loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Amani yavutia wawekezaji nchini

AMANI, utulivu na mazingira rafiki ya uwekezaji, vimetajwa kama sababu ya kuendelea kupokea wawekezaji wengi wapya kutoka nchi mbalimbali duniani kuja kuwekeza nchini zikiwamo kampuni 13 za Austria zilizofi ka nchini jana kwa nia hiyo.

Kupitia kampuni hizo zitakazoshirikiana na wazawa, miradi isiyopungua mitano mikubwa inatarajiwa kupatikana kutokana na uwekezaji wao. Tangu mwaka 1990, wawekezaji kupitia kampuni za Austria wamewekeza nchini kwa miradi zaidi ya 11 ya gharama ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 27.86(zaidi ya Sh bilioni 65) ambayo pamoja na faida nyingine za kiuchumi, imetoa ajira zaidi ya 786 kwa Watanzania.

Jana, kampuni hizo 13 zimefika katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) jijini Dar es Salaam, kufahamu na kuona namna wanaweza kushirikina na sekta binafsi nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwamo kilimo (maua), elimu mtandao, utengenezaji wa vifaa tiba, vifaa vya usalama barabarani na vya anga.

Balozi wa Austria nchini ambaye Ofisi yake ipo Nairobi nchini Kenya, Christian Fellner, akiwa kiongozi wa ugeni huo, alisema hali ya usalama na amani ya Tanzania pamoja na mazingira bora ya uwekezaji yamewavutia wawekazaji hao kutaka kufika kujionea na kuwekeza nchini.

“Kampuni za Austria zinataka kuwekeza Tanzania zaidi kutokana na usalama lakini pia tuzalishe vifaa vyenye ubora wa hali ya juu ambao siku zote Austria inao katika bidhaa zake hapa Tanzania. Maeneo ya uwekezaji ni elimu, elimu mtandao, kilimo, vifaa tiba, sekta ya usalama (anga na barabara),” alisema Balozi Fellner.

Balozi Fellner alitaja bidhaa za Tanzania ambazo zinanunuliwa sana nchini mwao na kueleza ni moja ya maeneo wanayolenga kuwekeza zaidi kuwa ni maua na korosho. “Kwetu maua kutoka Tanzania yana soko kubwa sana na korosho za hapa zina soko kubwa kwetu,”alisema. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dk Maduhu Kazi, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea ugeni wa viongozi wa kampuni nane kati ya 13 huku wengine wakiwa njiani, alisema amani, utulivu na ukuaji wa uchumi mzuri ni sababu zinazowaleta wawekezaji nchini wakimemo hao wa Austria. Dk Kazi alisema lengo la ugeni huo ni kuangalia vivutio vya uwekezaji vilivyopo nchini. “Ndugu zetu wa Austria wamesafiri kutoka nchini mwao kuja hapa kwetu kuangalia vivutio vya uwekezaji na tumeshirikiana katika hili na taasisi nyingine nchini na Ubalozi wetu kutoka Kenya na kwa namna walivyovutiwa, tunatarajia kupata miradi isiyopungua mitano,” alisema Dk Kazi. Alisema hivi sasa wanaendelea na mazungumzo ili kutumia fursa zilizopo kuongeza miradi nchini kutoka Austria. Alisema kwa sasa si tu Austria bali nchi nyingine nyingi zinakuja kuwekeza nchini kutokana na utulivu na amani iliyopo. “Kuna nchi kadhaa zipo mbioni zinakuja, zimevutiwa na hali ya utulivu iliyopo nchini mwetu lakini vilevile hali ya ukuaji mkubwa wa uchumi kama mnavyofahamu tumeingia katika ukuaji wa uchumi wa kipato cha kati kwa hivyo inamaana kuna fursa zaidi za uwekezaji. Alisema Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji na kikubwa zaidi taasisi hiyo inaitikia mwito wa Rais John Magufuli kupitia maagizo yake na hotuba yake alipofungua Bunge la 12 mjini Dodoma, Novemba 13 mwaka huu kwamba serikali yake itajielekeza kukuza uchumi zaidi kupitia sekta binafsi na uwekezaji.

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa leo amekagua kitalu cha ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi