loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM atoa neno mawaziri wapya

JPM atoa neno mawaziri wapya

RAIS John Magufuli amesema wazi kuwa atabadili sura ya Baraza la Mawaziri kutokana na wabunge wapya kuwapo wengi, lakini akawatoa wasiwasi wateule wake wengi wasiopigiwa kura, akisema hatarajii kuwabadilisha.

Amesema watendaji pekee atakaowaondoa kwenye nafasi zao ni wale wanaostaafu, wasiochapa kazi na wasioendana na kasi yake.

Rais Magufuli ambaye hivi karibuni ameshinda tena nafasi ya urais kwa kupata kura milioni 12.5, alitoa msimamo wake huo Ikulu, Chamwino wakati akimuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi.

Aliwataja watu hao ambao hatawabadili kuwa ni Katibu Mkuu Kiongozi, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wakurugenzi na watendaji wengine serikalini hadi ngazi za vijiji.

Akifafanua sababu ya kutoa kauli hiyo alisema: “Nilitaka nichomekee hapa, kumekuwa na tabia kila serikali mpya au awamu nyingine inapoingia watu wanakuwa na hofu hasa watendaji ndani ya serikali kwamba kunatokea mabadiliko. Sasa wakuu wa mikoa na wilaya wana hofu sana, nawashangaa kwa nini wanakuwa na hofu,” alihoji Rais.

“Kama mafanikio ya serikali ni pamoja na watu, kama ushindi wa asilimia 84 (ushindi wake wa urais) ni pamoja na wao wamewezesha kwa kufanya kazi vizuri katika maeneo yao.

“Wanasiasa ambao tumeguswa na hili, mimi rais na makamu wangu, waziri mkuu na mawaziri, mwingine atakayeguswa ni spika na naibu ambao sisi tunapigiwa kura. Sasa mkuu wa mkoa unakuwa na wasiwasi gani ‘unless performance’ yako haikuwa nzuri. Napata meseji kuwa mkuu wa mkoa anasema nimefanya vizuri kwenye kipindi chako,” alifafanua Rais Magufuli.

Alisema kuna uwezekano kusitokee mabadiliko hata ya mtu mmoja na akahoji “kwa nini nibadilishe Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, DAS (Katibu Tawala wa Wilaya) mkurugenzi, serikali ni ileile, mtu ni yuleyule. Najua wananisikia, wachape kazi, wasipochapa kazi shauri zao. Labda waandike barua ya kuondoka, mi najua nilianza nao namaliza nao. Makatibu wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi ni walewale sasa wasiwasi wa nini”.

Badala yake, Rais Magufuli aliweka wazi kuwa atafanya mabadiliko kwenye nafasi za uwaziri na manaibu tu ambako wapo watakaorudi na wengine kuondolewa kabisa.

Alisisitiza kuwa kwenye hilo hataki kusema uongo kwani lazima atafanya mabadiliko kutokana na wabunge wapya kuwepo wengi aliokwenda nao kuomba kura na wenye uwezo wa kazi.

Katika Bunge la 12 linaloanza vikao vyake leo jijini Dodoma, CCM wapo wabunge wa majimbo 256 na wa Viti Maalumu 94, hivyo Rais anao wigo mpana wa kuchagua mawaziri wake miongoni mwa hao.

Alitoa wito kwa watendaji wa serikali kuendelea kuchapa kazi kwani ataendelea kuwa nao kwenye utendaji kutokana na kuwaona wanafaa, isipokuwa wale watakaostaafu au utendaji wao hauendani na kasi yake.

Rais Magufuli alisema: “Kuapisha kunachosha, uanze kuapisha wakuu wa mikoa 26, Ras 26, siwezi. Nitaapisha yule atakayejiondoa mwenyewe. Mchape kazi msiwe na wasiwasi. Tukatatue shida za wananchi.”

 

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi