loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Ma-RC ‘wafunguka’ ushindi darasa la saba

  WAKUU wa mikoa iliyoshika moja na nafasi 10 bora kitaifa katika ufaulu wa mtihani wa darasa la saba mwaka huu wameeleza siri ya mafanikio hayo ukiwemo ushirikiano, usimamizi, motisha na utekelezaji kwa vitendo mipango wanayokubaliana.

 Mikoa iliyo kwenye 10 bora kinara ni Dar es Salaam, ikifuatiwa na Arusha, Simiyu, Katavi, Kilimanjaro, Iringa, Kagera, Morogoro, Pwani na Mwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare amesema ufuatiliaji wa karibu wa ufundishaji shuleni, vikao na wakuu wa shule na walimu wakuu wa shule za msingi vimeuwezesha mkoa huo kushika nafasi ya nane kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

 Sanare ambaye kitaaluma ni mwalimu alisema jana kuwa pia uamuzi wa kuwavua vyeo viongozi wasiowajibika na kuwapatia wengine kutoka shule hizo umekuwa chachu ya mafanikio hayo.

 Alilieleza gazeti hili kuwa wakati Rais John Magufuli alipomteua kuwa Mkuu wa Mkoa huo alikuta ufauli wa shule za msingi na sekondari ukiwa chini na hivyo akaitisha vikao na walimu wakuu na wakuu wa shule ili kuweka mikakati ya kuongeza ufaulu.

 Alisema, suala lingine lililosaidia mafanikio hayo ni kujiwekea utaratibu kila siku kabla ya kuingia ofisini kupita kwenye shule moja au mbili kuona walimu iwapo wanafika kazini muda gani, kuangalia maandalizi yao ya kazi ya ufudishaji kabla hawajingia darasani.

Aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi kwa kufanya vizuri na kushika nafasi ya tisa kitaifa na kuzishinda halmashauri zilizopo kwenye mazingira mazuri .

 Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Mhandisi Joyce Baravuga, alisema katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba ya mwaka huu mkoa huo umekuwa wa nane kitaifa kwani umepata asilimia 87.21. Mwaka jana ulipata asilimia 78 na kushika nafasi ya 16 kitaifa.

 Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella amesema umeshika nafasi ya 10 kitaifa kutokana na ushirikiano baina ya walimu, wanafunzi, wazazi na serikali.

Alisema hajaridhika mkoa huo kushika nafasi hiyo na amewataka wadau wa elimu mkoani humo wajipange zaidi ili mkoa uweze kushika nafasi ya juu zaidi.

“Ushindi huu ni changamoto kwetu, tutafakari na tujipange zaidi, nawapongeza walimu kwa kazi nzuri waliyofanya na watoto wetu kwa ufaulu waliopata na wazazi pia, kimsingi hatuwezi kuubeza ushindi huu tuliopata,” alisema Mongella jana. Alisema wanafunzi waliofaulu kwenye mtihani wa darasa la saba kitaifa mwaka huu, wote watapata fursa ya kuendelea na masomo kwa kuwa umekamilisha ujenzi wa miundombinu muhimu.

 Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Marco Gaguti, alisema matokeo ya kubaki kwenye shule 10 bora yanatokana na kufanyakazi kama timu kwa walimu, wazazi, wanafunzi na maofisa elimu ngazi zote.

Aliwapongeza watendaji wote kwa kazi kubwa waliofanya na wananchi kwa kutoa ushirikiano na msaada kwa mamlaka za shule, malezi kwa watoto na kazi kubwa walimu walioifanya kuhakikisha wanafunzi wanafauli. Gaguti alisema wamejipanga kuhakikisha wanafunzi wote 45,422 waliofaulu ambao ni sawa na asilimia 88.28 ya watahiniwa 51,457 waliofanya mtihani mkoani humo, wanaingia kidato cha kwanza.

Mwaka huu mkoa huo umeshuka kwa ufaulu baada ya kushika nafasi ya saba kitaifa kutoka nafasi ya nne mwaka jana.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta, ambaye mkoa wake umeshika nafasi ya pili kitaifa, alitaja mambo matatu yaliochangia kufanya vizuri kwa mkoa huo kuwa ni wajibikaji wa walimu, utaratibu wa mkoa kuwa na mitihani ya pamoja na uboreshaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali.

 Kimanta aliliambia HabariLeo jana kuwa, walimu mkoani humo wamewajibika ipasavyo kuhakikisha mkoa unafanya vizuri kielimu na pia pamoja na kuwa na mitihani kwa kila shule, mkoa huo una mtihani mmoja unaofanywa kwa shule zote ili kupima uelewa na uwezo wa wanafunzi.

Alisema pamoja na mikakati hiyo ya mkoa, uboreshaji wa miundombinu unaofanywa na Serikali ya Rais John Magufuli umechangia ufaulu huo ikiwamo elimu bila malipo, ujenzi wa madarasa, hamasa kupata madawati na mengine aliyosema yameleta mapinduzi katika elimu mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya viongozi wa mkoa, maofisa elimu ngazi zote, walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe na dhamira ya mkoa ni kushika nafasi ya kwanza na ndiko wanakoelekea. Mkoa huo umekuwa wanne kitaifa.

“Kilichotuwezesha kupanda nafasi ni ushirikiano, kuna mikakati tulijiwekea na wote tukaitekeleza, kwa mfano tulianzisha makambi shuleni kwa darasa la saba, la nne, kidato cha pili na cha nne”alisema na kuongeza; “Nilikuwa nakusanya mitihani ya majaribio kitaifa ya miaka iliyopita ya mikoa yote Tanzania Bara nampa Ofisa Elimu Mkoa anasambaza kwa wilaya zote.

Mwaka jana (2019) mimi kama RC (Mkuu wa Mkoa) nilitoa zaidi ya milioni kumi kama motisha kwa walimu, wanafunzi, maofisa elimu na shule zilizofanya vizuri na kwa waliofanya vizuri kwa masomo ya sanaa na sayansi,” alisema Homera.

 Kuhusu mipango walionayo kwa wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza, Homera alisema mwaka jana asilimia 97 ya waliofaulu waliripoti shuleni na mwaka huu wameongeza nguvu ya pamoja kuanzia ngazi ya familia na kuanzisha mkataba kwa bodi za shule kuhakikisha wanafunzo wote wanaripoti shuleni na kusoma mpaka wamalize kidato cha nne.

 Homera alisema mwaka 2019 walijenga shule mpya nane za sekondari na mwaka huu wamejenga nne na kufanya idadi ya shule 12 zilizojengwa kwa fedha zilizotokana na kutaifishwa kwa fedha za uvunaji haramu wa mbao mkoani humo hivyo wana uhakika wanafunzi wote waliofaulu wataingia kidato cha kwanza.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema jana kuwa, mkoa huo umefanya vizuri kwenye mtihani huo kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya walimu, wanafunzi, viongozi wa serikali na wananchi.

Mtaka alisema alisema pasipo ushirikiano ni rahisi ama kwa walimu kuvunjwa moyo, wanafunzi, wazazi na viongozi kuvunjwa moyo, lakini mshikamano walionao ni msingi wa mafanikio kwa mkoa huo ulioshika nafasi ya tatu kitaifa.

SERIKALI imewataka waliohujumu mali za vyama vya ushirika kujisalimisha ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi