loader
Dstv Habarileo  Mobile
Macho, masikio yaelekezwa uteuzi mawaziri

Macho, masikio yaelekezwa uteuzi mawaziri

MACHO na masikio ya watu wa kada tofauti, yameelekezwa kwenye Baraza la Mawaziri litakaloundwa na Rais John Magufuli.

Wengi wao wanasema wanahitajika watu sahihi wa kubeba maono yake na kuyatekeleza kwa vitendo, kumwepusha kufanya mabadiliko ya mara kwa mara.

Miongoni mwa waliozungumza na gazeti hili, wamerejea hali ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, ambacho Rais Magufuli alilazimika kufanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kutoridhishwa na utendaji wa baadhi ya wateule wake.

Hata hivyo, wachambuzi hao wa siasa, wasomi na watu wa kawaida, wameonesha matumaini kwamba Baraza la Mawaziri litakaloteuliwa, litakuwa na watu wanaoelewa vyema majukumu yao kutokana na kuelewa juu ya nini Rais anataka.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema kutokana na ahadi alizotoa Rais Magufuli wakati wa kampeni ni wazi kuwa atataka watendaji wake kuwa wachapakazi, wabunifu na wenye uwezo wa utendaji katika nafasi walizopewa.

“Rais aliahidi awamu yake hii ya pili kuboresha zaidi maendeleo katika maeneo kama vile kilimo, masuala ya vijana, huduma za kijamii kama elimu, afya, maji na umeme lakini pia miundombinu. Ili ahadi hii itekelezwe kwa jinsi anavyotaka watendaji watakaosimamia utekelezaji lazima wawe na sifa tofauti,” alisema Dk Mbunda.

Alisema waziri au mtendaji yeyote atakayeteuliwa na rais kwa sasa, atakuwa ameshajua kiongozi aliyemchagua anataka nini. Lakini, pia rais atakuwa na uzoefu wa watu anaowataka kupitia Baraza la Mawaziri lililomaliza muda wake.

“Hata hivyo, kiukweli safari hii Rais ana uwanja mpana wa kuunda Baraza la Mawaziri kutokana na Bunge kusheheni watu wengi na wenye uwezo. Hatapata shida,” alisisitiza.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Yusuf Segere alisisitiza kuwa changamoto iliyopo ni kupata wasaidizi wa kubeba na kuyatafsiri maono ya Rais Magufuli kwa vitendo.

Mwanasiasa na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Samson Mwigamba alisema ana hakika watu wengi wameshamwelewa Rais anachotaka wateule wake wafanye.

“Nategemea atakayeteuliwa sasa, atajipima. Akiona hawezi kasi ya Rais Magufuli ni bora akamuomba amuache…sisi wananchi tunasema aendelee tu kutumbua wale watakaoshindwa kasi yake,” alisema Mwigamba.

Mwigamba ambaye amewahi kuwa mwanachama wa upinzani kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema ilizoeleka mtu alipoteuliwa uwaziri au nafasi yoyote, alikuwa na uhakika wa kukaa muda wote bila kujali utendaji wake, jambo ambalo ni tofauti katika awamu hii.

“Kwa hiyo watu walijifanyia kazi kwa mazoea wakijua hakuna wa kuwagusa. Lakini katika uongozi wa Magufuli, lazima mtu achape kazi na aoneshe tija ili kuepuka kutumbuliwa…Amerejesha falsafa ya cheo ni dhamana. Watu waache kufanya kazi kwa mazoea,” alisema.

Alisema watakaoteuliwa hawana budi kujitathimini juu ya uchapakazi, uzalendo, uwazi, ubunifu, uwajibikaji wao na kuhakikisha wanakuwa na nidhamu ya utumishi wa umma.

Magufuli alivyotumbua

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) mkoani Iringa, Profesa Gaudence Mpangala alisema tegemeo kubwa la Baraza la Mawaziri ni kuwa na mawaziri wachapakazi wanaoendana na sifa anazotaka Rais Magufuli.

Alisema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa katika awamu ya kwanza, Dk Magufuli alitumbua mawaziri na watendaji wengi, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Tanzania.

Katika miaka mitano ya uongozi wake, Rais Magufuli alifanya mabadiliko madogo kwenye baraza lake takribani kila mwaka ama kwa kutengua uteuzi wa baadhi ya mawaziri/manaibu na kuteua wengine au kuwabadilisha wizara.

Mwaka 2016

Ikiwa imepita miezi takribani sita tangu alipotangaza Baraza la Mawaziri la kwanza Desemba 10, 2015, Magufuli alitengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga. 

2017

Machi 2017 alitengua uteuzi wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye. Vile vile alifanya mabadiliko madogo kwa kumteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Pia alimteua Dk Harrison Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mei 25, 2017, alitengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Oktoba mwaka huo alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kwa kugawanya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na ya Nishati na Madini na kuongeza wizara mpya mbili na kufikisha wizara 21. Katika mabadiliko hayo, mawaziri wawili na naibu mawaziri waliongezwa.

Wakati huo huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe uteuzi wake ulitenguliwa na nafasi yake ilichukuliwa na Dk Hamis Kigwangalla aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Afya. Pia Gerson Lwenge nafasi yake ya Waziri wa Maji ilichukuliwa na Mbunge wa Katavi, Issack Kamwelwe aliyekuwa naibu wa wizara hiyo.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura nafasi yake ilichukuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Juliana Shonza. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani pia aliondolewa na nafasi yake ilichukuliwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga.

2018

Julai Mosi, 2018, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Dk Mwigulu Nchemba wa uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Hasunga alihamishwa kutoka unaibu Waziri wa Maliasili na Utalii na kuwa Waziri wa Kilimo, baada ya waziri Dk Charles Tizeba uteuzi wake kutenguliwa. 

Joseph Kakunda alitoka kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi na kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji baada ya waziri Dk Charles Mwijage uteuzi wake kutenguliwa.

Constantine Kanyasu aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Dk Mary Mwanjelwa alihamishwa kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

2019

Juni, 2019, Rais Magufuli alimteua Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara na kuchukua nafasi ya Kakunda ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Mwezi uliofuata alimteua Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe kuwa Naibu Waziri wa Kilimo kuchukua nafasi ya Bashungwa. Mbunge wa Bumbuli, January Makamba uteuzi wake wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ulitenguliwa na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene aliteuliwa kumrithi Makamba.

2020

Januari 23, 2020 alitengua uteuzi wa Kangi Lugola wa uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, na nafasi yake ikashikwa na Simbachawene. Vile vile Mbunge wa Ilala, Azzan Zungu aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Uteuzi baada ya kuapa

Waziri Mkuu, mawaziri na naibu mawaziri walifikia ukomo utumishi wao juzi, baada ya Rais Magufuli kuapa kuongoza kipindi kingine hivyo nafasi zao ziko wazi.

Kwa mujibu wa Katiba, baada ya kushika madaraka, Rais kabla ya kuteua mawaziri, atamteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka katika jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi bungeni kuwa Waziri Mkuu.

Mbunge huyo hatashika madaraka hayo mpaka kwanza uteuzi wake uwe umethibitishwa na Bunge, kwa azimio litakaloungwa mkono na kura za wabunge walio wengi.

Baada ya hapo, Baraza la Mawaziri litaundwa kwa kuteuliwa na rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu, ambapo pia naibu mawaziri, rais anaweza kuwateua baada ya kushauriana na Waziri Mkuu. Katiba inaeleza kuwa mawaziri na naibu mawaziri wote watateuliwa kutoka miongoni mwa wabunge.

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi