loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli awashukuru  waumini Chamwino

Magufuli awashukuru waumini Chamwino

RAIS John Magufuli amewashukuru waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu-Chamwino kwa kuanzisha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa Chamwino.

Ujenzi wa msikiti huo mkoani Dodoma umekamilika na waumini wa dini ya Kiislamu wameanza kuutumia.

Rais Magufuli alitoa shukrani hizo jana katika Misa Takatifu ya Jumapili ya 32 ya Mwaka “A” iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Paul Mapalala.

Magufuli alisali ibada ya kwanza ya Jumapili tangu aapishwe kuwa Rais wa Tanzania kwa kipindi cha pili chga miaka mitano.

Novemba tano mwaka huu Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma alimuapisha kwenye uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma ili endelee na madaraka hayo.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa katika misa hiyo Magufuli alikuwa na mkewe Mama Janeth Magufuli

Aliwashukuru pia waumini wa madhehebu mengine waliochangia ujenzi wa msikiti huo na Kanisa la Bikira Maria Imakulata Ikulu-Chamwino ambalo ujenzi wake ulifanyika kabla.

Kwa mujibu wa Rais, michango hiyo inadhihirisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati wa Watanzania.

Aliwashukuru waumini wa madhehebu yote kwa sala na dua za kuombea mchakato wa Uchaguzi Mkuu tangu wakati wa kampeni hadi kuapishwa kwake.

Magufuli alisema kanisani hapo kuwa, kuchaguliwa kwake kuwa Rais ni ushindi wa Watanzania wote.

Aliwaomba viongozi wa dini na Watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa na kuiombea Serikali anayoiongoza ili itekeleze ahadi zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020/25 zenye lengo la kujenga uchumi imara na ustawi wa jamii.

Kabla ya kuanza kujengwa msikiti huo Rais Magufuli aliendesha harambee kanisani hapo Chamwino kwa ajili ya ujenzi huo.

Katika harambee hiyo waumini Wakatoliki na wa madhehebu mengine walichangia zaidi ya Sh milioni 48, mifuko ya saruji 48 na malori matano ya mchanga.

Magufuli alisema mahali ambako ni makao makuu ya nchi ni lazima paende na Mungu na kabla ya harambee hiyo alimuomba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Beatus Kinyaiya amruhusu afanye uchangishaji wa ujenzi wa msikiti.

"Kama tulivyoanza kuchangia kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa kanisa hili, nakuomba sana kama utaniruhusu Askofu na kama sitakukwaza tuchange angalau tuanze kujenga msikiti wa ndugu zetu Waislamu."alisema Rais Magufuli na kuongeza;

"Msikiti wao ni mdogo na wapo pale kwa ajili ya kumtukuza Mungu, kuna baadhi ya wasaidizi wangu wengine ni Waislamu, kuna Alhaji humu kwenye wasaidizi wangu ninapoingia humu (kanisani) lazima aingie lakini inapofika siku yake ya kwenda kumtukuza Mungu anaenda na nimeambiwa ule msikiti haujawa mkubwa."

Wakati wa uzinduzi wa msikiti huo wa Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Rais Magufuli aliagiza Sh milioni 1.133 zilizobaki kwenye ujenzi kiwe kianzio cha kujenga kanisa la Wasabato Chamwino.

“Tulianza kujenga nyumba ya ibada kwa wanaosali Jumapili, na sasa tumekamilisha kwa wanaosali Ijumaa, sasa tunakwenda kujenga kwa wanaosali Jumamosi, nataka nyumba za ibada zote zinazozunguka Ikulu ziwe za hadhi,”alisema.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi