loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mradi ulivyodhibiti uvuvi  haramu, kuongeza mapato

Mradi ulivyodhibiti uvuvi haramu, kuongeza mapato

KATIKA hotuba yake ya kuzindua Bunge la 12 jijini Dodoma, Novemba 13, mwaka huu, Rais John Magufuli alizungumzia azma ya serikali yake katika miaka mitano ijayo kuipa msukumo sekta ya uvuvi.

Aliwaambia wabunge na Watanzania kwa ujumla kuwa mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa bado ni mdogo.

“Nchi yetu pia imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yanayofaa kwa shughuli za uvuvi, ikiwemo Ukanda wa Pwani, maziwa, mito na mabwawa. Hali hii inafanya sekta hii kuwa na nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza Pato la Taifa na pia kupambana na umasikini na tatizo la ajira. Hata hivyo, kwa sasa, mchango wake bado ni mdogo,” alisema Rais Magufuli katika hotuba yake hiyo kwa Bunge.

Aliongeza: “Hivyo basi, kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia kuikuza sekta hii, ikiwemo kuimarisha shughuli za uvuvi kwenye bahari kuu, ambako tumekuwa tukipoteza mapato mengi.”

Rais Magufuli alibainsha kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati ya Bunge kuhusu Shughuli za Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 2018; shughuli za uvuvi kwenye eneo hilo zinaweza kuingizia serikali mapato ya moja kwa moja ya takriban Sh bilioni 352.1 kwa mwaka endapo mifumo ya usimamizi na udhibiti ingekuwa imara na samaki wakawa wanachakatwa nchini.

“Hata hivyo, mapato yaliyokuwa yamekusanywa kwa kipindi cha miaka tisa (2009 hadi 2017) yalikuwa shilingi bilioni 29.79, sawa na shilingi bilioni 3.3 kwa mwaka.  Kiwango hiki cha mapato hakikubaliki.

Hii ndiyo sababu, tunataka, kwenye miaka mitano ijayo, kusimamia vizuri shughuli za uvuvi wa bahari kuu ili Taifa letu linufaike na rasilimali zake, kwa kuhusisha sekta binafsi. Kwa bahati nzuri, tayari, mwaka huu (2020) tumetunga Sheria Mpya ya Kusimamia na Kuendeleza ya Uvuvi wa Bahari Kuu,” alieleza Rais Magufuli.

Kuonesha msisitizo, alisema kuwa serikali imepanga kununua meli nane za uvuvi kwa kushirikiana na Shirika IFAD (nne upande wa Zanzibar na nne upande wa Tanzania Bara) ili zishiriki katika uvuvi wa bahari kuu, kwa kuwa suala la uvuvi wa eneo holo ni la Muungano.

“Tunakusudia pia kujenga bandari kubwa ya uvuvi itakayotoa ajira zipatazo 30,000; na tutaendelea kuihamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuchakata samaki,” alieleza Rais Magufuli.

“Sambamba na kusimamia Bahari Kuu, tutakuza shughuli za uvuvi kwenye maziwa yetu makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa) pamoja na mito yetu mikubwa. Tutahamasisha wavuvi wetu wadogo kujiunga kwenye vikundi ili tuweze kuwapatia mitaji, ujuzi, vifaa na zana za uvuvi; na halikadhalika tutapitia upya tozo na maeneo mbalimbali ili kuwapunguzia wavuvi kero na kuvutia uwekezaji,” alisema.

“Tutahamasisha pia watu binafsi kujenga mabwawa na kufuga kisasa kwa kutumia vizimba. Sekta ya uvuvi ni lazima itoe mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu. Wateule wote wa sekta hii ni lazima walisimamie hili.”

Msisitizo huu wa Rais Magufuli unaungwa mkono na ukweli kuwa katika miaka mitano iliyopita, serikali ilianzisha mradi mkubwa wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish).

Lengo la mradi ni kuimarisha usimamizi madhubuti wa uvuvi katika ngazi ya kijamii, kitaifa na kimataifa; kujenga uwezo wa nchi kusimamia rasilimali za uvuvi; kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika ulinzi wa rasilimali za uvuvi wa Bahari Kuu; kuinua uchumi wa jamii ya watu wa pwani na kuinua Pato ya Taifa kutokana na rasilimali za uvuvi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya uvuvi, Dk Rashid Tamatamah, Mradi wa SWIOFish unatekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Tanzania Bara na iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar, pamoja na Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu.

Dk Tamatamah anasema wanufaika ni wavuvi wa pwani ya Bahari ya Hindi, wakulima wa mwani, wafugaji wa viumbe maji na wachakataji wa mazao ya uvuvi wakiwamo wanawake na jamii inayozunguka maeneo hayo.

Anabainisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha miaka sita na unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 36. Ulianza Juni 22, 2015 na utafikia tamati Septemba 21, 2021.

Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo, mradi huo umepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka mitano sasa ikiwamo kudhibiti uvuvi haramu wa kutumia baruti/mabomu kwa asilimia 100.

Akifafanua, anasema uvuvi haramu wa kutumia baruti/mabomu umedhibitiwa kwa asilimia 100 kutokana na kuimarishwa kwa doria pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa jamii ya pwani kuhusu madhara ya uvuvi haramu.

“Aidha, usajili wa vyombo vya uvuvi umeongezeka maradufu hadi kufikia asilimia 58 kutoka asilimia 25 ya awali kabla ya mradi. Hii imechangiwa na usimamizi wa utekelezwaji wa sheria na kanuni za uvuvi,” anasema Dk Tamatamah.

Mradi huo unaotekelezwa katika maeneo ya pwani ya Tanzania katika wilaya tano za mfano zikiwamo Mkinga, Tanga Jiji, Pangani, Bagamoyo na Lindi, kabla ya kuongezwa Halmashauri ya Chalinze.

Anayataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa samaki wanaovuliwa kutokana na kurekebishwa kwa baadhi ya kanuni za uvuvi ikiwamo Kanuni ya Uvuvi ya Mwaka 2009 kuhusu kubadilisha ukubwa wa macho ya nyavu za kuvulia kuwa milimita nane badala ya milimita 10, hatua ambayo imeongeza tija kwa wavuvi wa dagaa maeneo ya pwani.

“Vile vile, baadhi ya samaki waliotoweka wameanza kuonekana, kwa mfano samaki aina ya sangoro na wengineo. Haya ni baadhi ya matokeo ya kuimarika kwa usimamizi wa rasilimali za uvuvi nchini,” anasema Katibu Mkuu Uvuvi.

Pia mradi umefadhili mafunzo ya uvuvi endelevu ambayo yamesaidia kuongezeka kwa uelewa kwa jamii ya pwani, pamoja na uanzishwaji wa vikundi 50 vya usimamizi wa rasilimali za uvuvi (BMU) katika wilaya za mfano.

Pia umewezesha utunzaji wa mazingira ya pwani ambako ukataji wa misitu ya mikoko umepungua badala yake mikoko imekuwa ikipandwa katika vijiji mbalimbali kwa lengo la kutunza mazingira.

“Usafi wa fukwe katika maeneo ya mradi umeboreshwa na uchimbaji wa mchanga katika fukwe hususan Bagamayo umepungua kwa kiasi kikubwa,” alieleza.

Kuhusu mapato, anatoa mfano wa mapato ya Halmshauri ya Wilaya ya Pangani ambayo yameongezeka kutoka Sh milioni 56 mwaka 2016/17 hadi kufikia Sh milioni 235 mwaka 2018/19.

Mbali ya hayo, anasema mradi umewezesha kuandaliwa kwa viwango vya dagaa na mwani vilivyopitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Uandaaji wa viwango hivyo ni mchakato wa kukidhi masoko ili bidhaa hizo ziweze kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Aidha anasema kumekuwa na maboresho kwa miundombinu ya taasisi shiriki ikiwamo Maabara ya Utafiti iliyoko Kunduchi jijini Dar es Salaam, kujenga ofisi tano za vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari na pwani (BMU) na kuboreshwa kwa mfumo wa ukusanyaji wa takwimu za uvuvi ambazo sasa zinakusanywa kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Mratibu wa Mradi wa SWIOFish Tanzania Bara, Nichrous Mlalila anasema licha ya mafanikio hayo, changamoto mbali mbali zimekuwa zikijitokeza zikiwemo za ugumu wa upatikanaji wa fedha za kuendesha shughuli za kila siku za BMU, kutokea kwa baadhi ya matukio ya uvuvi haramu wa kutumia nyavu zisizofaa kisheria na upatikanaji wa takwimu sahihi katika mifumo ya ukusanyaji taarifa.

Mlalila amesema hadi sasa asilimia 65 ya shughuli za mradi zimetekelezwa na kukamilika, ambako asilimia nane zipo katika utekelezaji kwa zaidi ya asilimia 75, asilimia 19 ya shughuli za mradi zinaendelea kutekelezwa kati ya asilimia 25 hadi 75 ya utekelezaji. Asilimia nne 4) zipo katika utekelezaji wa asilimia chini ya 25.

Anaongeza kuwa mradi unaonesha matokeo chanya na upo katika mwelekeo mzuri wa utekelezaji.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/296753011cd7be2dff2e519fc28cfad9.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi