loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wafungwa 256 wafutiwa adhabu ya kifo

Wafungwa 256 wafutiwa adhabu ya kifo

RAIS John Magufuli amebadilisha hukumu ya wafungwa 256 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na kutamka kuwa wafungwe kifungo cha maisha. Pia amewapunguzia adhabu wafungwa wengine 3,316 waliofungwa kwa makosa mbalimbali.

Aliagiza wafungwa hao 3,316 wengine wapunguziwe adhabu na wengine waachwe huru, kwa kuzingatia mapendekezo yalitolewa na Kamishna Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee.

Alibadilisha hukumu hiyo jana Ikulu Chamwino jijini Dodoma wakati akiwaapisha mawaziri na naibu mawaziri. Pia jana ilikuwa kumbukumbu ya miaka 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara na aliwapongeza Watanzania wote kwa kusherehekea siku hiyo muhimu.

"Najua katika kipindi cha miaka mitano mpaka leo, nilitakiwa niwe nimewanyonga watu 256 waliohukumiwa kunyongwa, lakini sijamnyonga hata mmoja,"alisema Rais Magufuli.

Aliongeza "Kwa hiyo wale wafungwa 256, kwa mamlaka niliyopewa, nawapunguzia kifungo chao cha kunyongwa na sasa wafungwe maisha. Kwa sababu wapo waliohukumiwa kunyongwa kwa sababu waliua, labda mwingine aliua mtu mmoja au wawili au watatu, mimi sheria inaniambia niue 256. Nani mwenye dhambi zaidi? Huyu aliyeua mmoja au wawili au mimi nitakayeua 256?".

Magufuli alisema miongoni mwa wafungwa hao, wapo walioua mtu mmoja au wawili au watatu. Lakini yeye anatakiwa kuwaua hao 256. Alisema akifanya hivyo atakuwa ameua wengi zaidi kuliko hao wafungwa.

"Kwa hiyo nimeshindwa kuwaua. Mnisamehe kwa hilo kwa sababu mimi ndio nitakuwa muuaji wa kuuwa wengi kwa sababu wenzangu wameua mtu mmoja au wawili au watatu na wakahukumiwa kunyongwa, halafu mimi niue 256. Si nafuu mimi ninyongwe hapo hapo hata bila kupelekwa mahakamani?," alihoji Rais Magufuli.

Baada ya kubadilisha hukumu hiyo, aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani kushughulikia suala hilo la wafungwa 256 kwa kuzingatia taratibu na sheria ili wafungwe maisha na wafanye kazi.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi