loader
Wizara yakerwa kukosekana mabaraza ya ardhi, nyumba

Wizara yakerwa kukosekana mabaraza ya ardhi, nyumba

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewaagiza makatibu tawala wa mikoa wateue wajumbe washauri wa mabaraza ya ardhi na nyumba wahudumie wilaya zisizo na mabaraza hayo.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk Angeline Mabula alitoa agizo hilo jana mkoani Lindi wakati akizungunza na watendaji wa sekta ya ardhi, uongozi wa mkoa huo na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa.

 

Dk Mabula alikuwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

Alitoa agizo hilo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kueleza kuwa  mkoa huo una baraza moja la ardhi na nyumba linalohudumia wilaya zote tano za mkoa huo jambo alilolieleza limekuwa likileta usumbufu na kero kwa wananchi kutembea umbali mrefu.

 

"Mkoa wetu una baraza moja tu la ardhi na nyumba la wilaya linalohudumia wilaya za mkoa huu, fikiria mtu anatoka Liwale kuja hapa umbali wa kilometa 250 ni kumuumiza mwananchi," alisema Zambi. 

Kwa sasa kuna jumla ya mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya 57 yanayotoa huduma nchini wakati sheria inataka kuwa na mabaraza 139 hivyo kusababisha baadhi ya wilaya kukosa huduma za mabaraza hayo.

 

Dk Mabula alisema baada ya serikali kuona wananchi wanapata shida ya kuzipata huduma za mabaraza ya ardhi imeamua kuwaelekeza makatibu tawala wa mikoa wateue wajumbe washauri wa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.

Pia aliwataka wakurugenzi wa halmashauri watenge ofisi itakayoendesha mashauri na kuwa na watumishi kama makarani ili kuwawezesha wenyeviti kufanya kazi kulingana na mahitaji ya wilaya husika. 

"Pamoja na kuwa na mabaraza ya ardhi katika wilaya mbalimbali lakini tumeona bado kuna 'gape' mahali hasa zile wilaya ambazo hazina mabaraza ya wilaya, maana baraza la wilaya moja linahudunia wilaya tatu kwa hiyo bado hatujatatua tatizo la wananchi kusafiri umbali mrefu kwa kusogeza huduma kwa wananchi wanaoteseka," alisema Dk Mabula.

Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kwa mujibu wa sheria Na 2 ya mwaka 2002 lina wajumbe wasiozidi saba na watatu kati yao ni wanawake.

Wajumbe hao huteuliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na mapendekezo ya mkuu wa mkoa kutoka katika eneo la wilaya husika.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e7c3a2e488b7c2c62add44f1e4927cf9.jpg

WAFANYABISHARA mbalimbali wa Temeke, ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Lindi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi