loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM apongeza kasi ya mawaziri

JPM apongeza kasi ya mawaziri

RAIS John Magufuli amewapongeza mawaziri na naibu mawaziri, kwa kuanza kazi zao vizuri baada ya kuwaapisha Desemba 9 mwaka huu Ikulu Chamwino Dodoma.

Aliyasema hayo jana mjini Dodoma, alipokutana nao kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Mawaziri, kilichofanyika Ukumbi wa Jakaya Kikwete.

Hatua hiyo ya Rais Magufuli kufungua kikao cha Baraza la Mawaziri kikiwa mbashara kupitia vyombo vya habari huku wananchi wakifuatilia, ni ya kipekee katika historia ya Tanzania kwa kuwa haijawahi kutokea.

Mara baada ya Rais Magufuli kuingia kwenye ukumbi wa mkutano wa kikao hicho, jambo lililofuata ni kuapishwa kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kazi hiyo ya kumuapisha Dk Mwinyi, ilifanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

“Nachukua nafasi hii kumpongeza Dk Hussein Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuapa kuwa Mjumbe wa baraza hili la mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nakupongeza sana na karibu kwenye kikao chetu,”alisema Rais Magufuli.

Aliongeza “Waheshimiwa wajumbe karibuni sana na hongereni sana kwa kuwa wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimeona leo (jana) tukutane hapa wote ili tujue mwelekeo, lakini kwa ujumla mmeanza vizuri, hongereni sana.”

Miongoni mwa mawaziri walionza kazi mara tu baada ya kuapishwa ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima.

Dk Dorothy alikutana na watumishi wa wizara hiyo Desemba 10 mwaka huu na kuwataka kufanya kazi kwa bidii ili wizara hiyo iwe kituo cha ubora katika uongozi kwa kutengeneza timu nzuri, itakayojibu mahitaji ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hotuba ya Rais Magufuli wakati akifungua Bunge la 12 ili waweze kuzijibu ahadi zote zilizotolewa zinazohusu wizara hiyo pamoja na shida za wananchi zinazojitokeza kama kero.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, baada ya kuapishwa alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Geita, Modest Apolinary ili kupisha uchunguzi kutokana na kununua gari lenye thamani ya Sh milioni 400.

Jafo pia alikagua ujenzi wa daraja katika Mto Msimbazi eneo la Ulongoni, Gongo la Mboto Dar es Salaam na ujenzi wa daraja katika Mto Ng’ombe eneo la Tandale Kwa Mtogole. Katika maeneo yote hayo, Jafo hakuridhishwa na kasi ya ujenzi na kuwataka wakandarasi kuongeza kasi ili wamalize kwa wakati.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, pamoja na mambo mengine alianza kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa), David Palangyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wake na kusema atapangiwa kazi nyingine.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ummy Mwalimu, alifanya ziara katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambapo aliitaka menejimenti ya NEMC kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira na kushughulikia changamoto ya utoaji wa cheti cha mazingira.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, wakati akiripoti ofisi za wizara hiyo, aliwataka wafanyakazi kujua kwamba wana wajibu wa kutekeleza Ilani na hotuba ya Rais Magufuli kwa kishindo kikubwa zaidi kuliko ilivyokuwa miaka mitano iliyopita. Hao ni baadhi tu ya mawaziri.

Lakini, kwa ujumla mawaziri na naibu mawaziri,  kila mmoja kwa wakati wake, alianza kazi mara moja mara baada ya kuapishwa kushika nyadhifa walizonazo.

foto
Mwandishi: Na Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi