loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Miundombinu mji wa serikali Dodoma inavyosukwa kisasa

BAADA ya Dodoma kuwa rasmi Makao Makuu ya Serikali, Aprili 13 mwaka jana, Rais John Magufuli alizindua ujenzi wa mji wa serikali wa Mtumba, uliopo katika Kata ya Ihumwa, umbali wa takribani kilomita 17 kutoka katikati ya mji wa Dodoma.

 

Eneo lililotengwa kwa ajili ya mji wa serikali lina ukubwa wa hekta 617.15, sawa na ekari 1,542.88. Mji wa serikali kwa upande wa magharibi unapakana na Ihumwa, kaskazini mashariki unapakana na kata ya Mtumba na upande wa kusini unapakana na barabara kuu iendayo Morogoro - Dar es Salaam.

 

Mji huo umegawanyika katika maeneo tofauti kama wizara za serikali, ofisi za mabalozi, nyumba za serikali, huduma za jamii, maeneo ya biashara, mahakama, maegesho ya magari na eneo la majitaka.

 

Takwimu zinaonesha makadirio ya gharama za kukamilisha Mji wa Serikali ni Dola za Marekani bilioni 4,788,749,111, sawa na shilingi trilioni 10.7. Gharama hizi zinategemewa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya fedha kama vile serikalini, wafadhili, mashirika ya umma, taasisi binafsi na za serikali, na mashirika binafsi.

Tarehe 11 Juni, 2020, Rais Magufuli alizindua majengo ya ofisi za makao makuu ya Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mjini Dodoma, kisha aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara za mji wa serikali Mtumba na kukabidhi pikipiki 448 za maofisa tarafa hapa nchini.

Kwenye shughuli hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi, Rais Magufuli alisema mji wa serikali Mtumba unaendelea kuboreshwa kutokana na kuanzishwa kwa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami ambazo zitakuwa na urefu wa kilomita 51.2.

Kwa mujibu wa Tarura Makao Makuu ambayo ndio yenye jukumu la ujenzi wa barabara hizo, ujenzi umegawanyika katika makundi mawili; kundi la kwanza litajumuisha barabara zenye njia mbili na kundi la pili litajumuisha barabara zenye njia nne.

Barabara zenye njia mbili zitakuwa na jumla ya urefu wa kilomita 38.8 wakati barabara za njia nne zitakuwa na urefu wa kilomita 12.4 na gharama za kukamilisha ujenzi wa barabara hizo ni shilingi bilioni 89.1.

Lengo kuu la ujenzi wa barabara hizi katika mji wa serikali ni kuunganisha taasisi zote za serikali pamoja na wizara zote zilizopo katika mji wa serikali Mtumba. Kwa maana nyingine, katika mji huo wa serikali hakutakuwa na barabara za vumbi kwani zote zitajengwa kwa kiwango cha lami.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Barabara za Mijini wa Tarura, Mohamed Mkwata, sambamba na barabara hizo kutakuwa pia kuna usafiri wa treni za kisasa za mjini (metro train).

Mkurugenzi huyo anasema usafiri huo utawarahisishia wafanyakazi waliopo katika mji wa serikali pamoja na wananchi kuweza kusafiri kwa urahisi zaidi kutoka katikati ya jiji na kufika katika mji wa serikali ili kupata huduma kwa urahisi.

Anasema usanifu wa barabara za mji wa serikali tayari umeshafanywa na Tarura makao makuu na kwamba umegharimu shilingi milioni 113 kwa kutumia wataalamu wa ndani wa wakala huo.

Kutokana na uamuzi wa kutumia wataalamu wa ndani, Mkwata anasema wameweza kuokoa takribani shilingi milioni 400 kama wangetumia wataalamu wa nje kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba utekelezwaji wa mradi huo umefikia asilimia 50.

 

Mkurugenzi huyo wa barabara za mijini anasema kutokana na usanifu wa barabara hizo, ujenzi utakapokamilika mji utakuwa na mandhari nzuri na ya kuvutia na kwamba wanatarajia utakuwa mji wa kisasa sana, kama siyo kwa bara la Afrika zima basi kwa dunia.

Mhandisi Mkwata anasema ujenzi wa barabara za lami unakwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mingine itakayojengwa chini au sambamba na barabara hizo, kama vile miundombinu ya kupitishia maji, umeme, gesi, mawasiliano pamoja na miundombinu ya mifumo ya kamera zitakazofungwa kila kona kuuzunguka mji huo wa serikali.

Tunataka barabara hizo zikishakamilika kusiwe na usumbufu wowote wa kuja kukata tena barabara ili kuweza kupitisha kitu kingine chini. Lakini pia barabara hizi zitazungukwa na miti aina mbalimbali ya matunda ambayo itakuwa imepandwa pembezoni mwa barabara na sehemu mbalimbali ya mji wa serikali.

Sambamba na barabara hizo, Mkwata anasema kutakuwa na ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge), ambayo itakuwa na urefu wa kilomita 101 kulizunguka jiji la Dodoma.

Reli hiyo anasema itaanzia Ihumwa, itapita Chamwino na kuelekea Vikonje ambapo hapo itajengwa stesheni kubwa, kisha reli itakwenda mji wa serikali, soko la Ndugai, Stendi mpya ya mabasi ya mikoani mpaka katikati ya mji kisha itaelekea Nara ambaki ni lililo nje ya mji.

“Katika mji wa serikali kutakuwa na kituo cha treni ambapo wafanyakazi na wananchi watakaotaka huduma katika mji huo wataitumia,” anasema.

Anasema kujengwa kwa miundombinu hiyo itarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji katika mji wa serikali na Jiji la Dodoma.

Serikali ya awamu ya tano, iliamua kutekeleza azma ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya serikali kuhamia Dodoma aliyoianzisha tangu mwaka 1973.

Kutokana na Dodoma kuwa katikati mwa Tanzania, moja ya malengo makubwa ya kuhamia Dodoma ilikuwa ni kusogeza huduma kwa wananchi ambao walikuwa wakilazimika kuzifuata Dar es Salaam ambako ni mbali kutoka katika baadhi ya maeneo ya nchi kama Mara, Kagera, Kigoma na Ruwaka.

MKUU wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi