MWENYEKITI wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa rasilimali hiyo watumie masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini badala ya kutorosha kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuhujumu uchumi wa nchi.
Profesa Kikula aliyasema hayo jana mjini Chunya mkoani Mbeya kwenye mafunzo ya wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji katika mikoa ya Mbeya, Chunya na Songwe.
Alisema serikali kupitia Tume ya Madini imeanzisha masoko 38 na vituo vya ununuzi wa madini 39 hivyo amewataka watume masoko na vituo husika badala ya kuyauza nje ya mfumo wa masoko.
“Kufanya biashara ya madini nje ya mfumo wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini ni kinyume na sheria, adhabu kali inatolewa, ikiwa ni pamoja na utaifishaji wa madini pamoja na vyombo vya usafiri vilivyotumika kusafirisha madini husika,” alisema Profesa Kikula.
Alisema serikali imeanzisha ofisi za maofisa madini wakazi wa mikoa na maofisa migodi wakazi kwenye mikoa yote ili kusogeza huduma kwa wananchi na kufuta kodi nyingi ambazo zilikuwa ni kero kwa wachimbaji.
Katika mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Simon Mayeka aliwataka wachimbaji watoe ushirikiano kwa serikali kupitia ofisi za maofisa madini wakazi wa mikoa kwa kuwa serikali imedhamiria kuwainua wachimbaji wadogo.
Mbunge wa Jimbo la Lupa wilayani Chunya mkoani Mbeya, Masache Kasaka aliipongeza Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawapa uelewa mpana wachimbaji wadogo.