loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli apania Tanzania iwe kinara madini Afrika

Magufuli apania Tanzania iwe kinara madini Afrika

RAIS Magufuli amesema anataka kuona Tanzania inakuwa ya mfano katika madini, uchumi na kila kitu, hivyo ameitaka Wizara ya Madini ishirikiane na wizara zingine ili kufikia azma hiyo.

Aliyasema hayo jana Ikulu Chamwino Dodoma baada ya kumuapisha Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya.

Magufuli alisema sekta ya madini inaweza kutoa mchango mkubwa kwa taifa, kwa kuwa Tanzania ina madini ya kila aina yakiwemo chuma, coal, uranium. chuma, grahite, shaba, tin na mengine mengi.

Aliwataka wataalamu wa madini kujiuliza kwa nini Tanzania ina tani nyingi ya madini ya chuma, lakini haiyeyushwi na kutengenezwa nondo, na badala yake nondo zinatengenezwa kwa maturuma ya reli yanayoibwa.

“Haya ndiyo maswali magumu mnayotakiwa kuyafanya, yale mliyoyasoma kwenye nadharia myaweke kwenye vitendo na kuona ni kitu gani kimeshindikana kuwapatia maeneo ya kuchimba madini ya chuma wenye viwanda vya kutengeneza nondo na chuma ili wachimbe, hata kama ni kwa kuwapa bure kwa sababu atatengeneza ajira kwa watu watakaochimba chuma, kwenye sekta ya usafirishaji, ajira viwandani na serikali itakusanya mapato,”alisema Rais Magufuli.

Aliiomba Wizara ya Madini kulisimamia hilo, kwa kuwa hata wenye viwanda vya saruji wanalalamika hawapati madini ya coal ya kutosha.

“Tumesikia Kiwanda Cha Saruji Dangote kule Mtwara, akienda kule anapimiwa, na nimeambiwa kuna mtu amehodhi pale, sifahamu kama keshaondoka au bado yupo? Kwa nini hii coal ya Tanzania isitumike kama nishati mbadala wakati wataalamu wapo? Sasa ni jukumu la ninyi Wizara ya Madini kujipanga. Mfanye kazi vizuri usiku na mchana ili zawadi ya madini mengi tuliyopewa na Mwenyezi Mungu yaanze kutumika,”alisisitiza Rais Magufuli.

Alisema nchi jirani ya Uganda ina madini ya uranium na wameanza kuchakata madini hayo, lakini Tanzania madini hayo bado hayajafanyiwa kazi.

Kuhusu Profesa Manya, Rais Magufuli alimtaka akachape kazi, kwa kuwa amemteua kuwa naibu waziri wa madini, baada ya kuona wizara hiyo kwenye nafasi za juu ilikuwa inayumba kitaalamu kwa sababu waziri hajui madini kwani kitaaluma ni mwalimu, lakini pia Katibu Mkuu Profesa Simon Msanjila ni mtaalamu wa kompyuta, hivyo naye hajui madini.

“Tumeona tukuweke wewe ukawe kiungo kizuri kwenye wizara hii, wewe ni Profesa lakini haina maana kwamba maprofesa waliowahi kukaa kwenye Wizara ya Madini walifanya vizuri. Kwa hiyo nenda na mtazamo huu, kwa sababu tuliwahi kuwa na waziri na katibu mkuu maprofesa, tena wa madini, lakini mambo hayakwenda vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza kuwa, “Nataka kukutahadharisha wewe, utakapoenda kule usije ukaangukia kwenye mtego huu ambao maprofesa wenzako waliufanya walipokuwa Wizara ya Madini. Sitaki kukuficha, ni lazima nikueleze ukweli. Najua umefurahi na umeshangilia, na watu wako wa Tume ya Madini wameshangilia na nilijua walikuwa wanakwamishwa baadhi ya mambo kuyaamua, sasa kayaamue wewe.”

Alimueleza Profesa Manya kwamba kwa kuwa wapo maprofesa wenzake walioshindwa, ilimfanya ajiulize sana kuhusu uamuzi wake wa kumteua tena profesa. Hivyo, alimtaka akatumie taaluma yake katika kulinda ukweli.

Magufuli alisema sekta ya madini ni sekta muhimu, hivyo endapo wizara itajipanga na kuwahusisha wataalamu vizuri na kushirikiana vizuri, sekta ya madini inaweza kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

foto
Mwandishi: Na Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi