loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM: Acheni kutumia WhatsApp  kwa mawasiliano ya kiserikali

JPM: Acheni kutumia WhatsApp kwa mawasiliano ya kiserikali

RAIS John Magufuli amewataka mawaziri na watendaji wote serikalini, kuacha kutumia mitandao ya kijamii, kufanya mawasiliamo rasmi ya kiserikali, ikiwemo kutumiana barua au ujumbe.

Aliwakumbusha viongozi hao kuwa serikali inafanya kazi na kuwasiliana kwa njia ya maandishi kwenye karatasi na siyo mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp.

Aliyasema hayo jana Ikulu Chamwino jijini Dodoma, baada ya kuwaapisha mawaziri 21 na naibu mawaziri 22, ambapo Naibu Waziri mteule, Francis Ndulane uteuzi wake ulitenguliwa baada ya kushindwa kuapa.

“Ndani ya Serikali sasa hivi kuna ugonjwa mmoja, kwa sababu hata mawasiliano yanatumwa kwenye ‘ma-group’ wakati barua zingine ni za siri, mtu anasema tunatakiwa tukutane mahali fulani saa fulani na ajenda yetu ni hii na hii, unakuta labda Makatibu Tawala wa Wilaya wanaandikiana hivyo au Wakuu wa Wilaya au Mawaziri au Makatibu Wakuu na ndiyo maana siri ndani ya serikali zinavuja,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli aliwakumbusha viongozi wote serikalini kuwa serikali inafanyakazi kwa njia ya karatasi, hivyo teknolojia japo ni nzuri, lakini wanapaswa kuangalia wapi wanatakiwa kuitumia. Lakini, alisisitiza kwenye mambo ya serikali, wazingatie maadili ya viapo vyao.

Alisema hivi sasa kumekuwa na ‘ma-group’ mengi yakiwemo ya Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Makatibu Tarafa na Watendaji wa Kata, ambayo wakati mwingine yeye huingia kwenye makundi hayo na kuona yanayoandikwa yanavyoshangaza.

“Niwaombe, ndani ya serikali tufanye kazi zetu kwa uadilifu mkubwa, siyo kila kitu kinapelekwa kwenye ‘group’, yale yanayohusu utendaji na masuala ya maagizo ndani ya serikali, yafuate utaratibu wake. Najua kuna ma-group mpaka ya Polisi, unakuta saa nyingine mhalifu anatumwa kwenye WhatsApp na maeneo mengine. Hivyo, naomba ndani ya serikali tujitahidi sana kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na tuzingatie siri na maadili yetu tuliyonayo,”alisisitiza.

Aliongeza “Nataka mkafanye kazi, lakini sitaki ule muonekano wa kisasa yaani gari linateremka kwenye mteremko halafu unajipiga picha (Selfie) kwamba unavyoniona hivi sasa ndo nafungua mlango, naondoka na gari langu, ndo ninaenda kukagua mradi. Hayo ndugu zangu yamepitwa na wakati, ukifanya kazi utajulikana tu.”

Pamoja na angalizo hilo alilowapa, Magufuli alisema anaamini mawaziri na naibu mawaziri aliowateua na kuwaapisha, anawaamini na watakwenda kufanya maamuzi na kuchapa kazi kwa maslahi ya taifa na wananchi.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi