loader
Dstv Habarileo  Mobile
Neema ya kiuchumi yashuka Ziwa Nyasa

Neema ya kiuchumi yashuka Ziwa Nyasa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amezindua safari ya meli mpya ya MV Mbeya II itakayotoa huduma katika Ziwa Nyasa nchini na nchi jirani za Msumbiji na Malawi.

Meli hiyo yenye thamani ya Sh bilioni 9.1 ni mwendelezo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kwa lengo la kuboresha uchumi.

Alizindua safari za meli hiyo jana katika Bandari ya Mbamba Bay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma. Aliwataka wananchi waitunze meli hiyo ambayo imejengwa na kampuni ya Kitanzania ya Songoro Marine.

Alisema Tanzania imezungukwa na nchi nane ambazo zinategemea kupata bidhaa mbalimbali kutoka nchini. “Wananchi tumieni fursa ya uwepo wa meli hii kufanya biashara,” alisema Majaliwa.

Meli hiyo ni kati ya meli tatu zilizotengenezwa na serikali kwa ajili ya kuhudumia wananchi wanaotumia Ziwa Nyasa. Alisema serikali imetumia zaidi ya Sh bilioni 20.1 kutengeneza meli tatu zitakazofanya kazi ya kusafirisha abiria na mizigo Ziwa Nyasa na ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kazi nzuri inayofanya.

Alisema Mkoa wa Ruvuma ni kati ya mikoa muhimu iliyopewa kipaumbele kutokana na uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula kwa wingi.

Alisema serikali imedhamiria kufungua milango ya utalii kwa kutumia Ziwa Nyasa, na akasisitiza kuwa lengo la serikali ni kutaka kila mmoja kutumia fursa hiyo kujiletea maendeleo badala ya kukaa na kulilia.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alisema Serikali ya Awamu ya Tano ni ya vitendo badala ya maneno na kauli hiyo imedhihirishwa baada ya kutengeneza meli ambayo imeanza safari katika ziwa hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema katika kuboresha huduma katika bandari zote za Ziwa Nyasa, wameweka mikakati ya kuimarisha huduma ya usafiri Ziwa Nyasa ili Watanzania wafanye shughuli zao za uchumi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa barabara ya Mbinga- Mbambabay mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilometa 66 na kuridhishwa na kazi iliyofanyika.

“Nimekuja na barabara hii nateleza tu, wakati ule ulikuwa unatembea katika mawe, makorongo lakini sasa unalala tu. Naipongeza kampuni ya CHICO kwa ujenzi wa mradi huu,” alisema Waziri Mkuu jana.

Alisema kukamilika kwa barabara hiyo pamoja na kuanza kwa safari ya meli ni ukombozi wa kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa na ukanda mzima wa kusini. “Sasa Nyasa imefunguka,” alieleza.

Meneja wa Wakala wa Barabara wa Mkoa wa Ruvuma, Alinanuswe Lazeck alisema ujenzi barabara ya Mbinga-Mbamba Bay yenye urefu wa kilometa 66 umegharimu Sh bilioni 129.361.

Alisema baada ya kukamilika kwa barabara ya Mbinga Mbambabay, serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mbambabay Liuli, Lituhi hadi Kitai kwa lengo la kuchochea maendeleo hasa ikizingatia kuwa barabara hiyo ni muhimu kutokana na kutumika kusafirisha makaa ya mawe kwenda Bandari ya Ndumbi.

foto
Mwandishi: Muhidin Amri, Nyasa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi