loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

NIMR yahimizwa kufanya utafiti

TAASISI ya Taifa ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) imeelekezwa kujikita kufanya utafiti zaidi ili kupata majawabu ya matatizo ya Watanzania, yakiwamo magonjwa ili kuwa na jamii yenye afya.

Mwito huo ulitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dk Seleman Serera, wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge katika sherehe za miaka 40 za taasisi hiyo ambazo kikanda zilifanyika katika Viwanja vya Nyerere Square jijini  hapa.

"Tafiti hizi mnazozifanya zitakuwa na tija kwa Watanzania iwapo mtalenga njia bora za kutokomeza magonjwa ambayo yanasumbua jamii yetu hivi leo," alisema Dk Serera.

 Alisema tafiti za magonjwa ni muhimu katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Dodoma unaoshuhudiwa kupokea ongezeko kubwa la watu tangu serikali ilipotangaza kuhamishia rasmi shughuli zake.

Aidha, aliipongeza taasisi hiyo kwa kuyaishi maono ya Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kupambana na adui maradhi ili wananchi waweze kuchapa kazi.

"Rais Dk John Magufuli anasisitiza watu kufanya kazi, lakini hatuwezi kufanya kazi kama tunaendelea kusumbuliwa na maradhi na hatuwezi kuwa na afya njema kama utafiti wa kina haufanyiki kujua matatizo tuliyo nayo," alisema.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Profesa Yunus Mgaya, Dk Mary Mayige alisema taasisi hiyo ilianza tafiti za magonjwa ya binadamu tangu mwaka 1920 na baada ya Uhuru vituo  vya utafiti vilikuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

NIMR ilianzishwa kisheria mwaka 1979 baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika na kuanza kazi zake rasmi mwaka 1980.

Kwa mujibu wa Dk Mayige, hadi sasa taasisi hiyo ina vituo vinane na itaendelea kufungua vituo zaidi ili kusaidia wananchi kwa karibu zaidi.

"NIMR ina majukumu mengi ikiwemo kuhamasisha utafiti na kufanya ugunduzi wa utafiti mbalimbali ili kuhakikisha taifa linakuwa na  jamii ya watu wenye afya njema," alisema Dk Mayige.

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi