loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa amuombea msamaha aliyeshindwa kuapa

Majaliwa amuombea msamaha aliyeshindwa kuapa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemuombea msamaha kwa Rais John Magufuli mbunge wa Kilwa Kaskazini, Francis Ndulane (CCM) aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Madini na kushindwa kuapa mbele ya Rais Jumatano iliyopita, kwamba anaweza kuangaliwa tena.

Majaliwa aliyasema hayo jana Ikulu Chamwino mjini Dodoma wakati wa kuapishwa kwa Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya.

Msamaha huo wa Waziri Mkuu, ulikuja baada ya Spika Job Ndugai kuchombeza kwamba kabla ya kumuapisha Profesa Manya kuwa mbunge alimuuliza kama anatoka Mkoa wa Lindi; na alipojibiwa kuwa hatoki Lindi, akasema basi leo (jana) hali itakuwa salama.

Majaliwa alisema asingependa sana kuzungumzia hoja ya Spika, kwa kuwa anajua kuwa eneo ambalo watu wanakula kiapo mbele ya Rais, siyo eneo la mzahamzaha, kwa kuwa hata yeye siku alipoitwa kuapa, ilibidi atumie nguvu kidogo.

“Kwa hiyo  Rais yaliyotokea juzi (Jumatano) si kwa wa Lindi tu, bali tuendelee kumuombea kijana wetu, naamini bado unaweza ukaangalia angalia,”alisema Majaliwa.

Kuhusu uteuzi wa Profesa Manya, Majaliwa alisema anamfahamu vizuri naibu waziri huyo kwa kuwa kati ya mambo makubwa yaliyofanyika kwenye madini yeye akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, amekuwa na mchango mkubwa, hivyo uteuzi wake ni sahihi.

Alisema wanaupokea uteuzi huo wakiwa na imani kwamba Profesa Manya atakwenda kufanya ufuatiliaji wa karibu pamoja na kutumia nafasi yake kufanya marekebisho kupitia chombo cha Bunge na kushiriki kikamilifu kuueleza umma wa Watanzania namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inavyoweka jitihada rasilimali ya madini inawanufaisha Watanzania.

“Nikiri kwamba uteuzi huu ni uteuzi sahihi, wizara sasa imepata watu ambao wanaifahamu kwa kuwa waziri mwenyewe amefanya kazi nzuri katika kipindi chake cha miaka mitatu iliyopita kwa kusimamia, kukemea na kuona namna rasilimali hii inaweza kuleta pato kubwa ndani ya taifa,”alisema Majaliwa

Aliongeza kuwa “Naibu Waziri ambaye leo (jana) ameshaapa, kwa yale yote ambayo nimeyazungumza kama mchango wake kwenye wizara, naamini sasa tumepata timu nzuri kwa kushirikiana na Katibu Mkuu, watendaji wa madini na wadau wa madini kutusaidia katika kutunza rasilimali hii ili iendelee kutuletea manufaa makubwa zaidi.”

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi