loader
Dstv Habarileo  Mobile
Baraza la Mawaziri lililobeba matumaini

Baraza la Mawaziri lililobeba matumaini

*Ni kauli ya wasomi, wateule watoa neno

BAADA ya Rais John Magufuli kutangaza baraza lake la mawaziri, wasomi wamesema ni baraza lililobeba matumaini kwa Watanzania.

Wakati huo huo baadhi ya mawaziri wateule, wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwaamini katika nafasi alizowateua.

Wameahidi kufanya kazi kwa bidii ili kutekeleza kwa mafanikio Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Miongoni mwa wasomi hao waliozungumza jana na HabariLEO ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk Richard Mbunda aliyesema kuwa kitendo cha Rais Magufuli kuchukua muda mrefu kutangaza baraza lake la mawaziri, kililenga kupata watu wenye ujuzi, weledi na wabunifu katika kuisaidia serikali na kutekeleza ahadi za CCM zilizotolewa wakati wa kampeni.

Dk Mbunda alisema kwa sasa Bunge lina watu wengi wenye utaalamu mbalimbali na uwezo mkubwa na isitoshe kwenye utawala wa nchi, serikali inapofanya vizuri anayesifiwa ni rais na inapofanya vibaya anayekosolewa ni rais pia, ndiyo maana Rais Magufuli alitumia muda mrefu kumfuatilia kila mmoja na kujiridhisha kabla ya kumteua.

“Walioachwa kwenye nafasi za uwaziri wasijisikie vibaya, inawezekana utendaji wao ulikuwa mzuri lakini kwa sasa inawezekana Bunge limepata watu wengi wazuri na wenye ujuzi na uwezo wa kuleta mabadiliko, lakini walioteuliwa wajue kwamba huu siyo wakati wa kusherehekea kwa kuwa Rais Magufuli haoni shida kuwatumbua watakaoshindwa kazi,”alisema Dk Mbunda.

Aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda, alisema uamuzi wa Rais Magufuli kuweka sura nyingi mpya na vijana wengi kwenye baraza lake ni hali inayoleta matumaini kwa Watanzania na taifa.

Mapunda alisema mchanganyiko huo wa mawaziri vijana, sura mpya na mawaziri wa zamani, unawafanya wananchi kuona kuwa uongozi wa nchi ni wao na hakuna mtu mwenye hati miliki, bali uongozi ni wa kuachiana.

“Rais ameteua baraza la mawaziri la watu wenye sura ya utendaji, inatoa matumaini mapya kwa kizazi kijacho na kwa kila mtu, ni baraza lililozingatia mtawanyiko wa mikoa, jinsia na rika, kwa hiyo ni baraza ambalo liko vizuri sana,”alisema Mapunda.

Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima, alisema kwa kuwa mawaziri ndiyo watendaji wakuu kwa huduma za umma, hivyo mchanganyiko ambao Rais Magufuli ameufanya wa kuwaweka vijana wengi, sura mpya na wengine wa zamani ni mzuri kwa kuwa unawaleta pamoja watu wenye uzoefu wa muda mrefu na vipaji, lakini pia inatoa fursa kwa vijana kujifunza uzoefu huo.

“Tuko kwenye karne ya 21 sasa, wengine wamefanya kazi zaidi kwenye karne ya 20, kwa hiyo kwenye karne ya 21 lazima kizazi kipya kianze kujifunza namna ya kuendesha serikali, kuendeleza nchi na kuangalia mahitaji mapya ya nchi, mahitaji makubwa kwa nchi yetu sasa hivi yanaangalia wingi wa vijana waliopo, kwa hiyo lazima wawepo mawaziri ambao watawatumikia hawa vijana vizuri,” alisema.

Kuhusu walioachwa kwenye baraza la mawaziri, Dk Kitima alisema ni mabadiliko ya kawaida kwa kuwa uwaziri ni huduma kwa umma, hivyo kubadilishana madaraka lazima kuwepo. Alisema kung’ang’ania madaraka, siyo tabia ya Watanzania kwa sababu Tanzania ina vipaji vingi na vya kutosha na mtu kutorudishwa kwenye ofisi, haina maana hafai.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU), Profesa Gaudence Mpangala, alisema kwa kuwa Rais Magufuli alichukua muda mrefu kutangaza baraza lake, anaamini aliowateua watamsaidia katika kujenga taifa.

Alisema Rais Magufuli ndiye rais wa kwanza hapa nchini, kufanya mabadiliko mengi ya mawaziri kwa kuwa anataka watu wanaoendana na kasi yake, lakini pia kitendo cha kuwateua vijana wengi ni harakati zake za kuleta mwendelezo wa uongozi kwa kuwa vijana watajifunza uongozi wa nchi.

Wakili Albert Msando alisema baraza jipya la mawaziri, linaonesha dhamira ya Rais Magufuli juu ya kile anachotaka kufanya kwa taifa katika miaka mingine mitano ya utawala wake.

Mawaziri Wateule

Waziri mteule wa Viwanda na Biashara, Geofrey Mwambe, alimshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini na kumpa jukumu la kumsaidia kusimamia sekta ya viwanda na biashara, ambayo ndiyo mwajiri mkuu katika kutengeneza mapato ya mwananchi mmoja mmoja na mapato ya serikali.

Alisema atatumia uzoefu alionao kwenye sekta za uchumi, biashara na uwekezaji katika kutimiza majukumu yake na kwa kushirikiana na mawaziri wenzake, wataweza kumsaidia rais katika kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati wa juu.

Ummy Mwalimu ambaye ni Waziri mteule wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), alisema ameupokea uteuzi huo kwa unyenyekevu na kuahidi kuchapa kazi kwa bidii.

Alisema watahakikisha wanatunza na kuenzi moja ya tunu za taifa hili yaani Muungano wa serikali mbili, pamoja na kuimarisha utunzaji na uhifadhi mazingira na kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri mteule wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema amepokea uteuzi huo kwa shukrani na heshima kubwa kutokana na rais kuendelea kuwa na imani naye.

Waziri mteule wa Ujenzi na Uchukuzi ambaye pia ni Mbunge mteule, Dk Leonard Chamuriho, alimshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini katika kumsaidia kwenye ujenzi wa taifa.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi