loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kwaheri Maradona tutakukumbuka

JUMATANO ya wiki hii anga la soka liligubikwa na simanzi baada ya kutolewa taarifa za kifo cha gwiji la soka Maradona. Jina hili siyo geni masikioni mwa wapenda soka kote ulimwenguni, hii ni kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya katika kipindi chake chote alichokuwa akicheza soka.

Cheti chake cha kuzaliwa kinaonesha kuwa jina lake kamili ni Diego Armando Maradona, ambaye alizaliwa Oktoba 30, 1960 katika mji wa Lanús, Buenos Aires, Argentine.

Maradona alianza kucheza soka la ushindani mwaka 1976 katika klabu ya Argentinos Juniors na kustaafu mwaka 1997 kwenye Klabu ya Boca Juniors.

Kwenye maisha yake ya soka amepitia kwenye klabu kadhaa za Ulaya zikiwemo Barcelona na Napoli na mpaka anastaafu kwenye ngazi ya klabu alikuwa amecheza jumla ya mechi 491 na kufunga mabao 259.

Pia aliitumikia timu yake ya taifa ya Argentina kati ya mwaka 1977 na 1994 na akaifungia jumla ya mabao 34 kwenye mechi 91.

Licha ya makubwa yote hayo aliyoyafanya, lakini ulikuwa ukimuangalia huwezi kuamini kutokana na umbo lake, hakuwa na umbo kubwa la kutisha kwani vipimo vya urefu vinaonesha alikuwa na meta 1.65, ambazo ni sawa na futi 5.5 kwa wale wanaonifahamu yaani tunalingana urefu.

Maradona hakuwa mchezaji tu bali pia ni zaidi ya mchezaji, kwani alikuwa akiwaongoza vema wenzake wanapokuwa uwanjani. Alipachikwa jina la utani la “El Pibe de Oro” likiwa na maana ya mtoto wa dhahabu hili lilitokana na maajabu aliyokuwa akiyafanya uwanjani kipindi akiwa na umri mdogo.

Maradona ambaye ndiye aliyeipa heshima namba 10 kutokana na umahiri wake uwanjani na muda wote alikuwa akivaa jezi namba 10 ndiye mchezaji wa kwanza duniani kuweka rekodi ya kusajiliwa kwa dau kubwa mara mbili.

Mara ya kwanza aliposajiliwa na Barcelona kwa dau kubwa kipindi hicho likiwa ni pauni milioni 5 kisha mara ya pili aliposajiliwa na Napoli kwa dau kubwa la pauni milioni 6.9 kwa kipindi hicho ni kubwa mno. Katika fainali za Kombe la Dunia la Mwaka 1994 dunia ikaanza kumisi maufundi yake, katika hali isiyotarajiwa Maradona alicheza mechi mbili tu na hakuruhusiwa kuendelea na mashindano.

Ilikuwa katika mchezo wa Argentina dhidi ya Nigeria, Juni 25,1994 baada ya kufanyiwa vipimo vya damu kama alitumia dawa za kuongeza nguvu, ambazo haziruhusiwi mchezoni. Fainali hizi zilifanyika Marekani, ambapo alifunga bao moja tu dhidi ya Ugiriki.

Licha ya kucheza mechi hizo chache, lakini aliondoka na umaarufu katika ushangiliaji wa bao lake hilo pekee kwenye mashindano hayo. Hakika Maradona amefanya makubwa mno kwenye soka ambayo kamwe hayatakuja kusahaulika na katika kulithibitisha hilo ni kutokana na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa karne, FIFA Player of the 20th Century award.

foto
Mwandishi: Mohammed Mdose

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi