loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wabunge EALA mnaiangusha EAC

KITENDO cha Spika wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Martin Ngoga kujitokeza hadharani kuwalalamikia wabunge wa bunge hilo kwa utoro kinaonesha dhahiri kuwa ndani ya chombo hicho kinachotunga sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna matatizo.

Martin Ngoga bila kutaja utaifa wa wabunge watoro alisema ni aibu kuona Bunge la Afrika Mashariki linashindwa kufanya shughuli zake sababu ya utoro wa baadhi ya wabunge ambao kila kukicha wanapeleka barua kwa Spika kuelezea kutokuwepo kwao katika chombo hicho muhimu.

Ina maana wabunge hawa walichaguliwa kwenda Arusha kwenye makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutumikia bunge hilo au kwenda katika mambo yao binafsi katika mataifa yao? Haiwezekani wabunge 27 kutoka mataifa sita wanachama kuchukua posho tu na kwenda katika matanuzi yao na kuacha jambo la msingi la kuwawakilisha wananchi wa EAC katika chombo hicho.

Hii ni aibu kubwa kwa wabunge hao ambao walichaguliwa katika mabunge ya nchi wanachama wa EAC ili kutekeleza majukumu ya chombo hicho muhimu kinachosaidia kuimarisha utangamano wa nchi zote zinazounda jumuiya hiyo.

Ni aibu pia kwa nchi zilizotoa wabunge hao kwa kuwa ndio wawakilishi wa nchi husika katika Bunge la EALA lenye wabunge 27 kutoka kwa nchi wanachama. Kila nchi inahitaji iwakilishwe vizuri na kwa maslahi mapana ya taifa na wananchi wake.

Kuna habari kuwa wabunge hao hawaonekani bungeni Arusha kwa sababu nchi zao zipo katika harakati za maandalizi ya chaguzi hivyo wana hofu ya kuangushwa katika majimbo yao, sababu ambayo haina mashiko.

Binafsi nakifananisha kitendo cha utoro wa makusudi katika Bunge hilo kama hujuma dhidi ya utendaji wa EALA kwa sababu utoro wa wabunge hao umesababisha shughuli nyingi kukwama mpaka sasa.

Kwa mujibu wa Spika wa Bunge hilo, miongoni mwa athari za moja kwa moja ambazo Bunge hilo limezipata kutokana na utoro wa wabunge ni pamoja na kushindwa kukaa kwa Kamati ya Bajeti ambayo ilitakiwa kujadili na kupitisha bajeti ya fedha kabla ya Mei 30, mwaka huu lakini mpaka sasa hilo halijafanyika.

Pia mawaziri wa EALA kutoka nchi zote sita za Afrika Mashariki wanatajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha mijadala katika Bunge hilo kwani wamekuwa hawana ushiriki mzuri katika vikao muhimu vya Bunge hilo.

Kwa kukwamisha utendaji wa EALA, wabunge hao wanarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana mpaka sasa hasa katika muktadha wa mtangamano wa jumuia nzima ya Afrika Mashariki.

Ni kutokana na utendaji wa pamoja na ushirikiano kwa mamlaka zote ndani ya jumuiya ndio maana mpaka sasa EAC ndio jumuiya bora kabisa barani Afrika. Kukwamisha shughuli za Bunge hili ni sawa na kuipoka jumuiya hiyo nafasi yake adhimu ya kuwa jumuiya bora Afrika na jumuiya ya pili bora duniani ikitanguliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU).

Ni vyema sasa itungwe sheria kali ambayo itamng’ata mbunge yeyote kutoka nchi yoyote atakayekosa kikao bila sababu za msingi. Sheria hiyo itamsaidia Spika wa EALA badala ya kulalamika atachukua hatua ya kukomesha tabia hiyo.

Bunge la Afrika Mashariki ambalo lilianzishwa mwaka 2001 ni moja kati ya mamlaka muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki inayohusisha nchi sita za Kanda ya Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Bunge hilo hutumika kutengeneza sheria za jumuiya hiyo likiwa na wabunge ambao huchaguliwa na mabunge ya nchi wanachama.

MACHI 8 kila mwaka ni maadhimisho ya kimataifa ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi