisha kila Mtanzania pamoja na kufuata masharti ya watalaamu wa afya, anafanya kazi kama kawaida.

Katika kipindi chote cha takribani miezi miwili cha kukabiliana na janga hilo, tofauti na nchi nyingine, Tanzania iliendelea na shughuli zake kama kawaida hususani za kiuchumi.

Hali hiyo, iliibua hisia na shutuma mbalimbali dhidi ya rais huyo kiasi cha baadhi ya wabunge wa upinzani kuamua kususia Bunge la Bajeti wakishinikiza hatua zaidi kuchukuliwa ikiwemo shughuli zote za maendeleo kusitishwa na wananchi kuzuiwa kutoka nje kama nchi nyingine zilizofanya.

Shutuma hizo hazikuishia ndani, bali hadi nje ya nchi ambapo Tanzania ilikumbana na vikwazo kadhaa ikiwemo kuwekewa mizengwe katika mipaka ya nchi jirani kutokana na suala hilo la corona.

Rais Magufuli alifikia hatua ya kufanyia majaribio vipimo vya maambukizi ya corona na kubaini kuwa vipimo hivyo vina hitilafu baada ya kuonesha maambukizi ya corona katika majimaji ya tunda la papai na mbuzi.

Hata hivyo, tofauti na watu walivyotarajia, mpaka leo Tanzania inaendelea vyema na uchumi wake haukutetereka isipokuwa katika maeneo ambayo yanahusiana na nchi nyingine kama vile usafiri wa anga, utalii na maeneo mengine.

Akizungumzia changamoto alizokabiliana nazo kutokana na msimamo wake wa kutoifunga nchi, Rais Magufuli anasema alimweka Mungu mbele na kuwataka Watanzania kwa imani zao kumuomba ili kuipusha nchi na janga hilo.

“Baba wa Taifa alikuwa haongozwi ongozwi wala kupelekeshwapelekeswa. Tukasema haiwezekani Watanzania ambao chakula chao chenyewe wanakitafuta kila siku, leo ufungiwe nyumbani,” alisema Rais Magufuli wakati wa mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu hivi karibuni.

Aliongeza, “Nikasema Watanzania wote milioni 60 wafungiwe ndani ofisini waache kwenda, hospitali ziache kufanya kazi, miradi isimame tungekuwa wapi leo?

Alisema wanaotoa maagizo ya nchi kufungwa ni wale waliozoea kutoa amri ambazo Baba wa Taifa alizikataa.

“Nikasema na mimi hapana. Nikawaomba viongozi wa dini tukafunga kwa siku tatu. Ni maajabu ya Mungu. Huu ni ushuhuda wa kweli ambao Mungu ametuonesha sisi Watanzania. Hata asiyeamini Mungu basi aamini kwa sababu hakuna corona,” alisisitiza.

Msimamo huo, ulimpatia sifa kiongozi huyo ndani na nje ya nchi ambapo walewale waliokuwa wakipinga uamuzi wake wa nchi kuendelea na shughuli zake bila wananchi kuzuiwa, walianza kuunga mkono wazo hilo.

Katika mtazamo unaofanana na wa Rais Magufuli, WHO ikaeleza kuwa jamii inapaswa kujifunza kuishi na corona huku shughuli nyingine zikiendelea kwani hakuna dalili ya kumalizika hivi karibuni.

Shirika hilo liliufananisha ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona na Ukimwi, ambao tangu uingie na kusambaa duniani, hadi leo jamii imejifunza kuishi nao na kuendelea na shughuli za kijamii na kiuchumi kama kawaida, licha ya kutopatikana kinga wala tiba mpaka sasa.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao Mei 13, mwaka huu, Mkurugenzi wa Masuala ya Dharura wa WHO, Dk Mike Ryan alisema ni muhimu dunia ikajiandaa na kujiweka tayari kwani janga hilo kwani  halina dalili ya kuondoka hivi karibuni.

Alisema jamii inapaswa kutafuta njia za jinsi ya kuishi nalo huku shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi zikiendelea.

“Nafikiri wakati umefika tuwe wakweli, sidhani kama kuna mtu anaweza kutabiri kuwa ugonjwa huu utaisha hivi karibuni. Nafikiri hakuna ahadi wala tarehe katika hili. Ugonjwa huu unaweza kuwapo kwa muda mrefu, ni jambo linalowezekana,” alisema Dk Ryan.

Pamoja na shirika hilo, mataifa mengine nayo yaliyokuwa akipinga msimamo wa Dk Magufuli yalianza kulegeza masharti na kuiga hatua zilizochukuliwa na daktari huyu wa kemia na hesabu anayeingia sasa kwenye muhula wake wa pili akiwa Rais wa Tanzania.

Aidha, hatua hiyo ya Rais Magufuli kutolegeza msimamo wa kuifunga nchi, iliungwa mkono na kupongezwa na Watanzania wengi hususani wafanyabiashara ambao wengi walieleza wazi endapo nchi ingefungwa kama nchi nyingine, mitaji yao ingekufa na wao wangekufa njaa.

Baadhi ya Watanzania hao ni pamoja na Wamachinga wa Mkoa wa Mwanza waliofanya maandamano ya kumpongeza Rais Magufuli kwa mapambano dhidi ya ugonjwa huo na kutowaweka Watanzania kwenye zuio la kutotoka nje.

Ndio maana wakati wote wa kampeni, wananchi wa Tanzania na viongozi wa dini walipongeza msimamo wake huo na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu, huku wakieleza kuwa watapampatia kura ili aendelee kuisimamia Tanzania kwa nguvu tena na kutoyumbishwa na yeyote.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/21200ce8e8778d8e475382e301eb0556.jpg

TAARIFA za matukio ya mimba na ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi