loader
Dstv Habarileo  Mobile
Walanguzi saruji kunyang’anywa leseni

Walanguzi saruji kunyang’anywa leseni

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela amewaonya wauzaji wa saruji kwa jumla na rejareja kuwa wasipouza kwa bei elekezi iliyowekwa na serikali watafutiwa leseni.

Alitoa onyo hilo wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kutaka wakuu wa mikoa wachunguze kwa nini bei ilipanda na wampe taarifa ifikapo kesho.

Shigela alisema wauzaji saruji watakaobainika kuuza bidhaa hiyo kwa kuongeza bei watachuliwa hatua kali kama wahujumu uchumi kwa kuwa hadi sasa serikali haijaongeza kodi kwenye bidhaa hiyo.

“Haiwezekani kwa sasa wakati ambapo serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ambayo inahitaji matumizi ya saruji kwa wingi halafu lijitokeze kundi la watu wachache ambalo linataka kunufaika kinyume na utaratibu,” alisema na kuongeza kuwa ni marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kwenye mkoa huo kupandisha bei ya saruji na kama anataka kufungiwa auze kwa bei anayoitaka yeye.

“Nimeshawaagiza ma-DC, wakurugenzi wa halmashauri pamoja na maofisa biashara kuhakikisha wanafanya ukaguzi katika maduka na maghala ya kuhifadhi saruji ili kujiridhisha na upatikanaji wa bidhaa hiyo pamoja na bei,” alisema.

Shigela alisema hivi karibuni alifanya ziara ya kutembelea viwanda vinavyozalisha saruji mkoani Tanga kuona hali ya uzalishaji na kujiridhisha na namna walivyojipanga katika uzalishaji.

“Wenye viwanda wamenithibitishia kwamba hakuna uhaba wa saruji, walikuwa kwenye matengenezo ya mitambo lakini haikuchangia upungufu wa bidhaa kwani walizalisha zaidi ya kiwango kinachohitajika,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara waache propaganda za kulazimisha kuwa saruji imeadimika wakati viwandani uzalishaji unaendelea.

Gazeti hili jana lilipita katika baadhi ya maduka ya wauzaji wa bidhaa hiyo na kujionea bei imeshuka kutoka Sh 19,000 hadi Sh 14,000 kwa mfuko mmoja.

Mfanyabiashara Ali Haroun alisema kupanda kwa bidhaa hiyo kulitokana na taarifa walizozipata kwa wenzao kuwa wemepandisha na wao wakaona waongeze bei.

“Hatukuwa na uhaba ila unajua sisi wafanyabiashara tunapeana taarifa pindi ambapo sehemu fulani biadhaa inakuwa haba na hivyo kuazimia kuongeza bei,” alisema Haroun.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella jana alisema hali ya upatikanaji saruji jijini humo ni nzuri na kwa sasa inauzwa Sh 19,000 kwa mfuko ingawa bei imekuwa ikiongezeka kati ya Sh 100 na 200.

Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwa mawakala watatu wakubwa wanaosambaza saruji Mwanza, alisema haijapanda bei isipokuwa mahitaji ya bidhaa hiyo yamekuwa makubwa kuliko kiwango kinachopelekwa humo.

“Hatutaruhusu bei ya saruji kupanda kwa sababu yoyote ile, kimsingi saruji inakuja ila haiji kwa kiwango kinachotakiwa, lakini nitoe rai kwa wafanyabiashara wote tuwe makini,” alisema Mongella.

Kwa mujibu wake, bei kwa mawakala wakubwa watatu haijabadilika kwa kuwa mfuko unauzwa kati ya Sh 19,100 hadi Sh 19,200.

“Bei hiyo imekuwa inaongezeka kutokana na ubora (quality) wa aina mbalimbali za saruji, kuna ile yenye ubora wa juu na wa chini kutegemea na aina ya saruji,” alisema.

Mongella alisema baada ya wakuu wa mikoa kupokea maelekezo ya Waziri Mkuu, mambo makubwa yaliyozungumzwa na mawakala ni kuwa mahitaji ya saruji kwa mkoa wake yamekuwa makubwa.

“Na mimi nafikiri hii ndio neema ya maendeleo kwa mkoa wetu, kama mmewasikia mawakala wote, ni kwamba mahitaji ya saruji ni makubwa hii ni neema, maana yake uchumi wetu unaenda mbele,” alisema.

Aliongeza “Hili la mahitaji makubwa ya saruji katika mkoa wetu, tutalichukua tulipeleke kwa mamlaka ili tuone kama nchi tunafanyaje, maana yake nchi inaenda mbele watanzania wameamka.

Alisema anaamini viwanda vyote vikifanya kazi kwa nguvu zote mamlaka itaona juhudi hizo, Wizara ya Viwanda na Biashara na watu wa uwekezaji wataona ili wasaidie kusukuma uwekezaji uwe mkubwa zaidi kwenye sekta ya ujenzi.

Mkuuwa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alikiri kupanda kwa gharama ya saruji katika mkoa huo kutoka bei elekezi kati ya Sh 20,000 na 20,500 hadi Sh 22,000 na 23,000.

“Baadhi yao wananiambia kwamba madereva wao wamekuwa wakikaa muda mrefu eneo la uzalishaji wakisubiri bidhaa hiyo huku wakitumia gharama kubwa ya kuishi maeneo kwa matumizi binafsi na hii ndio sababu ya kupanda kwa bidhaa hiyo,” alisema Gabriel.

Hata hivyo, alisema hakuna sababu yoyote kwa yeyote kupandisha bei ya saruji kiholela kwani ni kinyume cha sheria ya nchi na kwa kufanya hivyo wanakuwa wamefanya makosa.

Ameonya wafanyabiashara watakaokiuka tamko la serikali kuwa watakutana na mkono wa sheria hivyo wajihadhari na mienendo hiyo kwa kuwa inasababisha wanaojishughulisha na ujenzi wapate wakati mugumu.

. Imeandikwa na Amina Omari (Tanga) na Nashon Kennedy (Mwanza).

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi