loader
Majaliwa: Umeme  kipaumbele chetu

Majaliwa: Umeme kipaumbele chetu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano iko mstari wa mbele kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na wa gharama nafuu na kwa kutambua hilo imeweka vipaumbele katika sekta ya nishati nchini.

Waziri Mkuu alisema hayo katika hotuba yake ya uzinduzi wa njia ya mchepuko kupitisha maji katika handaki lenye urefu wa mita 703.6 kwenye Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) uliopo Mto Rufiji Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani jana.

Majaliwa alisema kwa kutambua hilo, serikali inahakikisha hali ya upatikanaji wa umeme inaimarika ili huduma za kijamii na maendeleo yanawafikia wananchi.

“Upatikanaji wa umeme wa bei nafuu nchini kwetu na uhakika nchini kwetu kutachochea sana ukuaji wa mapinduzi kwenye sekta ya viwanda kwa kushusha gharama za uendeshaji umeme viwandani, kukabiliana na mfumuko wa bei, kuwezesha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya Afrika Mashariki na duniani kote,” alisema Majaliwa.

Alisema kupungua kwa gharama za uendeshaji kutavutia uwekezaji mkubwa wa kati na mdogo katika sekta mbalimbali nchini kutokana na kupungua kwa gharama za umeme katika kuzalisha, uzalishaji pamoja na Watanzania wote wa mjini na vijijini ni kumudu gharama zake na bila kukatika katika na kuwezesha kufanya biashara na nchi jirani pia.

Hivyo alisema matumaini makubwa ya Watanzania kwa sasa yanatengenea kukamika kwa mradi huo mkubwa na wa kimkakati ambao ni wa kwanza na aina yake Afrika Mashariki na nchi za kusini mwa Afrika na wa nne katika Afrika.

“Naipongeza Wizara ya Nishati, Tanesco, TECU na mkandarasi kwa kutekeleza ujenzi wa mradi huu ambao utawezesha nishati ya umeme kuwa ya uhakika,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema moja katika ahadi kubwa aliyoitoa Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu pamoja na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ilikuwa kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo huo wa JNHPP ambao utazalisha megawati 2,115 za umeme ukifadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu alisema serikali itaendelea kuwaamini wataalamu wa ndani kutokana na mradi huo mkubwa kuendeshwa na kusimamiwa na wataalamu wa ndani na kusimamiwa na Mhandisi wa Kitanzania.

Alisisitiza wakandarasi na wataalamu wa ndani kuhakikisha usimamizi na ujenzi huo unakuwa na viwango na pia ukamilike kwa wakati kwani serikali imeshalipa kila hatua ya fedha kwa mkandarasi tangu ujenzi hadi ulipofika sasa.

Aidha, Waziri Mkuu alisema mradi huo utakapokamilika utasaidia kuongeza mapato kwa Tanesco pamoja na kuimarisha huduma za kijamii na kuondoa umaskini.

Aliwapongeza wafanyakazi wa Kitanzania kwenye mradi huo kwa kuwa waaminifu kwani kulingana na taarifa za mkandarasi kuwa hakuna tukio lolote la wizi lililofanyika jambo ambalo alisema ni la kujivunia kuona Watanzania ni waaminifu na wanaweza kufanya kazi sehemu yoyote ile.

Pia aliwapongeza wakandarasi wa Kampuni ya Arab Contractors na Elsewedy Electric za Misri na kuwataka kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri wao wa Umeme wa kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa wakati uliopangwa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Zena Saidi kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, alisema umeme umekuwa ni kichocheo muhimu katika kuleta maendeleo ya Watanzania.

Alisema umeme wa mradi huo utaleta faida kubwa kwa wananchi kutokana na kupata umeme kwa bei nafuu, kupunguza matumizi ya miti (mkaa)na kutunza mazingira.

Kwa upande wa manufaa ya mradi huo, Katibu Mkuu alisema hadi kufikia Oktoba 31, mwaka huu, umefanikisha kuajiri Watanzania kwa asilimia 90 ambao kati ya waajiriwa 6,364, Watanzania ni 5,728.

Aliyataja mafanikio mengine ya wizara kwa ujumla ni usambazaji wa umeme vijijini ambao kati ya vijiji 12,264 vilivyopo nchini vilivyopata umeme hadi sasa ni 9,884.

“Serikali imepanga kufikisha umeme kwenye vijiji vyote vilivyobakia ndani ya kipindi cha miaka mitatu ijayo na pia serikali, Tanesco na REA itaendelea kuingiza umeme vijijini kwa gharama ya Sh 27,000 tu,” alisema Katibu Mkuu.

Mawaziri kutoka Misri, wa Umeme na wa Nishati Jadidifu, Dk Mohamed Shaker Elmarkabi na mwenzake wa Nyumba, Dk Asim Abdelhamid Hafiz Elgazar, walisema baada ya miaka mitatu ijayo Tanzania itakuwa ndio nchi pekee inayozalisha umeme mwingi katika nchi za Afrika Mashariki na utaondoa changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri wa Nyumba alisema mradi huo unafuatiliwa kwa ukaribu na rais wa nchi yao na anatarajia kuwa utaisha kwa muda muafaka na kuwaletea manufaa wananchi wa Tanzania.

Alisema Serikali ya Misri ilitoa nafasi za mafunzo kwa Watanzania 25 katika nyanja ya umeme ambao walitakiwa kupatiwa mafunzo hayo mwanzoni mwa mwaka huu, lakini kutokana na mlipuko wa corona, mpango huo ulisimama na sasa baada ya hali kuwa nzuri watapatiwa mafunzo hayo nchini humo.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/009750ebdb7b2c47fd639f0b02cbb8ac.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Rufiji

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi