loader
Dstv Habarileo  Mobile
Rais wa Comoro  aipongeza Tanzania

Rais wa Comoro aipongeza Tanzania

RAIS wa Visiwa vya Comoro, Azali Assouman ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanya uchaguzi huru, wa amani na haki.

Rais Assouman ameipongeza Tanzania jana jijini Dar es Salaam alipokuwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) tayari kuondoka nchini na kurejea Comoro, baada ya kushuhudia uapisho wa Rais John Magufuli uliofanyika Novemba 5, mwaka huu jijini Dodoma.

Rais Assouman alisema Tanzania ni nchi ya amani na utulivu wa kisiasa, kwani wakati wote wa tukio la kuapishwa kwa Dk Magufuli, aliona mambo ambayo yanapaswa kuigwa na mataifa mengine hususan kwenye nyakati za uchaguzi.

“Kwa kweli tangu nimefika hapa Tanzania nimeona mambo mazuri na ambayo tunapaswa kuyaiga sisi viongozi wa mataifa mengine,” alisema Rais Assouman, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrka Mashariki jana.

Mbali na kujifunza masuala mbali mbali ikiwemo ya uchaguzi, pia Rais Assouman aliahidi ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika nyanja za mbali mbali ikiwemo diplomasia ya uchumi, biashara, uwekezaji na utalii.

“Najisikia niko nyumbani kwa sababu uhusiano wetu umeimarishwa zaidi, mahusiano yetu yamekuwa katika masuala ya kijamii, utamaduni, biashara na mambo mengine mengi,” alibainisha Rais Assouman.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Sylvester Mabumba alisema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Comoro katika kuhakikisha kuwa sera ya uchumi wa nchi zote mbili unakua zaidi.

“Sisi tutaendelea kushirikiana vyema na Comoro kibiashara ili kukuza Sera ya 2025 tunaifikia ipasavyo kwa kuhakikisha kuwa uchumi wetu unafikia kiwango cha juu sana, naamini kuwa tunapokuwa na masoko ya uhakika Viswa vya Comoro uchumi wetu utakua zaidi,” alisema Balozi Mabumba.

Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania, Dk Ahmada El Badaoui Mohammed alisema kuna fursa nyingi za kiuchumi ambazo Comoro na Tanzania zinaweza kushirikiana.

Rais Assouman aliwasili nchini Novemba 4, mwaka huu kuhudhuria hafla ya uapisho wa Rais Magufuli uliofanyika Novemba 5 na baada ya shughuli hiyo alitembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro alikojiona vivutio vya utalii.

 

Tanzania na Comoro zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo, elimu, afya, biashara na uwekezaji.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi