loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM ampongeza Biden  kwa ushindi Marekani

JPM ampongeza Biden kwa ushindi Marekani

RAIS John Magufuli kwa niaba ya Watanzania amempongeza Rais mteule wa Marekani, Joe Biden na Makamu wake mteule, Kamala Harris kwa kuchaguliwa kuongoza taifa hilo.

Biden anakuwa Rais wa 46 wa Marekani na anatajiwa kuapishwa Januari 20, mwakani.

Aligombea nafasi hiyo kupitia Chama cha Democratic na kumshinda mpinzani wake mkuu, Rais Donald Trump aliyegombea kupitia chama cha Republican. Trump hadi sasa amekataa kukubali kushindwa.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Rais Magufuli alimhakikishia Rais huyo mpya wa Marekani kuwa Tanzania itaendelea kudumisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo.

“Kwa niaba ya serikali na Watanzania, nakupongeza Rais Mteule wa Marekani Joe Biden pamoja na Makamu wa Rais, Kamala Harris kutokana na ushindi wenu katika Uchaguzi Mkuu wa Marekani. Nakuhakikishia kuwa Tanzania italinda na kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi zetu,” aliandika Rais Magufuli.

Rais Magufuli anaungana na viongozi wengine Afrika na dunia kumpongeza Biden na Harris kwa ushindi wao.

Viongozi wengine Afrika waliowapongeza wateule hao ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Muhammadu Buhari (Nigeria), Uhuru Kenyatta (Kenya), George Weah (Liberia), Abdul Fattah al-Sisi (Misri), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), Nana Akufo-Addo (Ghana), Macky Sall (Senegal) na Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini).

Pia wametuma pongezi Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.

Viongozi hao wa Afrika wamezungumzia rekodi ya Biden na kueleza namna wanavyotarajia kufanya kazi naye.

Viongozi wengine duniani walimpongeza Biden ni Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Ireland, Michael Martin, Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, mawaziri wakuu wa Canada, Justin Trudeau, na Australia, Scott Morrison.

Viongozi wengine ni Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern, Waziri Mkuu wa Indonesia, Joko Widodo, Waziri Mkuu wa Japan, Yoshihide Suga, Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi, na Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan.

Biden mwenye umri wa miaka 77, alichaguliwa mara ya kwanza katika Bunge la Seneti la Marekani mwaka 1972 na kuhudumu kwa miaka 36, na kushika nafasi ya Makamu wa Rais chini ya Rais Barack Obama kwa miaka minane.

Aidha, Kamala Harris ameingia katika historia akiwa ni Makamu wa Rais mwanamke wa kwanza nchini humo.

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi