loader
Majaliwa amerudi kwa 100%

Majaliwa amerudi kwa 100%

SAFU ya juu ya uongozi wa nchi imekamilika jana, na sura tatu zilizoanza pamoja katika Serikali ya Awamu ya Tano, zimerejea kuendelea na ‘Hapa Kazi Tu’, baada ya Kassim Majaliwa kuteuliwa na kuthibitishwa kuwa Waziri Mkuu.

Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu, ulimrejesha kwa kishindo madarakani Rais John Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan kwa kushinda kura milioni 12.5 sawa na asilimia 84.4 ya kura halali zilizopigwa.

Na ilikuwa ikisubiriwa nani atakuwa Waziri Mkuu katika muhula wa pili na wa mwisho wa awamu ya tano, na kitendawili hicho kiliteguliwa jana asubuhi bungeni baada ya Rais Magufuli kuonesha imani kubwa kwa mbunge huyo wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, alipowasilisha jina lake ili lithibitishwe kwa kura na wabunge.

Rais Magufuli amemteua Majaliwa kushika wadhifa huo kwa kuzingatia Ibara ya 51 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoeleza kuwa Rais atamteua Waziri Mkuu ambaye ni mbunge kutoka katika jimbo la uchaguzi ambaye anatoka katika chama chenye wabunge wengi bungeni.

Rais Magufuli jana aliwasilisha jina la Majaliwa bungeni kupitia Mpambe wake, Kanali Bernard Mlunga ambaye aliingia akiwa na bahasha yenye karatasi iliyoandikwa jina la Waziri Mkuu.

Kanali Mlunga aliyeingia ukumbini humo saa 3:53 asubuhi, alimkabidhi Spika Ndugai bahasha hiyo kisha Ndugai akamtaka Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai kuifungua. Wakati ikifunguliwa, Spika Ndugai alieleza namna ilivyohifadhiwa kwa kufungwa kisha kupigwa mihuri sita yenye chapa ya siri.

Baada ya bahasha hiyo kufunguliwa, Spika Ndugai alisoma kile kilichoandikwa, ambako alilitaja jina la Kassim Majaliwa kuwa ndiye aliyependekezwa na Rais Magufuli kuwa Waziri Mkuu.

Bunge lamthibitisha

Akiwasilisha hoja ya serikali kuhusu kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi alisema Majaliwa ni mzoefu katika nafasi hiyo na alitumikia kwa ufanisi mkubwa nafasi hiyo katika miaka mitano iliyopita.

Alisema Majaliwa ni mtu muadilifu, asiye na makuu na ana uwezo wa kubeba na kuhimili majukumu yote yanayoendana na wadhifa wake kwa mujibu wa Katiba.

“Mwenye hekima na busara nyingine, msikivu wa hali ya juu na mchapakazi hodari, anayemudu majukumu yake katika zama hizi za uwajibikaji, mwenye uwezo wa kuchambua kwa kina na kupima hoja mbalimbali zinapojitokeza,” alisema Profesa Kilangi ambaye kama Majaliwa, naye aliteuliwa hivi karibuni kuendelea tena na wadhifa huo.

Alisema ana umahiri katika kusimamia utendaji na kudhibiti nidhamu katika utumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa na usimamizi bora wa sera za taifa na uongozi bora wa serikali katika utekelezaji wa shughuli za Bunge.

“Utendaji wake umejidhihirisha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, pia utendaji wake umejidhihirisha akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria ya Baraza la Mawaziri, yenye jukumu la kupitia mapendekezo yote ya miswada kabla ya kuwasilishwa bungeni,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akitangaza matokeo baada ya wabunge kupiga kura, Spika Ndugai alisema kura zilizopigwa ni 350 na kwamba Majaliwa amepigiwa kura zote za ndiyo sawa na asilimia 100.

“Nakupongeza sana Waziri Mkuu kwa uteuzi huu, tunamshukuru sana Rais kwa kuturudishia wewe, tumefanya kazi pamoja miaka mitano tayari tunajuana, naamini tutakuwa na ushirikiano mkubwa zaidi huku tunakokwenda na hali ya utulivu bungeni itakuwa kubwa zaidi,” alisema Ndugai.

Alisema Bunge ni sehemu ambayo siasa zinahamia kwa miaka mitano kutoka kwenye kampeni.

“Tunategemea sana mwenzetu wa shughuli za serikali bungeni, kwamba tutakuwa na ushirikiano na tuna uhakika kupitia wewe mambo ya wabunge yatafika serikalini, na kama ulivyosema hutakuwa na ubaguzi, tutakupa kila aina ya ushirikiano,” aliongeza Spika Ndugai.

Majaliwa atoa neno

Akizungumza baada ya kuthibitishwa, Waziri Mkuu Majaliwa alisema amepokea uteuzi huo kwa mikono miwili na kuahidi ushirikiano kwa wabunge wote bila kujali chama walichotoka.

“Tukio la leo (jana) limenipa mshituko na faraja kupita kiasi, sikutarajia, tulikuwa hapa sote, hakuna aliyekuwa na uhakika na hili jambo, kwa kweli lilipokuja limetushtua na mimi niendelee kushukuru kwa namna yote,” alisema.

“Pamoja utumishi wangu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mnakumbuka katika nyakati tofauti Mheshimiwa Rais alisema kwenye Baraza la Mawaziri huku nitashughulika nalo, mimi nikiwa mmoja wa wajumbe wa Baraza la Mawaziri, kwa hiyo hakuna ambaye alikuwa na uhakika, jambo hili nimelipokea kwa mikono miwili..."

Alimshukuru Rais Magufuli kwa kuendelea kumuamini ili amsaidie katika kipindi kilichopita na kinachokuja.

“Natambua maamuzi ya Rais katika maamuzi yake anaweza kumshirikisha Makamu wa Rais kwa kuwa wanafanya kazi pamoja, nitumie nafasi hiyo kumshukuru Mama Samia Suluhu Hassan kwa kushiriki kuridhia ili jina langu liweze kuja mbele ya Bunge na kuidhinishwa na wabunge ili tuweze kushiriki katika shughuli za maendeleo,” alisema.

Alimshukuru Magufuli kwa kutambua mchango wake katika kumsaidia kufanya kazi.

“Niendelee kumhakikishia kwamba matamanio yake yaliyompelekea kuleta jina hili mbele ya Bunge, matamanio yake ambayo anaamini wabunge wenzangu kwa namna mmepiga kura nyingi tunaamini nitamsaidia kazi niwahakikishie nitafanya hivyo,” alisema Waziri Mkuu.

Aliwaeleza wabunge kuwa atakapokutana na Rais Magufuli, atamshukuru tena na kumuombea kwa Mungu amuongezee afya, uwezo na busara ili aendelee kulitumikia taifa kwa weledi na atamsaidia kadiri Mungu atakavyomuwezesha.

Kura zamshtua

 “Idadi ya kura zenu mlizonipigia mmenipa changamoto sana. Haijawahi kutokea mmepiga kura kwa asilimia 100, haijawahi kutokea nawashukuru sana. Nitaendelea kushirikiana na wabunge wenzangu wote nikijua nyie ni wawakilishi wa Watanzania wanaotamani kupata maendeleo kupitia uwakilishi wenu,” alisema Majaliwa.

Aliwaahidi wabunge kuwa ataendelea kushirikiana nao wote wakiwemo wa vyama vya upinzani, kwa kuwa anatambua ni wawakilishi wa watanzania kwenye majimbo.

“Tutapita kukagua miradi na kukutana na wananchi kuona na kupokea kero na kuona namna mzuri ya kutatua changamoto zao, nitafanya hivyo kwa majimbo ya CCM na majimbo ya vyama rafiki tukijua kwamba walioko huko ni Watanzania wa vyama vyote na maendeleo bado kauli yetu hayana chama maendeleo ni ya Watanzania wote,” alisema.

Wabunge wamzungumzia

Awali kabla ya kupigwa kura, wabunge walipewa nafasi kuzungumzia Majaliwa wakati wa kuunga mkono hoja.

Mbunge wa Ismani, William Lukuvi alisema Majaliwa ni binadamu mwenye upendo, mchapakazi asiyekuwa na majivuno na kwa mara ya kwanza ameshuhudia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akizunguka kwenda kuwatetea wabunge nchi nzima.

“Sifa kuu ya kiongozi ni unyenyekevu, kujishusha na kusikiliza na sifa hizo Mheshimiwa Majaliwa anazo, ninaamini wote tutampitisha kwa asilimia 100 ili kuliambia taifa nini tunakwenda kukifanya kwa miaka mitano baada ya miaka mitano ya mafanikio ambayo imeleta ushindi wa kimbunga,” alisema Lukuvi. 

Mbunge wa Newala Mjini, George Mkuchika alisema Majaliwa anamfahamu vizuri na amewahi kufanya kazi wakiwa Ofisi ya Rais –Tamisemi, kwamba ni mstaarabu, msikivu, asiyejikweza, hajipendekezi na anatenda haki kwa kila mtu.  

“Katika kipindi cha miaka mitano hakubagua wabunge katika uetekelezaji wa shughuli za Bunge na ni mtu msikivu sana. Amesimamia sana katika kufufua uchumi hasa mazao ya biashara, amerejesha mamlaka ya mkonge mikononi mwa serikali. Ameratibu vizuri shughuli za wizara zote,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe.

Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete alisema Majaliwa hakuwa mbaguzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na amefanya mambo makubwa, hivyo alimpongeza Rais Magufuli kwa kuwarejeshea, kwani anastahiki kuwa Waziri Mkuu na hakuna anayeweza kupinga jambo hilo.  

Mbunge wa Viti Maalumu, Fakharia Shomari alimshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi alioufanya katika nafasi ya Waziri Mkuu kwa sababu ni uteuzi ambao walikuwa wanaufikiria, ila hawakuweza kuamua kabla ya yeye kutamka.  

Mbunge wa Tunduma, David Silinde alisema Majaliwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kusimamia maono ya Rais Magufuli katika kuibadilisha nchi na pia ana uwezo wa kuunganisha nchi yote kupitia Bunge na hivyo kufanya kazi ya rais kuwa nyepesi.

Mbunge wa Bumbuli, January Makamba alisema Majaliwa ni kiongozi msikivu, muadilifu, mnyenyekevu, hodari, mchapakazi na shupavu ambaye nafasi hiyo anaimudu na anaiweza na hakuna shaka yoyote ataitendea haki.

Historia ya Majaliwa

Majaliwa Kassim Majaliwa alizaliwa Desemba 22, 1960 mkoani Lindi, na kusoma Shule ya Msingi ya Mnacho, kati ya mwaka 1970 na 1976. Alijiunga na Shule ya Sekondari Kigonsera mkoani Ruvuma kati ya mwaka 1977 na 1980.

Baada ya hapo, alijiunga katika Chuo cha Ualimu Mtwara kati ya mwaka 1991 na 1993 kisha mwaka 1994 alijiunga na Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) ambako alisomea ualimu kisha kuhitimu mwaka 1998.  Mwaka 1999 alijiunga na Chuo Kikuu cha Stockholm nchini Sweden kwa masomo ya stashahada ya uzamili.

Kuanzia mwaka 1984, Majaliwa ametumikia nafasi mbalimbali za utumishi serikalini ikiwemo kufundisha shule mbalimbali mkoani Lindi.

Vilevile aliwahi kuwa Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya na baadaye mkoa, kisha aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani mwaka 2006 na Urambo mkoani Tabora.

Majaliwa alijitosa kwenye uwanja wa siasa mwaka 2010, alipopitishwa CCM kugombea Jimbo la Ruangwa. Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 2010, alimwangusha mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Abubakar Kondo baada ya kupata kura 27,671 sawa na asilimia 72.98 dhidi ya kura 9,024 sawa na asilimia 23.8 alizopata Abubakar.

Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri Tamisemi akisimamia elimu.

Mbali na uwanja wa siasa, Majaliwa ni mwanamichezo mahiri hususan mpira wa miguu ambako amechukua mafunzo ya ukocha akiwa na leseni daraja A yenye uwezo wa kufundisha timu ya soka daraja lolote.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4fbf87269ea27540a41b8286338d4f64.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi