loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa atoa maagizo saba kwa waajiri

Majaliwa atoa maagizo saba kwa waajiri

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo saba kwa waajiri nchini katika kuboresha ajira, huku akieleza kuwa serikali itaanza kufanya mapitio ya mitaala ya elimu nchini ili mwanafunzi atakapomaliza masomo ya juu aweze kwenda moja kwa moja katika kazi yake ya taaluma.

Amesema suala la ajira nchini ni mgogoro, lazima litafutiwe njia ili vijana wanaomaliza masomo kila mwaka wajiajiri na sio kutegemea kuajiriwa peke yake.

Waziri Mkuu alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 60 ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) huku akiwataka waajiri kutazama upya eneo la mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao, kwa kuwa wengi wana ajira za muda, jambo linalowanyima haki.

Akitaja maelekezo hayo kwa waajiri, alisema katika eneo la soko la ajira, vijana wengi wamekuwa wakihitimu kila mwaka kutoka vyuo vikuu vya elimu huku wahitimu wakisubiri kuajiriwa ambapo walitakiwa kujiajiri.

“Badala ya kumaliza chuo na kufikiria kuajiriwa, ifikie mahali mitaala ya elimu iseme ukimaliza ni kuanza kufanya kazi za taaluma yake na mhitimu aende huko,” alisema Majaliwa huku akisisitiza vijana kusoma kozi ambazo mbele zinatumika vyema na sio kufuata mkumbo na anapomaliza kujikuta akitembea na bahasha za vyeti kutafuta kazi.

Alisema maelekezo mengine ni katika maslahi ya wafanyakazi, ambapo waajiri wametakiwa kutazama suala hilo kwa umakini, kwa kuwa wapo waajiri wanaodaiwa na wafanyakazi wao kutopeleka michango mbalimbali, jambo ambalo hutoa shida kwa serikali wakati wa kuhitaji mafao yao.

Aliwaagiza waajiri kuhakikisha michango ya wafanyakazi wao, inawasilishwa kwa wakati na kwa usahihi. Katika eneo la vyama vya wafanyakazi, aliwataka waajiri kutokuwa wagumu kwa wafanyakazi wao kuanzisha na kujiunga katika vyama vyenye kutetea haki zao.

“Zipo taarifa kuwa wapo waajiri wanaodiriki hata kuongeza mkataba kwa wafanyakazi wanaokuwa katika vyama hivyo kwa sababu za kudai posho,” alisema. Alihimiza kuwa wafanyakazi waruhusiwe kuanzisha na kujiunga na vyama, jambo litakalopunguza ama kuondoa migogoro mahali pa kazi.

Alisema maelekezo mengine ni katika eneo la afya na usalama mahali pa kazi, waajiri wazingatie na kusajili maeneo yao ya kazi ili vyombo kama Wakala wa Usalama  Mahali pa Kazi (OSHA) waweze kukagua.

Kadhalika, aliwataka waajiri kuzingatia mafunzo mahali pa kazi na waajiri waainishe mahitaji ya ujuzi kwenye soko ili serikali iweke mkazo katika suala hilo ili kufanya kazi kwa umahiri zaidi.

Alisisitiza katika ulipaji kodi kwa waajiri kwa wakati huku akiwapongeza kwa hatua hiyo kwa kuwa inachangia katika kukuza uchumi wa nchi.

Vilevile aliwataka waajiri watoe kipaumbele kwa mafunzo ya urasimishaji ujuzi katika maeneo yao ya kazi, kwa kuwa lipo ongezeko la wahitimu wengi kutoka katika vyuo mbalimbali nchini wakihitaji mafunzo ya ujuzi wa kazi ili waajiriwe.

Kuhusu kuimarisha uchumi nchini, aliwataka waajiri kuishauri serikali katika yale wanayoona yanafaa kwa kuwa serikali inahitaji mchango wao ili uchumi uzidi kukua na pia iko tayari kufanya mazungumzo ili kutatua migogoro ya kibiashara kwa wafanyabiashara.

Aidha, aliwaalika wawekezaji katika sekta mbalimbali nchini na kwamba zipo fursa nyingi katika mafuta na gesi, na Tanzania ni mahali sahihi pa kuwekeza.

Hata hivyo, aliwataka wafanyakazi wanapopata ajira kuhakikisha inakuwa na matokeo chanya kwa eneo lake la kazi na kuacha tabia za kuwa na shughuli nyingi za binafsi nje ya ajira hizo.

“Tutumie pia Jumuiya za Kitaifa na Kimataifa kama SADC na EAC kuwa sehemu ya masoko yetu ili kujenga uchumi wenye manufaa kwa wote,” alisema Waziri Mkuu na kukumbusha kuwa Watanzania pia wanaajirika katika maeneo mbalimbali na kipaumbele kiwe kwao.

Mwenyekiti wa Bodi ya ATE, Jayne Nyimbo alisema ATE ilianza mwaka 1960 ikiwa na wanachama 1,400, lengo  kubwa ni kutetea maslahi ya waajiri nchini.

Nyimbo alisema waajiri wamekuwa wakiendeleza ujuzi na kutoa fursa kwa vijana wahitimu na kuwapa nafasi, jambo ambalo katika maadhimisho hayo ni la kutiliwa mkazo na kila mwajiri ili kupata wataalam katika fani mbalimbali.

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi