loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM kuzindua Bunge kesho

JPM kuzindua Bunge kesho

RAIS John Magufuli kesho anatarajiwa kuzindua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Spika Job Ndugai amebainisha hayo jana wakati akizungumza katika Kikao cha Pili cha Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 12.

“Napenda kuwataarifuni kuwa, kwenye Mkutano wa Kwanza wa Bunge jipya kama huu wa kwetu huwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anahutubia Bunge, kwa maana ya kuweka dira kwenye serikali yake kwa miaka mitano inayokuja na utekelezaji wa ilani kadiri anavyoona inafaa,” alisema Spika Ndugai.

Akaongeza: “Hotuba hii ni muhimu, lakini kupitia sisi wabunge anakuwa analihutubia Taifa, kwa hiyo naomba niwataarifuni kuwa keshokutwa siku ya Ijumaa asubuhi saa tatu kamili tunawaomba waheshimiwa wote tuwe ndani ya ukumbi huu.”

Alisema shughuli hiyo itatanguliwa na gwaride maalumu ambalo Rais Magufuli atalikagua kabla ya kuingia bungeni kuhutubia taifa na kuzindua Bunge.

“Kwa wabunge ambao mliondoka Dodoma, natoa mwito mrudi Dodoma tayari kusikiliza hotuba, tumpokee Rais wetu na tumpe kila aina ya ushirikiano, na mlikokuwa mnafikiria kuondoka msiondoke ili tumalize kazi hii kwa amani,” alisema Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa.

Rais Magufuli atahutubia Bunge hilo ambalo kwa zaidi ya asilimia 90 lina wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichoshinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 wa Rais, Wabunge na madiwani.

Kati ya majimbo ya uchaguzi 264 ya Tanzania, CCM kimeshinda majimbo 256 na kina wabunge wa Viti Maalumu 94.

Wakati akizindua Bunge la 11, Rais Magufuli alitaja maeneo 20 ambayo ni kero alizozibaini wakati akiwa kwenye kampeni na kuahidi kuzishughulikia.

Maeneo hayo ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) walioshindwa kukusanya kodi, upotevu wa mapato, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi na uzembe.

Aidha, katika sekta ya ardhi hususani migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kushamiri kwa rushwa bandarini, uwepo wa kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama.

Lingine ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hususani kushamiri ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa kushindwa kukusanya kodi hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabiashara wakubwa.

Pia huduma za afya hususani kuimarisha utoaji wa huduma, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, uhamiaji na ajira, kuimarisha sekta ya elimu, kuimarisha Jeshi la Polisi, Zimamoto, sekta ya madini, kilimo na mifugo, uvuvi, usafiri wa reli na usafiri wa anga.

Pia Rais Magufuli aliahidi kushughulikia kero wanazokumbana nazo watu wa makundi maalumu kama ya wazee, walemavu, wanawake na watoto ambao haki zao zimekuwa zikikiukwa, pamoja na wafanyakazi, wasanii na wanamichezo kuelemewa na mzigo wa kodi na maslahi yao kukandamizwa.

“Kero hizi tutazishughulikia kwa nguvu zetu zote. Wizara, ofisi na taasisi husika zijipange ipasavyo kutatua kero hizi. Nimetaja baadhi ya kero hizi ili nanyi waheshimiwa wabunge mzitambue na mshirikiane na serikali na wadau wengine tuzitatue haraka,” alisema Rais Magufuli wakati huo.

Moja ya vitu vya kukumbukwa katika hotuba hiyo, ni msemo wake wa kujipa kazi ya ‘kutumbua majipu’ alipozungumza kwa kina na kwa uchungu suala la mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

“Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu, lakini bahati mbaya halina dawa nyingine.”

“Hivyo ninaomba waheshimiwa wabunge na Watanzania wote mniombee na mniunge mkono wakati natumbua majipu haya,” alisema Rais Magufuli ambaye amefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika vita hii ikiwamo kuanzisha Mahakama ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.

Spika Ndugai jana aliendelea kuwaapisha wabunge ambao kwa asilimia kubwa ya wabunge wamekula kiapo cha uaminifu, kabla ya kuahirisha Bunge hadi leo asubuhi.

foto
Mwandishi:  Na Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi