loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM ataja sababu 3 za  kuingia uchumi wa kati

JPM ataja sababu 3 za kuingia uchumi wa kati

RAIS John Magufuli amesema maeneo ya kiuchumi yaliyowezesha Tanzania kuingia kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati ni kuongezeka kwa Pato Ghafi la Taifa, kudhibiti mfumuko wa bei na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa ya nje.

Aidha, amesema katika miaka mitano ijayo serikali imejipanga kuendeleza jitihada za kukuza uchumi kutoka wastani wa asilimia saba hadi asilimia nane ili manufaa yanayopatikana yawanufaishe wananchi kwa kukuza vipato vyao, kupunguza umaskini na kuwezesha upatikanaji wa ajira zikiwemo milioni nane alizoahidi.

Rais Magufuli aliyasema hayo hivi karibuni bungeni jijini Dodoma katika hotuba ya kuzindua Bunge la 12 la Tanzania. Hotuba hiyo ilitoa mwelekeo wa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Tano.

“Kwenye miaka mitano ijayo pia, tumejipanga kuendeleza jitihada za kukuza uchumi. Kama unavyofahamu, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tulijitahidi kusimamia vizuri uchumi wetu, ambapo ulikua kwa wastani wa asilimia saba kwa mwaka,” alisema Rais Magufuli.

Julai mwaka huu Tanzania ilipata sifa ya kuwa na uchumi wa kati ikiwa ni miaka mitano kabla ya kipindi kilichotarajiwa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Pato ghafi la Taifa liliongezeka kutoka Sh trilioni 94.349 mwaka 2015 hadi kufikia Sh trilioni 139.9 mwaka 2019.

Mfumuko wa bei ulidhibitiwa kutoka asilimia 6.1 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia 4.4 na kuongeza akiba ya fedha ya kigeni kutoka Dola za Marekani bilioni 4.4 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 5.2 mwezi Julai, 2020.

Rais Magufuli alisema fedha hizo zinatosha kuliwezesha Taifa kununua bidhaa na huduma kwa miezi sita.

Alisema katika miaka mitano iliyopita, mauzo ya nje yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 8.9 mwaka 2015 hadi Dola za Marekani bilioni 9.7 mwaka 2019 na pia kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 14.6 sawa na zaidi ya Sh trilioni 30.

“Aidha, tulifanikiwa kupunguza umasikini wa kipato hadi kufikia asilimia 26.4 kwa takwimu za mwaka 2017/2018. Mafanikio haya, bila shaka, ndiyo yamewezesha, mwezi Julai 2020, nchi yetu kutangazwa kuingia kundi la nchi za uchumi wa kati kutoka kundi la nchi masikini. Na mafanikio hayo yamepatikana miaka mitano kabla ya muda uliopangwa, yaani mwaka 2025,” alisema Rais Magufuli.

Alisema katika miaka mitano ijayo serikali inakusudia kuendeleza mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana na kuhakikisha ukuaji uchumi unanufaisha wananchi hasa kwa kuinua vipato vyao, kupunguza umaskini na tatizo la ajira.

“Na katika hilo, tunalenga kukuza uchumi wetu kwa wastani wa angalau asilimia 8 kwa mwaka na pia kutengeneza ajira mpya zipatazo milioni nane. Tutaendelea pia kuboresha sera zetu za uchumi jumla na sera za fedha na pia kuhakikisha viashiria vyote vya uchumi; ikiwemo thamani ya sarafu yetu, mfumuko wa bei pamoja na viwango vya riba; vinabaki kwenye hali ya utulivu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema pia kuwa serikali itaongeza jitihada za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba ama yenye riba nafuu, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri zote nchini na pia kupitia mifuko na programu mbalimbali zilizoanzishwa na serikali ambayo kwa idadi zipo 18.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi