loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM aapa, asema sasa  ni kuleta maendeleo

JPM aapa, asema sasa ni kuleta maendeleo

RAIS John Magufuli amekula kiapo cha kuiongoza Tanzania kwa muhula wa pili, huku akisisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na kuwa jukumu lililopo ni kujenga na kuleta maendeleo ya nchi.

Aliapishwa jana kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini hapa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, katika sherehe ambayo ilihudhuriwa na marais watatu na wageni zaidi ya 83 wa kimataifa na maelfu ya wananchi.

Akihutubia taifa baada ya kula kiapo cha kuongoza Tanzania kwa muhula wa pili wa awamu ya tano, Rais Magufuli aliahidi kukitumikia kiapo hicho kwa kuwatumikia wananchi.

“Uchaguzi sasa umekwisha, uchaguzi sasa umekwisha, uchaguzi sasa umekwisha,” alirudia maneno hayo mara tatu.

“Jukumu kubwa na muhimu lililopo mbele yetu hivi sasa ni kuendeleza jitihada za kulijenga na kuleta maendeleo kwa taifa letu. Na katika hilo niwahakikishie Watanzania wenzangu kuwa kiapo nilichokiapa hivi punde na alichoapa Makamu (Samia Suluu Hassan) tutahakikisha tunakienzi kwa nguvu zote,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema atashirikiana na watu wote bila kujali tofauti za kiitikadi, dini, kabila au rangi. Alisisitiza kutekeleza aliyoyaahidi wakati wa kampeni na yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Pia ninawaahidi bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, dini, kabila au rangi nitashirikiana nanyi wote kutekeleza yote niliyoahidi wakati wa kampeni, bado nayakumbuka tuliyoahidi na yameandikiwa katika kurasa 303 za ilani, ikiwa ni pamoja na kuendelea kulinda amani na usalama wa nchi yetu, uhuru wa nchi yetu na mipaka yetu bila kusahau Muungano pamoja na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar,” alisema.

Aliongeza, “zaidi ya hapo nitashirikiana nanyi nyote kwa karibu katika kuendeleza jitihada zetu za kujikomboa na kujenga taifa linalojitegemea na katika hilo tunaenda kukamilisha miradi mikubwa tuliyoianzisha na kwenda kuanza kutekeleza miradi mipya.”

Aidha, Rais Magufuli pia ameahidi kuimarisha usimamizi wa maliasili za nchi ikiwa ni madini, rasilimali za bahari na majini, misitu, wanyamapori na mifugo.

Alisema pia serikali yake itatekeleza kwa nguvu kubwa katika kukuza uchumi na kushughulikia changamoto za umaskini, ukosefu wa ajira hususani kwa vijana na kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Pia aliahidi kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali za umma.

Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa mataifa mbalimbali, waliofika kwenye hafla ya kuapishwa kwake na waliomtumia salama za pongezi na kuahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano.

“Uwepo wenu hapa na salama mlizotutumia, sio tu zinatupa nguvu za kuwatumikia wananchi vizuri, bali ni ishara ya uhusiano na ushirikiano uliopo kati yetu. Napenda niwahahakishie kama ilivyokuwa kwenye miaka mitano iliyopita, kwenye miaka mitano ijayo tutaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano kati yetu pamoja na taasisi mnazoziwakilisha,” alisema Rais Magufuli.

Miongoni mwa wageni walikuwapo marais Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), Azali Assoumani (Comoro) na Yoweri Museveni (Uganda) pamoja na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.

Aidha, Rais Magufuli pia aliwashukuru wagombea wenzake wa nafasi za urais na wagombea wenza wao, kwa kushiriki vizuri kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu uliompa ushindi wa kura milioni 12.5.

Pia aliwapongeza na kuwashukuru Watanzania kwa kuonyesha utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.

“Kama mjuavyo kwenye baadhi ya nchi uchaguzi umekuwa chanzo cha uhasama, migogoro na vita, sisi Watanzania kwa mara nyingine tumevuka mtihani huu salama na hivyo kuudhihirishia ulimwengu kuwa sisi Watanzania ni wapenda amani na tumekomaa kidemokrasia.

“Hii ni ishara nyingine kuwa Mungu analipenda taifa letu la Tanzania, tangu tumepata Uhuru mwaka 1961, nchi imepita kwenye mitihani mingi na Mungu ametuvusha salama...Tumshukuru sana Mungu kwa maajabu anayolifanyia taifa hili,” alisema Rais Magufuli.

Aliahidi serikali yake itajenga uwanja mkubwa, ambao utaweza kuchukua wananchi wengi wakati wa sherehe zijazo.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi