loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli azuia fomu  za maadili mtandaoni

Magufuli azuia fomu za maadili mtandaoni

RAIS John Magufuli ameitaka Tume ya Maadili nchini, kuhakikisha fomu zote za maadili ya watumishi wa umma, zinajazwa na kurudishwa kwa mkono, badala ya kutumia njia ya mtandao ili kutunza siri za wahusika.

Aliyasema hayo jana Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kumuapisha Jaji Sivangilwa Mwangesi kuwa Kamishna wa Tume ya Maadili.

Magufuli alisema mtu anaweza kufanya mambo mengine yote kwa njia ya mtandao, lakini kurudisha fomu za maadili ya watumishi wa umma kwa njia ya mtandao ni kupoteza usiri na utakatifu wa idara hiyo, pale namba ya siri ya mhusika itakapojulikana na watu wengine.

“Nilimweleza Jaji Harold Nsekela na tulikubaliana kwamba mnaweza kuzipakua fomu kutoka kwenye mtandao, lakini ukishazijaza usizirudishe kwa njia ya mtandao, kila mmoja anajua anarudisha fomu yake wapi kulingana na nafasi yake ya kazi, nafahamu kwa mfano Mheshimiwa Spika huwa analeta kwangu, wewe (Mwangesi) unaleta kwangu, mimi nazileta kwako,”alisema Rais Magufuli.

Alisema kwa kuwa wanaojaza fomu hizo ni wengi wakiwemo wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala na wengine wengi, hivyo wanatakiwa kuzipakua hizo fomu kutoka mtandaoni, lakini wanaporudisha, wazirudishe mahali panapotakiwa wao wenyewe na siyo kuzirudisha kwa njia ya mtandao, kwa kuwa lazima kuwepo siri kwa fomu zao.

“Wadukuzi wapo wengi, unaweza ukajaza shilingi milioni 10, yeye akakujazia una shilingi milioni 100, halafu baadaye unakuja kuulizwa ulijaza una shilingi milioni 100 na saini yako ipo hapa, lakini pia uhalisia unapotea kwa kitu ambacho umekitoa nakala na kukiskani, kwa hiyo Tume ya Maadili msikubali kamwe kupokea fomu hizi kwa njia ya mtandao,”aliagiza.

Kuhusu umuhimu wa fomu hizo, Rais Magufuli aliwataka watumishi wa umma wanaopaswa kuzijaza fomu hizo, wafanye hivyo kabla ya Desemba 30 mwaka huu.

Alisema aliamua kumteua Kamishna wa Maadili mapema ili kusiwepo na kisingizio cha kutorudisha fomu hizo kabla ya Desemba 30, ambayo ndiyo kikomo kwa watumishi wote, akiwemo yeye mwenyewe na watumishi wengine zaidi ya 15,000 wanaotakiwa kuzijaza na kurejesha fomu hizo.

“Najua wengi ninapozungumza hapa hawajarejesha fomu, hata mimi fomu yangu nilikuwa sijarudisha, nitaijaza harakaharaka ili niweze kukufikishia hizi fomu kwa taratibu na sheria za nchi yetu,”alisema.

Katika kuwatakia Krismasi njema na heri ya Mwaka Mpya,  aliwataka watumishi kwenda kusherehekea sikukuu hizo majumbani mwao walau kwa siku nne au tano, kwa kuwa jambo hilo siyo baya, ila kwa viongozi waliozuiwa na Waziri Mkuu wakiwemo wakurugenzi watendaji, hawapaswi kwenda mpaka wakamilishe ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi, alisema ofisi yake itampatia ushirikiano wa kutosha Jaji Mwangesi katika majukumu yake ikiwemo kuhakiki mali zilizojazwa kwenye fomu.

Alisema lengo ni kurudisha nidhamu na maadili kwa watumishi wa umma na isitoshe asilimia 92 ya viongozi wa umma wanajaza fomu hizo na kutaja mali zao.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, alimpongeza na kumuahidi Jaji Mwangesi kupata ushirikiano kutoka wizara hiyo. Pia alimuomba Rais Magufuli awafikirie tena kuwaongezea majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, ombi ambalo rais alilikubali na kuahidi kulifanyia kazi.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi