loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

DC aingilia kati wananchi kuchomewa nyumba

SAKATA la askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kudaiwa kuteketeza nyumba 150 wanazodai zimejengwa hifadhini limemfanya Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda kuwataka madiwani kuwasilisha hoja katika baraza lao kuomba kipande cha ardhi kimegwe kutoka Hifadhi ya Misitu ya Akiba Lwafi na wakabidhiwe wananchi walime.

Amemuomba Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, Aida Khenan (Chadema) kusimamia hoja hiyo ikiwasilishwa katika baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi na kuiwasilisha serikalini ili wananchi wapate ardhi kwa ajili ya kilimo.

Mtanda alitoa maagizo hayo baada ya kusomewa taarifa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Itete, Robert Matwiga kwamba askari wa Tawa waliteketeza kwa moto nyumba 150 kwamba ziko hifadhini katika tukio lilitokea Alhamisi wiki iliyopita.

Mtanda alifika katika kijiji cha Itete kilichopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama wilaya. “Hili linawezekana ndio maana Rais John Magufuli hivi karibuni alimega sehemu ya ardhi ya hifadhi na kuwagawia wananchi, cha msingi ni kujenga hoja juu ya hili.

“Hoja hii ikipita katika baraza la madiwani miye kama DC nitaandika barua maalumu kusisitiza muhimu wa wananchi kutengewa kipande cha ardhi hifadhini ili wapate eneo la kulima,”alisisitiza.

Aidha aliwataka Tawa kuweka mipaka ya kudumu kwa kuchimbia mawe makubwa ardhi yakiwa na maandishi badala ya kusimika vibao ambavyo ni rahisi kuhamishika.

Alikiri kuwa eneo la ardhi wanaloishi wakazi wa Kijiji cha Itete ni dogo huku idadi yao ikiwa imeongezeka na ukubwa wa ardhi hauongezeki. Pia alimwagiza Ofisa Ardhi Wilaya ya Nkasi kulipima upya eneo hilo la mpaka kwa GPS akimpatia siku saba awe amekamilisha ripoti yake ili ukweli ubainike.

Mbunge Khenan ametoa msaada wa maturubai 100 ambayo yamefungwa katika eneo mbali na mpaka wa Hifadhi ya Lwafi ili waathirika wajisitiri kwa muda. Mwenyekiti wa Kijiji cha Itete, Matwiga na Diwani wa Kata ya Itete, John Garincha na baadhi ya waathirika wamesisitiza zilizoteketezwa na moto na askari wa Tawa ni zaidi ya nyumba 150.

“Kwani nikiiezeka nyumba yangu kwa nyasi inapoteza sifa ya kuitwa nyumba, walichotusaidia ni kwamba kabla ya kuziteketeza walituruhusu tuchukue kila kilichokuwa chetu kutoka ndani ya nyumba hizo zikiwemo nguo na vyakula “ alieleza mmoja wa waathirika.

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa leo amekagua kitalu cha ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame, Nkasi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi