loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa aonya mafataki, vifo vya Ukimwi vyapungua

Majaliwa aonya mafataki, vifo vya Ukimwi vyapungua

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameonya watu wenye umri mkubwa kuwarubuni wasichana wenye umri mdogo katika kushiriki mapenzi katika umri mdogo.

Aidha, amesema uimarishaji wa huduma za tiba ikiwemo matumizi ya dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARVs) umechangia kupunguza vifo vitokanavyo na Ukimwi kutoka vifo vya watu 85,000 mwaka 2001 hadi kufikia vifo 21,529 mwaka jana.

Aidha, serikali imebaini kuwa asilimia 40 ya maambukizi hutokea kwa vijana huku asilimia 80 ndani ya kundi hilo ni wasichana ambao huwa na wapenzi wengi na kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Ukimwi.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mandela katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Nataka nitoe tahadhari ya watu wazima wanaojihusisha na mapenzi na wasichana wadogo, ole wenu, ole wenu, ole wenu, vijana wa kike msijihusishe na mapenzi katika umri mdogo, lazima muwe na subira, nimefurahi katika mabanda kule wapo wanaofanya shughuli za kiuchumi,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu aliwataka vijana kutovutika na zawadi ndogondogo kama fedha, chipsi na vitu vingine vyenye ushawishi, huku pia vijana hao kuwa na matumizi mazuri ya kondomu, ulevi wa kupindukia na matumizi ya dawa za kulevya ambavyo huchochea maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni 'Mshikamano wa Kimataifa, Tuwajibike Pamoja.' 

Waziri Mkuu alisema maambukizi mapya ya Ukimwi nayo yamezidi kupungua kutoka watu 130,000 mwaka 2001 hadi kufikia watu 68,484 mwaka 2019, hivyo alitoa wito kwa wadau wote katika mapambano ya ugonjwa huo waongeze jitihada.

“Mafanikio yote haya yametokana na kuendelea kuimarika kwa huduma za tiba ikiwemo matumizi ya dawa za kufubaza VVU (ARVs) na afua za kinga zinazohusisha tohara ya kitabibu kwa wanaume na kuzuia maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” alisema.

Alisema Tanzania imefanikiwa kufikia malengo ya tisini tatu (90:90:90) hasa katika 90 ya pili na ya tatu.

“Kwa kujikumbusha tu, ni kwamba tisini tatu zinalenga kuhakikisha kuwa asilimia 90 ya WAVIU wanajua hali zao; asilimia 90 ya wanaojua hali zao wanaanza kutumia dawa za kufubaza mapema na asilimia 90 ya walioanza dawa za kufubaza VVU kinga zao za mwili zinaimarika ifikapo mwaka 2023,” alieleza.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau mbalimbali wa masuala ya mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, waongeze jitihada hususani katika kuhamasisha upimaji wa VVU ili wafikie lengo la 90 ya kwanza.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametoa siku 30 kwa kila mkoa uliowahi kufanya maadhimisho hayo uhakikishe kuwa unawasilisha taarifa yake Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania ndani ya mwezi mmoja kuanzia jana.

Vilevile, alitoa agizo kwa TACAIDS, Wizara ya Afya na wadau wote wa kudhibiti VVU na Ukimwi nchini, wajipange vizuri kubaini na kufanyia kazi maeneo mbali mbali ya uwekezaji yenye gharama nafuu katika kudhibiti Ukimwi, lakini yatakayoleta matokeo makubwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Anna Mghwira alisema kiwango cha maambukizi ya Ukimwi katika mkoa huo kimeendelea kupungua kutoka asilimia 7.3 mwaka 2004 hadi kufikia asilimia 2.6 mwaka 2017. “Kiwango hiki kipo chini ya wastani wa maambukizi kitaifa ambacho ni asilimia 4.8,” alisema Dk Mghwira.

Aliongeza, “Hata hivyo kiwango cha maambukizi kimkoa kuwa chini ya wastani wa kitaifa haimaanishi kuwa tuko salama; hivyo sote tunapaswa kuongeza juhudi za pamoja ili tufikie lengo la maambukizi sifuri ifikapo 2030.”

Balozi wa Marekani nchini, Dk Donald Wright aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kupambana na Ukimwi ikiwamo kuhakikisha kuwa watu wote wanaoishi na virusi hivyo wanapata dawa na kuahidi kuwa serikali yake itaendelea kushirikiana na Tanzania.

Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Leticia Mourice aliiomba serikali, asasi za kiraia, taasisi za dini na vyombo vya habari viendelea kutoa elimu ya makuzi, kubadili tabia na hofu ya Mwenyezi Mungu kwa vijana, wazazi na walezi ili kuwaepusha na matendo hatarishi.

Wakati huohuo, Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imesema maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa Jiji la Dar es Salaam yamefikia asilimia 4.7 na mkazo wa kuelimishwa ukilengwa zaidi kwa vijana kuanzia miaka 15 hadi 24.

Mratibu wa TACAIDS kwa Jiji la Dar es Salaam, Grace Kessy alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na gazeti hili kwa simu ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani.

Kessy alisema katika kuadhimisha siku hiyo, tume imefanya shughuli mbali mbali ikiwemo kukutana na vijana na kuzungumza nao kuhusu namna ya kujizuia kutopata maambukizi ya virusi hivyo.

Alisema vijana wanabeba sehemu kubwa ya kuwekewa mkazo hasa walio na umri wa miaka kuanzia 15 hadi 24 na kuelimishwa kuhusu matumizi sahihi na endelevu ya kondomu na matumizi sahihi ya dawa, unyanyapaa na ubaguzi.

Alisema katika mwaka 2003/4 maambukizi kwa Jiji la Dar es Salaam yalikuwa asilimia 10.9, mwaka 2007/8 yalifikia asilimia 9.3, mwaka 2011/12 yalifikia asilimia 6.6 na mwaka 2016/17 maambukizi yalikuwa asilimia 4.7.

Alisema changamoto bado zipo kitaifa na kimkoa, lakini elimu inahitajika zaidi haswa ikizingatiwa kuwa kitaifa maambukizi yamefikia 72,000 kwa mwaka ambapo watu 200 wamekuwa wakiambukizwa kila siku.

Alisema katika kiwango hicho vijana wanabeba asilimia 40 ambayo ni sawa na watu 28,800, na watoto wa kike wakichukua asilimia 80 sawa na watu 23,040 na watoto chini ya miaka 15 wakiwa 8,600.

Kitaifa kwa mwaka kiwango cha maambukizi ni 72,000 na asilimia 40 ni vijana 28,800 na asilimia 80 ni watoto wa kike. Kwa asilimia kiwango cha kitaifa ni asilimia 4.8.

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi