loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM amtaka Mwanasheria  Mkuu kujipanga vyema

JPM amtaka Mwanasheria Mkuu kujipanga vyema

RAIS John Magufuli amemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi ajipange na ahakikishe anaisimamia vizuri ofisi yake kwa maslahi ya Watanzania.

Akizungumza baada ya kumwapisha Profesa Kilangi kuendelea na wadhifa huo Ikulu jana, Chamwino, Rais Magufuli alisema: “Ukajipange kweli kweli na ukaisimamie vizuri ofisi yako ili yale yanayohusu maslahi makubwa ya Watanzania ukayashughulikie kikamilifu kwa sababu kazi hii ni dhamana na dhamana hii sisi tumekupa kwa niaba ya Watanzania.

Alisema Watanzania wanapenda kuona mafanikio katika kazi yake na wasingependa kuona kesi za serikali kila mara zinashindwa wakati Mwanasherika Mkuu wa Serikali yupo.

“Katika kipindi chako cha mwanzo ulijitahidi kufanya kazi vizuri, ndio maana tumekupa tena hii nafasi ili ukafanye vizuri zaidi, kikubwa ukamtangulize Mungu katika majukumu yako, maana mimi naamini uwezo unao, Mungu yupo, nina uhakika utafanya makubwa zaidi,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza: “Nina uhakika Watanzania wenzangu na hasa maskini watapenda kuona kesi ambazo zinazopelekwa mahakamani, zinazohusu serikali, zinazohusu mali zao zinatetewa kwa haraka na zinapata ufumbuzi mapema.”

Profesa Kilangi aliyeteuliwa Novemba 5, mwaka huu kushika tena wadhifa huo, aliapa kiapo cha uaminifu na uadilifu na aliahidi kuzishughulikia changamoto za kiutendaji ndani ya serikali na katika ofisi yake.

Anakuwa mtendaji wa kwanza katika muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Tano kuteuliwa na kula kiapo tangu Rais Magufuli ashinde Uchaguzi Mkuu. Kuteuliwa na kuapa kwake ni kuashirikia kuanza shughuli za kiserikali.

Profesa Kilangi alisema anapoanza majukumu tena anaanza akiwa na uelewa zaidi wa majukumu ya nafasi hiyo na changamoto zilizopo.

“Mheshimiwa Rais ninapoanza kipindi cha pili katika majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ninaanza majukumu haya nikiwa na uelewa zaidi juu ya nini majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini pia kuhusu changamoto ambazo pengine kwa aina moja au nyingine nitakabiliana nazo,” alisema Prpfesa Kilangi.

 

Aliongeza: “Kama nilivyosema nimeielewa zaidi hali halisi, naziona changamoto bado zipo za kiutendaji serikalini, changamoto ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu. Tunakushukuru kwa mabadiliko makubwa uliyoyafanya mwaka 2018, lakini naona bado changamoto katika ofisi mbalimbali za sheria katika serikali yetu.”

Aliahidi kuzifanyia kazi changamoto kwenye ofisi hizo kwa akili yake yote, kwa nguvu zake zote, na kwa uwezo wake wote.

“Nimeiona nia ya serikali yako ya kuleta maendeleo kwa watu na kwa haraka zaidi, na pia kupunguza utegemezi, lakini sikujua kwamba ulitangaza nia hizo kumbe wakati huo huo unakuwa umetangaza vita na vita hiyo inaibua mapambano ya kisheria na tunajua kwamba vita hiyo na mapambano hayo yanapigwanwa ndani na nje ya nchi,” alisema Profesa Kilangi.

Profesa Kilangi aliteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2018 kuchukua nafasi hiyo iliyokuwa inashikiliwa na George Masaju ambaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan pamoja na kumpongeza Profesa Kilangi kwa kuteuliwa, aliahidi kumpa ushirikiano na kubainisha kuwa imani aliyoionesha katika utendaji kazi ndio umempa imani Rais ya kumteua.

Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma alimshauri ahakikishe sheria zinawasaidia na kuwawezesha maskini.

“Shughuli za kisasa, kiuchumi na kijamii zote zinaongoza kwa sheria na wewe ndio msimamizi mkuu wa sheria. Baada ya uchaguzi kuna ilani ambayo itakuja mbele yako ili uitafsiri katika muktadha wa kisheria, sasa unapoitafsiri wakumbuke watu maskini kwa sababu mara nyingi watu maskini wamekuwa wanaachwa katika tafsiri zetu za kisheria,” alisema Jaji Mkuu.

Spika wa Bunge la 11, Job Ndugai alimhakikishia Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa atapata ushirikiano wa Bunge ambalo linamtegemea kwa ushauri.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi