loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

BRENDA SEMAYA, Mtaalamu wa Benki aliyeamua kuwekeza kwenye keki

SIKU hizi kuna neno limekuwa maarufu, nalo ni kujiongeza. Neno hili lina tafsiri nyingi sana kulingana na kila mtu anavyotaka kulichukulia au kulitumia.

Wako waliotumia neno hili na limeleta faida katika biashara zao, kazi zao, masomo na maisha yao kwa ujumla kwani wamelichukua neno na kulifanyia kazi kwa vitendo, tunaweza kusema wamejiongeza kwa vitendo na kufanikiwa katika maeneo mbalimbali katika maisha.

Brenda Semaya ni mwajiriwa wa benki na aliamua kujiongeza kwa kufanya shughuli nyingine za kujiingizia kipato, pia kufikiria kuwanufaisha wengine wakiwemo watoto ambao anaamini wakijengewa msingi wowote kuanzia utotoni wanaweza kuja kusimama wenyewe wanapokuwa watu wazima wanaojitegemea.

Tangu akiwa katika umri mdogo alipenda sana kujishughulisha na alipenda kujiona akifika mbali na alianza kufanya juhudi kwa kusoma kwa bidii kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vikuu.

Brenda anasema pamoja na kuwa yeye ni mwajiriwa, amekuwa akipata msukumo wa kujiongeza na kufanya kitu anachopenda kujiongezea kipato.

Mwanadada huyu kijana alishawahi kumiliki duka la nguo za watoto na alikuwa anakwenda nchi mbalimbali nje ikiwemo Uturuki na Afrika Kusini lakini baadaye aliamua kuachana na biashara hiyo.

Lakini kumbe alikuwa na kipaji chake kingine, nacho ni kuoka na kupamba keki na kama utani alieleza ndoto yake hiyo kwa ndugu zake na kusema anageukia kwenye upishi wa keki na alikwenda kusomea kidogo masuala ya keki kama wenzetu wanavyosema ‘and the rest is history.’

“Kwanza ni namna ya kuongeza kipato, pia nilipenda nifanye kitu ambacho nakipenda, lakini hapohapo kitu cha kwangu mwenyewe, ujuzi ambao haupotei zaidi ya kuboresha, kazi ambayo ni endelevu kizazi na kizazi,” anasema.

Brenda alianza kutengeneza keki rasmi mwaka 2014 za vipande na kuanza kusambaza kwa ndugu, jamaa na marafiki, na kila aliyekuwa akizionja alizipenda, kisha alijiongeza na kuanza kutengenezea ndugu, marafiki keki za shughuli ndogo kama birthday na kila aliyekuwa akionja akipenda anamuelekeza mwingine.

Biashara hii ya keki imeendelea kuongezeka na wateja walianza kuongezeka wakitoa oda ya keki za shughuli kubwakubwa kama harusi, kitchen party, kipaimara, mahafali na aliamua kufungua duka lake la kwanza la keki maeneo ya Mwenge TRA likijulikana kama Heaven Cakes.

Mwaka jana katika likizo ya mwisho wa mwaka Brenda amechukua hatua nyingine kubwa, kwanza alihamisha sehemu yake ya biashara ya keki na kuhamia sehemu kubwa zaidi maeneo ya Sinza Mapambano na duka linajulikana kama Heaven Cakes na alijiongeza kwa kuamua kutumia kipaji chake cha kuoka na kupamba keki kusaidia malezi ya watoto mbalimbali katika jamii inayomzunguka kupitia mpango wake aliouita Kids Baking Camp1.

Brenda akiwa ni mtoto wa nne na wa mwisho katika familia ya Aidan na Joyce, alizaliwa miaka 35 iliyopita jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Olympio iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam na baadaye akajiunga na Shule ya Sekondani Zanaki kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne.

Elimu yake ya kidato cha tano na sita alipata katika Shule ya Sekondari Jangwani kisha alijiunga na Chuo Kikuu Iringa kwa masomo ya Shahada ya Usimamizi wa Biashara baadaye akajiunga na Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Shirika kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, kimsingi Brenda ni mchumi.

Akizungumzia Kids Baking Camp, Brenda anasema ni mpango unaohusisha watoto kuanzia miaka mitano hadi 13 akiwa na lengo la kuwafundisha kuoka keki, kuvumbua vipaji vyao lakini pia kuwajengea kujiamini.

“Ni mpango unaohusisha watoto kuanzia miaka mitano hadi 13, na nitakuwa nikifanya hivi kila wanapofunga shule ili waweze kujifunza vitu tofauti, lakini pia kuwaondoa katika malezi ya kuangalia katuni ambayo jamii kubwa ya watanzania imeyashikilia sasa.

“Unaweza kuona nimechukua watoto wadogo sana wa miaka mitano, hii ni kwa sababu naamini mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Katika kuwafundisha kuoka kuna vitu vingi tunafanya.

Kuna mengi tunalenga ndani ya mtoto, kwa mfano kitendo cha kumvalisha aproni hata kama ni mdogo hafanyi kitu kwake ina matokeo… ukimpa apime na ukachanganya naye unga tayari kwake anaona kaweza na anaongeza ari ya kujaribu zaidi lakini pia kuwaza kuwa nikiwa mkubwa nitafanya hivi,”anasema.

Brenda anasema mpango huu maalumu utakuwa ukifanyika wakati wa likizo kwa sababu ni wakati ambao watoto wako nyumbani wakitumia muda mwingi kuangalia katuni ambayo kwake anaona kuna kila sababu ya msingi kuwapunguzia matumizi ya katuni na badala yake wakaingiza kitu kwenye ufahamu hao kitakachokuwa na faida na manufaa maishani mwao.

Anasema mpango huo ambao anatarajia uwe endelevu umeanza mwaka jana Desemba mpaka Januari, 2021 ukiwa na watoto 20.

Brenda anasema kambi hiyo itakuwa inafanyika wakati wa likizo tu lakini baada ya kambi kuvunjwa watakuwa wanafuatilia maendeleo ya kile walichowafundisha wakati wa likizo.

Mbali na kufundisha watoto, Brenda pia ana madarasa ya kufundisha wakubwa kuoka na kupamba keki, hivyo yeyote mwenye matamanio ama mwenye ndoto ya kupika na kupamba keki anaweza kujiunga.

Wito kwa wanawake Brenda anasema, “wanawake Mungu ametupa akili kubwa sana tukiitumia vizuri lazima ufanikiwe.

Kwanza uthubutu ni jambo kubwa kwenye maisha, usiogope kuanza mimi nilianzia jikoni kwangu na oveni ndogo ya nyumbani, sikujua nitauza wapi ila nilijua ipo siku na mimi nitakua na wateja watataka bidhaa zangu sikuangalia mazingira.

“Jambo la pili uvumilivu, wengi tunaanza jambo vizuri kwa nguvu changamoto zikitokea unakata tamaa na pengine kuacha ili uhamie kituo kingine lazima ukubali kuinu mguu na kutumia nguvu kwenda mbele na kufanikisha kile ulichokinuia au ulicholeanga kukifanikisha.”

Ndoto ya Brenda, mke na mama wa watoto watatu wa kike ni kuoka mikate, kutengeneza cookies, maandazi na chapati. Mwaka jana wakati anafungua kambi ya watoto kujifunza alifanya majaribio ya kuoka mikate lakini rasmi anatarajia kuanza Januari mwaka

WANAWAKE wamekuwa ni chachu kubwa ya ...

foto
Mwandishi: Anna Mwikola

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi