loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Magufuli siri ya ushindi wa CCM

OKTOBA 29, mwaka huu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza mwanasayansi mbobevu na mgombea wa urais wa Chama Cha Mapinduzi, Dk John Magufuli kuwa mshindi wa kiti cha urais, ikiwa ni matokeo ya kura zilizopigwa na Watanzania Oktoba 28, mwaka huu.

Matokeo hayo yalimpa ushindi Magufuli ambaye pia alikuwa akitetea kiti hicho kwa kura 12,516,252 ikiwa ni sawa na asilimia 84.4 za kura halali zilizopigwa. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Magufuli alipogombea mara ya kwanza alipata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 ya kura halali.

Ushindi wa kishindo wa mwaka huu umewaibua wasomi, viongozi wa dini, wafanyabiashara na wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia nchini ambao kwa nyakati tofauti wameeleza siri ya ushindi huo kuwa ni Magufuli mwenyewe na ndiye aliyewabeba wagombea wengine kuanzia udiwani na ubunge.

Wamesema miradi mikubwa ya maendeleo aliyofanya Rais John Magufuli kwa miaka mitano ndio hasa miongoni mwa mambo yaliyowezesha ushindi huo wa kihistoria wa CCM mwaka huu.

Waligusia pia namna Magufuli kwa miaka mitano alivyorejesha imani ya Watanzania kwa serikali, pia alivyorejesha nidhamu serikalini, uwajibikaji na matumizi sahihi ya kodi zinazotokana na mapato ya ndani.

Mambo aliyofanya Rais Magufuli yametajwa kama sababu ya CCM kupata ushindi katika majimbo 256 kati ya majimbo 264 ya uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Tanzania Bara na Zanzibar).

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Deogratias Mwangoka anasema kuwa uchaguzi huu wapinzani wana mengi ya kujifunza na pia chama tawala (CCM), kwa kuwa umedhihirisha kwa wazi nini maana ya uongozi.

Mwangoka anasema aliyoyafanya Rais Magufuli yamewajengea Watanzania imani kwamba siasa si uongozi, vitisho na maneno matupu, bali vitendo na ndio matokeo ya uamuzi walioufanya kupitia masanduku ya kura.

Anasema utekelezaji wa kishindo wa Ilani ya CCM ya 2015-2020 uliodhihirisha ahadi zinatekelezeka, ulichangia kurejesha imani ya wananchi kwa kiongozi huyo (Magufuli) hivyo kuongeza ushawishi na hamasa kwa wananchi  kuchaguliwa ili kuwaletea maendeleo zaidi.

“Wapinzani wajifunze kwamba kazi kubwa ya uongozi ni kuwaletea wananchi maendeleo. Magufuli amefanya mengi ya maendeleo na kuitekeleza Ilani ya CCM sawasawa. Amegusa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara wa kada zote, mafundi na wazalishaji mbali mbali,” anasema Mwangoka.

Akizungumzia nyota ya Magufuli, Dk Watengere Kitojo ambaye ni msomi na mwanadiplomasia, anasema matokeo ya wabunge wengi wa chama hicho kuibuka na ushindi mnono, wengi wao wametembelea nyota ya Magufuli.

“Wabunge wengi wa CCM wametembelea nyota ya Magufuli, yeye ndio kiongozi mkuu mbeba maono, hata ushindi wa wabunge ambao hadi sasa wameshashinda majimbo zaidi ya 220 (wakati huo akihojiwa) umetokana na kazi alizofanya kiongozi wao,” alisema Dk Kitojo.

Anasema si kwamba wabunge hao hawakustahili kushinda, lakini imani iliyojengwa na Rais Magufuli kwa Watanzania katika serikali ya awamu ya tano, ndiyo iliyowasaidia wabunge hao kupita kwa urahisi, kwani yuko kiongozi wao anayeaminika kwa kufanya yaliyochangia kuaminika.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima, aliipongeza serikali kwa uchaguzi wa amani kwa maeneo mengi na kueleza kuwa Rais Magufuli alifanya kazi kubwa kujenga nchi na kuonesha uzalendo mkubwa hivyo kupata ushindi wa kishindo haishangazi na anastahili.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini akizungumzia ushindi huo katika mahojiano na gazeti hili, anasema Watanzania wamependa maendeleo yaliyofanywa na Dk Magufuli na kushauri watu sasa wafanye kazi ikiwa ndio msisitizo wa Magufuli wakati wote kwa kuwa uchaguzi umekwisha.

“Anayetaka watu waende barabarani kuandamana yeye aanze mstari wa mbele. Mahubiri yangu siku zote kwa vijana wasikubali kutumika, watakaotolewa jicho, mguu ni wao. Anayelalamika aende mahakamani si barabarani,” anashauri Kilaini kwa yeyote anayeona hakutendewa haki katika uchaguzi huo uliompa ridhaa ya miaka mitano mingine Magufuli.

Naye mchambuzi wa masuala ya diplomasia, Maggid Mjengwa anasema anautazama uchaguzi huu kama tathimini ya wananchi wenyewe katika kupiga kura ya kutaka maendeleo dhidi ya hoja dhaifu iliyobebwa na wapinzani kupingana na dhana ya maendeleo ya vitu isivyohusiana na maendeleo ya watu.

Mjengwa anasema huwezi kutenganisha maendeleo ya vitu na maendeleo ya watu na Watanzania wameona yaliyofanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais Magufuli na wameamua kikatiba.

Mbunge Mteule wa Mbarali, Francis Mtega alipozungumzia ushindi wake na wa CCM kwa ujumla, alisema ushindi huo wa kishindo wilayani humo ni matokeo ya wananchi kuielewa vizuri ilani ya chama hicho sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika katika miaka mitano iliyopita chini ya Rais Magufuli.

Wafanyabiashara wadogo na waendesha bodaboda katika maeneo ya Kimara na Mbezi Luis wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam, wanasema kwa nyakati tofauti kuwa Rais Magufuli amefanya mambo makubwa yaliyowabeba wagombea wengine wa CCM wa udiwani na ubunge kiasi cha kuwashawishi wawapigie kura.

Miradi inayotajwa ni ya ujenzi wa madaraja ya juu eneo la Ubungo na Tazara jijini Dar es Salaam, madaraja ya kawaida, barabara zinazounganisha mikoa kote nchini, meli, vivuko, shule, vituo vya afya, upatikanaji wa huduma za afya hasa mama na mtoto na dawa na vifaa tiba.

Mingine ni kuongezeka kwa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ulinzi wa rasilimali kwa kujenga ukuta kwa madini pekee yanayopatikana nchini ya tanzanite Mirerani, kuboresha sheria za madini, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), kufufua reli ya kaskazini Dar es Salaam-Arusha, ujenzi wa masoko na stendi za mabasi na serikali kuhamia Dodoma.

Januari 5, mwaka huu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, akizungumza na gazeti hili alisema yale yaliyofanywa na chama hicho katika sekta ya afya, elimu, madini, miundombinu ikiwamo barabara, madaraja ya juu na ya kawaida, reli (SGR), kufufua safari za treni kaskazini, meli, anga, nidhamu serikalini, mikopo elimu ya juu, wana uhakika wa kushinda kwa asilimia 70 bila kampeni na asilimia 90 wakifanya kampeni.

Polepole katika mahojiano hayo alisema mwaka huu kwao ulikuwa wa kutoa hesabu kwa Watanzania ya utekelezaji wa Ilani (2015-2020) ili wawatathimini ikiwa wanafaa kuendelea kuongoza dola au la huku ikihesabu mitaji yake mikubwa miwili kuwa ni utekelezaji wa miradi kupitia Ilani ya 2015-2020 na huduma za jamii.

Alisema CCM imefanya kazi nzuri kwenye elimu, afya (ujenzi wa vituo vya afya zaidi), miundombinu ya barabara, kilimo, usafiri na usafirishaji kuanzia kwenye maji, reli, anga, kudhibiti na kupambana na rushwa, utoaji wa haki na kote huko Watanzania wameona kazi nzuri na wanakubali kiwango cha maendeleo kilichofikiwa kwa muda mfupi.

“Huu ni mtaji mkubwa sana kuelekea kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 mwezi Oktoba. Kwa hiyo sisi tunakwenda tayari tukiwa na mtaji wa kazi nzuri sana iliyovunja rekodi ya kihistoria,” alisema Polepole.

Serikali ya Magufuli kwa miaka mitano ilifanya mageuzi makubwa ya reli ya kati kwa kuiongezea uwezo kutoka reli ya ratili 45, 50 na 60 kuwa reli ya uzito wa ratili 80 itakayowezesha kasi zaidi ya treni.

Akizungumzia madini, Polepole alisema Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, mwaka 2015 tanzanite ilikuwa kilogramu 300 kwa mwaka, lakini Agosti mwaka jana alipita na kukuta tanzanite imechimbwa kilogramu 1,955.

Polepole alitolea mfano mradi wa ujenzi wa daraja kubwa Afrika la Busisi mkoani Mwanza, wilaya za Misungwi na Sengerema zinazotenganishwa na Ziwa Victoria la urefu wa kilometa tatu litakaloondoa kero ya kusubiri kivuko kwa saa mbili wakiwamo wanaokwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

Miradi hii na mingine mingi iliyotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano, ndio hasa siri inayoelezwa kuwabeba wabunge na madiwani wa chama hicho kupata ushindi wa kishindo.

 

WILAYA ya Rungwe mkoani Mbeya ni moja kati ya wilaya ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi