loader
Dstv Habarileo  Mobile
Miradi iliyompa kura JPM

Miradi iliyompa kura JPM

WAKATI Rais John Magufuli akijiandaa kuanza kipindi cha pili cha miaka mitano ya urais baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka huu, anajivunia moja ya silaha kubwa alizozifanya miaka mitano iliyopita ambazo zimechangia kumrejesha Ikulu.

Katika miaka mitano iliyopita, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Awamu ya Tano chini ya Dk Magufuli, imejitahidi kugusa maisha ya Watanzania kwa upana wake kwa kutekeleza miradi mbali mbali mikubwa ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, umeme, maji, elimu na afya.

Miongoni mwa miradi mikubwa ya usafirishaji ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeitekeleza na inaendelea  kuitekeleza ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) awamu ya kwanza na ya pili kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora Dodoma yenye urefu wa kilometa zaidi ya 700 kwa gharama ya Sh trilioni 7.026.

Kipande cha reli hii kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa kilometa 300, kimefikia zaidi ya asilimia 90 wakati kipande cha kutoka Morogoro hadi Makutupora Dodoma chenye urefu wa kilometa 422 kimefikia zaidi ya asilimia 40.

Meneja wa Mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Maizo Mgedzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), amewahi kuliambia gazeti hili kuwa ubora wa reli hii ni wa viwango vya juu ikilinganishwa na ubora wa reli ambazo zimeshajengwa kwenye baadhi ya nchi barani Afrika na itakuwa na uwezo wa kupitisha treni zenye uwezo wa mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa.

Mgedzi anasema reli hii itakuwa na upana wa milimita 1,435 ambao ni sawa na upana wa mita 1.435 tofauti na reli ya sasa yenye upana wa milimita 1,000 ambao ni sawa na upana wa mita moja na itakuwa na uwezo wa kupitisha mzigo wa tani kati ya milioni 17 hadi milioni 25 kwa mwaka na idadi kubwa ya abiria.

Amesema idadi ya stesheni katika reli ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Morogoro ni sita ambazo ni Dar es Salaam, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere na Morogoro. Awamu ya tatu ya ujenzi wa reli hii itakuwa kutoka Mwanza hadi Isaka ambayo Rais Magufuli amesema tayari zabuni imeshatangazwa ya kupata mkandarasi na ujenzi utaanza katika mwaka huu wa fedha.

Ukarabati wa reli

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema ukarabati wa reli ya kutoka Dar es Salaam-Tanga-Moshi-Arusha umegharimu zaidi ya Sh bilioni 14.

Kwa mujibu wa Kadogosa, kazi hii ya ukarabati imefanywa na wahandisi wazalendo wa Kitanzania kutoka TRC na mafundi mchundo na vijana 600 ambao walikuwa vibarua.

Bandari

Serikali ya Awamu ya Tano pia imefanya upanuzi wa bandari zake kuu nchini zikiwamo ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara kwa kuziboresha na kuziimarisha ili zihimili ushindani wa kibiashara katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Miongoni mwa maboresho katika bandari ya Dar es Salaam ni kujenga gati jipya la kupakulia magari, kuimarisha gati zilizokuwepo, kuongeza kina cha gati hadi kufikia mita 15 ili kuruhusu meli kubwa za mizigo kutia nanga bila tatizo pamoja na mpango wa kupanua na kuongeza kina katika lango la kuingilia meli bandarini.

Mkoani Mtwara Serikali ya Awamu Tano inajenga gati jipya namba mbili kwa gharama ya Sh bilioni 137.4. Meneja wa bandari hii, Juma Kijavara amewahi kusema kuwa sifa pekee ya gati hili ni kwamba limejengwa mahali ambako kuna kina kirefu cha maji cha asili kinachofikia mita 13 wakati maji yanapokupwa.

“Gati hili litakuwa na urefu wa mita 300 na likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye ukubwa wa tani 65,000 ikilinganishwa na gati la sasa lenye uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa tani 45,000, pia litakuwa na eneo la kuhifadhia mizigo lenye ukubwa wa mita za mraba 79,000 na uwezo wa kuhudumia tani zaidi ya milioni moja kwa mwaka,” alieleza Kijavara.

 

Serikali pia inafanya upanuzi katika Bandari ya Tanga ikiwemo kuongeza kina ili meli kubwa za mizigo na mafuta zitie nanga. Wakati anazindua safari za treni ya abiria kutoka Dar es Salaam hadi Arusha, Rais Magufuli ameweka wazi kuwa kupanuliwa kwa Bandari ya Tanga kutawezesha kuwapunguzia gharama za bidhaa wananchi wa mikoa ya kaskazini kwa kuwa baadhi ya meli kubwa za mizigo hazitalazimika kwenda Bandari ya Dar es Salaam.

Umeme

Ili kukidhi mahitaji ya umeme pamoja na kujenga uchumi wa viwanda, serikali inatekeleza ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere kwa gharama ya Sh trilioni 6.5 ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.

 

“Gharama ya umeme wetu ipo juu na uwezo wetu wa kuzalisha kwa sasa ni megawati 1,600, mradi huu wa megawati 2,115 ukikamilika tutausambaza umeme nchi nzima na tutaushusha bei kwa sababu huwezi kujenga uchumi wa viwanda kama huna umeme wa uhakika na wa gharama nafuu, mpaka sasa viwanda vipya 8,470 vimeanzishwa maeneo mbali mbali hapa nchini,” alieleza Rais Magufuli wakati wa kampeni.

Rais Magufuli anasema wakati anaingia madarakani mwaka 2015, vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa 2,018 kati ya vijiji vyote 12,280 vilivyopo, lakini serikali yake imepeleka umeme kwenye vijiji 9,700 na vimebakia vijiji 2,500 ambavyo navyo vitafikishiwa umeme katika muhula wake huu wa pili wa urais.

“Mwaka 2012, Benki ya Dunia ilisema Tanzania itaweza kufikisha umeme kwenye vijiji vyote 12,280 ifikapo mwaka 2100, mimi nasema tutapeleka umeme kwenye vijiji vyote ndani ya miaka mitano ijayo,” alieleza Rais Magufuli wakati akilihutubia Taifa kupitia Wazee wa Mkoa wa Dodoma, Oktoba 27, mwaka huu.

Bomba la Mafuta

Mradi mwingine mkubwa ambao Serikali ya Rais Magufuli imeanza kuutekeleza katika awamu yake ya kwanza ya urais ambao unatarajiwa kukamilika katika muhula wake wa pili wa urais ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani katika Bandari ya Tanga.

Rais Magufuli aliliambia Taifa hivi karibuni mjini Dodoma kuwa mkataba wa ujenzi wa bomba hili lenye urefu wa kilometa 1,445, umeshasainiwa na utagharimu Sh trilioni 8. Anasema mradi huu ni wa kwanza kwa ukubwa duniani na utapita kwenye wilaya 24 za Tanzania Bara na utatoa ajira zaidi ya 15,000.

Meli mpya

Katika kuhakikisha uchumi wa Tanzania na maisha ya Watanzania yanaboreka, serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa meli mpya na ya kisasa katika Ziwa Victoria iliyopewa jina la Mv Mwanza Hapa Kazi Tu. Kununuliwa kwa meli hii ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015-20 ukurasa wa 67 iliyoelekeza kujengwa kwa meli mpya katika Ziwa Victoria.

Wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu, Desemba mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Erick Hamisi, alimweleza Rais Magufuli kuwa meli hii inajengwa kwa gharama ya Sh bilioni 89.7 na gharama ya ujenzi wa cherezo ni Sh bilioni 36.4.

Hamisi amezitaja sifa za meli hii kuwa ina uzito wa tani 3,500 na uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400. Amefafanua kuwa meli hii itakuwa na urefu wa mita 92.6, upana mita 17, kimo mita 11.2 na itakuwa na madaraja matatu ya abiria ambapo daraja la kwanza litakuwa na uwezo wa kubeba abiria 50, daraja la pili abiria 316 na daraja la tatu abiria 834 pamoja na uwezo wa kubeba magari makubwa 3 na magari madogo 20.

“Meli hii itakuwa kubwa kuliko meli zote nchini na nchi jirani katika ukanda wa maziwa makuu. Meli ya Mv Mwanza Hapa Kazi Tu itakuwa inafanya safari zake kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Bandari ya Kemondo, Mwanza na Musoma, Mwanza na bandari za nchi jirani za Kenya na Uganda, itakuwa kichocheo kikubwa cha shughuli mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, kijamii katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za Kenya na Uganda,” alieleza Hamisi.

Anasema ujenzi wa meli hii unafanywa na kampuni ya kikandarasi kutoka Korea na utakamilika katika kipindi cha miezi 24 kuanzia Januari 2019 hadi Januari 2021.

Hivi karibuni, Dk Magufuli alisema serikali yake pia imefufua meli mbili zilizokufa kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 152 katika Ziwa Victoria, pia imenunua meli tatu Ziwa Nyasa ambazo zinafanya kazi.

Barabara na madaraja

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia toleo lao maalumu kwenye gazeti hili Oktoba 27, mwaka huu, inasema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali imeboresha miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko na viwanja vya ndege.

Wizara imesema katika kipindi hicho, jumla ya barabara zenye urefu wa kilometa 2,624.27, madaraja 10 na ukarabati wa barabra zenye urefu wa kilometa 404.7 katika mikoa mbalimbali nchini umekamilika.

Pia miaka hii mitano ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano, zaidi ya kilometa 82.6 za kupunguza msongamano katika miji zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini pia barabara zenye urefu wa kilometa 1,298.44 na madaraja saba unaendelea na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka mitatu ijayo.

Kuhusu miundombinu ya madaraja, imesema Serikali ya Magufuli imejenga madaraja makubwa 10 likiwemo Daraja la Magufuli Mto Kilombero, Daraja la Nyerere Kigamboni, Daraja la Kavuu Katavi, Sibiti Singida, Lukuledi Lindi, Ruvu Chini Pwani, Magara Manyara, Momba Rukwa, Mlalakuwa Dar es Salaam na Mara mkoani Mara.

Madaraja mengine ambayo ujenzi wake unaendelea ni Kigongo-Busisi Mwanza, Ruhuhu Ruvuma, Daraja la Tanzanite (Selander) Dar es Salaam, Daraja jipya la Wami Pwani, Kitengule Kagera, Msingi Singida na Daraja la Gerezani Dar es Salaam, huku usanifu wa Daraja la Simiyu Mwanza ukiwa umekamilika, Daraja la Mzinga Dar es Salaam usanifu wake bado unaendelea huku utaratibu wa kumpata mkandarasi wa kujenga Daraja la Pangani Tanga nao ukiendelea.

Ili kuondoa au kupunguza tatizo la foleni katika Jiji la Dar es Salaam, serikali pia imetekeleza ujenzi wa Daraja la Juu la Mfugale Tazara Dar es Salaam kwa gharama ya Sh bilioni 100, huku ujenzi wa barabara za juu Ubungo kwa gharama ya Sh bilioni 240 ukiendelea na ukiwa hatua za mwisho pamoja na upanuzi wa njia nane wa  Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kibaha Pwani yenye urefu wa kilometa 19.2 kwa gharama ya Sh bilioni 141.5 nao ukiendelea.

Usafiri wa anga

Kwa kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha maisha ya Watanzania yanaboreka kwa kuwajengea miundombinu wezeshi ikiwemo ya usafiri na usafirishaji, inafanya upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege mbalimbali nchini kikiwemo cha Mtwara, Songea na Iringa.

Miradi mingine ya viwanja vya ndege ambayo serikali inatarajia kuitekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na Kiwanja cha Ndege cha Kigoma, Musoma, Tabora, Sumbawanga na Shinyanga.

ATCL

Serikali ya Awamu ya Tano pia imeifufua Kampuni ya Ndege (ATCL) kwa kununua ndege mpya 11 kwa mpigo zikiwemo Boeing 787-8 Dreamliner mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 262 kila moja, Airbus A220-300 mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 130 kila moja, Bombardier Das 8 Q400 nne.

Ndege nane kati ya 11 zipo zinafanya kazi huku zingine tatu zikiendelea kutengenezwa kiwandani nje ya nchi. Ndege hizi zinafanya safari za ndani na nje ya nchi katika nchi mbali mbali.

Maji

Miongoni mwa mambo ambayo Rais Magufuli ameyashughulikia kwa nguvu zote ni upatikanaji wa maji safi na salama kwa Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini.

Wakati analihutubia Taifa jijini Dodoma, Rais Magufuli amesema serikali yake inatekeleza miradi 1,400 ya maji nchi nzima ukiwemo mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria jijini Mwanza kwenda Shinyanga-Nzega-Tabora hadi Igunga ambao pia utatoka Tabora-Itigi-Manyoni umbali wa kilometa 220 na kisha kufika Dodoma kilometa 127 pamoja na mradi wa Sh bilioni 520 mkoani Arusha na miradi mingine mingi kote nchini.

Elimu bure, mikopo

Katika kujali elimu ya Watanzania, Serikali ya Awamu ya Tano imetumia Sh trilioni 1.09 kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo kuanzia shule ya msingi hadi Kidato cha Nne kote nchini pamoja na kutumia Shtrilioni 2.28 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Afya

Ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya katika maeneo yao, Rais Magufuli amesema serikali yake imejenga jumla ya hospitali za rufaa tatu, hospitali 10 za rufaa za mikoa, hospitali 99 za wilaya, vituo vya afya 487, zahanati 1,198 na kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2015 hadi kufikia Sh bilioni 270.

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/91e8af051de95c38d63754d96c3bba8e.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi