loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hotuba ya kihistoria

Hotuba ya kihistoria

NI hotuba ya kihistoria. Ndivyo unavyoweza kusema kuielezea hotuba ya Rais John Magufuli jana, alipozindua Bunge la 12 jijini Dodoma.

Rais Magufuli amezindua rasmi Bunge la 12 na kutoa mwelekeo na dira ya muhula wa pili wa Serikali yake ya Awamu ya Tano katika kuboresha hali ya maisha ya Watanzania na uchumi kwa ujumla.

Katika hotuba yake iliyodumu kwa saa 1:22, Rais Magufuli alisema pamoja na serikali yake kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025 yenye ukurasa 303, pia itaendelea kutekeleza na kusimamia mambo yote aliyoyaeleza katika hotuba yake aliyoitoa Novemba 20, 2015 alipozindua Bunge la 11.

“Niliyoyasema Novemba 20, 2015 wakati nazindua Bunge la 11 yalitoa falsafa, dira na vipaumbele vya awamu ya tano. Yapo tuliyoyatekeleza, yapo mengi hatujayatekeleza na yapo yaliyo katika hatua za utekelezaji,” alieleza.

Alisema mambo muhimu yaliyopewa kipaumbele katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni pamoja na kulinda na kudumisha tunu za taifa ambazo ni amani, umoja na mshikamano, uhuru wa nchi na kulinda Muungano wa Zanzibar.

“Na katika hilo, naahidi kushirikiana kwa karibu sana na Rais mpya wa Zanzibar, Mheshimiwa Dk Hussein Mwinyi. Kamwe, hatutakuwa na mzaha na yeyote mwenye kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu; mwenye nia ya kuvuruga umoja na mshikamano wetu; na pia mwenye kutaka kutishia Uhuru wetu, Muungano na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,” alisema Rais Magufuli.

“Namuahidi Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwenye miaka mitano ijayo serikali itatoa ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Zanzibar. Tutafanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuleta maendeleo kwa pande zote za Muungano,” alisisitiza Rais Magufuli katika shughuli ambayo pia ilihudhuriwa na Dk Mwinyi.

Alisema serikali yake itaimarisha utawala bora na kusimamia nidhamu, kupambana na rushwa, wizi ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

“Kwenye miaka mitano iliyopita tuliwachukulia hatua watumishi 33,555 na kuiwezesha nchi yetu kushika nafasi ya kwanza kati ya nchi 35 za Afrika kwa kupambana na rushwa kwa mujibu wa Transparency International. Na pia kushika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 duniani kwa matumizi mazuri ya fedha za umma kwa mujibu wa utafiti wa Jukwaa la Uchumi la Dunia wa mwaka 2019,” alisema.

Rais Magufuli alitaja kipaumbele kingine cha serikali yake kwa miaka mitano ijayo kuwa ni kuendelea kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania.

“Hata hivyo, kwa upande mwingine, tutaendelea kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wetu wote ili yaendane na hali halisi ya maisha ya Watanzania. Kwa hiyo, watumishi wasiwe na wasiwasi,” alieleza.

Alisema pia serikali imejipanga kuendeleza jitihada za kukuza uchumi ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali hiyo ilijitahidi kusimamia vizuri uchumi huo ambao ulikua kwa wastani kwa asilimia saba.

Alisema katika miaka mitano ijayo serikali itaendeleza mafanikio ya kiuchumi, yaliyopatikana na kuhakikisha ukuaji wa uchumi unawanufaisha wananchi hususani kwa kuinua vipato vyao, kupunguza umasikini na tatizo la ajira.

Alisema serikali inalenga kukuza uchumi wake kwa angalau wastani wa asilimia nane kwa mwaka. Itatengeneza pia ajira mpya milioni nane.

Aidha, alisema serikali itaendelea kuboresha sera za uchumi jumla na sera za fedha na kuhakikisha viashiria vyote vya uchumi ikiwamo thamani ya sarafu, mfumuko wa bei na viwango vya riba vinabaki kwenye hali ya utulivu.

Alibainisha kuwa serikali itaongeza jitihada za kuwezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba au yenye riba nafuu ikiwamo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa katika halmashauri nchini.

Serikali itawezesha utolewaji wa mikopo kupitia mifuko na programu mbalimbali za zilizoanzishwa na serikali ambayo ipo 18. Itaimarisha usimamizi wa mifuko hiyo na kuhakikisha Watanzania wanaifahamu.

Baadhi ya mifuko hiyo ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (WDF), Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) na Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali (NEDF.

Vile vile serikali itaendelea kutekeleza programu za kukuza ujuzi na maarifa ikiwamo ujasiriamali ili kuwapa ujuzi na uzoefu wananchi utakaowawezesha kupata ajira au kujiajiri ndani na nje ya nchi.

“Tutaendelea pia kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya III (TASAF) mzunguko wa pili uliozinduliwa Februari, mwaka huu utakaogharimu kiasi cha Sh trilioni 2.032. tutahakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa,” alieleza.

Pia alisema katika miaka mitano ijayo sekta binafsi itapewa umuhimu wa pekee. Alisema milango itafunguliwa na serikali kwa sekta hiyo kufanya majadiliano ili kutafuta muafaka wa migogoro ya kibiashara kwa faida ya pande zote mbili.

“Lengo letu ni kuona Tanzania inakuwa mahali pazuri pa kufanya biashara duniani,” alisema na kusisitiza kuwa serikali inataka mtu yeyote anayetaka kuwekeza nchini asiwekewe vikwazo vyovyote.

“Hatutaki mtu yeyote anayetaka kuwekeza asumbuliwe na masuala yasiyo na msingi. Tunahitaji kuwa na mabilionea wengi wa Kitanzania wakiwemo wabunge. Tunataka Watanzania wote washiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi yao,” alisema Rais Magufuli katika hotuba iliyoshangiliwa sana na wabunge.

Sambamba na kuwekeza, alitoa mwito Watanzania wahamasishwe kuweka fedha zao katika benki za nchini kusaidia benki hizo kufanya biashara na kuimarisha mzunguko wa fedha na hivyo kupunguza riba kwa wakopaji.

Rais Magufuli alisema wakati wa kufanya mambo bila woga ni sasa na kueleza kuwa katika miaka mitano iliyopita serikali ilifuta tozo 168, ambazo kati yake  114 zilihusu kilimo, mifungo na uvuvi na tozo 54 zilihusu biashara.

Alisema pia serikali imejipanga kukuza na kuboresha sekta muhimu za uchumi ambazo ni kilimo, ufugaji, uvuvi, biashara, viwanda, utalii na madini kukuza uchumi wa nchi kwa kasi na kupunguza matatizo ya umasikini na ajira.

Akizungumzia huduma za jamii, alisema serikali kwa miaka mitano itaboresha zaidi miundombinu ikiwemo kushuhulikia tatizo la msongamano kwenye miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Dodoma na kukamilisha ujenzi wa barabara za lami.

Pia itaendelea kukamilisha ujenzi wa Reli ya Kati, na kukamilisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ikiwamo kununua vichwa 39 vya treni vya njia kuu na kukarabati vichwa 31, mabehewa ya mizigo 800 na kukarabati 690 ya abiria 37 na kukarabati 60.

Upande wa usafiri wa majini, alisema serikali itakamilisha kuboresha bandari zake kuu, kununua meli kote ilikoahidi kwa mujibu wa ilani. Kwa usafiri wa anga itafanya upanuzi wa viwanja vya ndege 11 na kununua ndege mpya tano ikiwemo ndege moja ya mizigo.

Sekta nyingine zitakazoboreshwa na serikali ni nishati ambapo itakamilisha miradi ya umeme iliyopo na kusambaza umeme katika vijiji vyote vilivyobaki, utalii kwa kuhakikisha watalii wanaongezwa kutoka milioni 1.2 hadi milioni 1.5. Itaboresha pia sekta za madini, maji, elimu na afya.

“Kuhusu umeme pia, kwenye miaka mitano ijayo, tumepanga kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ambavyo bado havijafikishiwa umeme, ambapo idadi yake haizidi 2,384. Kwenye miaka mitano iliyopita, kwa takwimu za hadi jana, tumefikisha umeme kwenye vijiji 9,884; kutoka vijiji 2,018 mwaka 2016. Nchi yetu ina vijiji 12,280,” alisema.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi