loader
TIC, Uwekezaji sasa chini ya Rais

TIC, Uwekezaji sasa chini ya Rais

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na masuala yote ya uwekezaji, yamehamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais, kurahisisha masuala ya uwekezaji na kuondoa urasimu unaowatesa wawekezaji kupata vibali.

Akizungumza jana kwenye hotuba yake ya kwanza ya kulifungua Bunge la 12 jijini Dodoma jana, Rais John Magufuli pamoja na mambo mengi aliyoyaainisha, alisema kuanzia sasa anataka mwekezaji anayetaka kuwekeza nchini akishafuata utaratibu apate kibali ndani ya siku 14.

“Kumekuwepo na vikwazo vingi kwa wawekezaji ikiwemo urasimu mwingi, wawekezaji kuzungushwa na kukatishwa tamaa, nataka mwekezaji mwenye fedha zake akija apate kibali ndani ya siku 14,” alisema Rais Magufuli.

Aliendelea, “Kwa sababu hiyo nimeamua masuala ya uwekezaji na Kituo cha Uwekezaji (TIC) kuhamisha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais, ili hao wanaokwamisha nikapambane nao mimi mwenyewe.”

Awali kabla ya kuhamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na kuteuliwa Waziri wa Uwekezaji, Angella Kairuki, masuala ya uwekezaji na TIC yalikuwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Katika kipindi cha Januari 2016 hadi Juni 2020, TIC imesajili miradi 1,312 ya uwekezaji yenye mtaji wa thamani ya Dola za Marekani bilioni 20 ikiwa ni takribani Sh trilioni 46, miradi hiyo inatoa ajira kwa Watanzania 178,101.

Katika usajili huo, sekta ya usindikaji na uzalishaji wa viwanda iliongoza kwa asilimia 54 ya miradi yote na kutoa ajira kwa Watanzania 67,992.

Kituo hicho kilianzishwa mwaka 1997 kwa Sheria ya Uwekezaji Tanzania kiwe taasisi kuu ya serikali ya kuratibu, kuhimiza, kukuza na kuwezesha uwekezaji nchini Tanzania na kushauri kuhusu sera ya uwekezaji na masuala yanayohusu uwekezaji.

TIC inashughulika na uwekezaji wote wenye mtaji usiopungua Dola za Marekani 300,000 iwapo mmiliki ni mgeni au Dola za Marekani 100,000 iwapo mmiliki ni Mtanzania.

Pamoja na majukumu yake, husaidia wawekezaji wote kupata vibali, idhini na vitu muhimu vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria nyingine ili kuanzisha na kuendesha uwekezaji nchini.

Katika Baraza la Mawaziri lililomaliza muda wake, Rais Magufuli alikuwa na wizara mbili; Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/675aa68ff8131241de969d0721dbc447.jpg

UMOJA wa Vijana wa Chama ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi