loader
Dstv Habarileo  Mobile
Chuo cha Uongozi na Itikadi cha Mwalimu Nyerere Kielelezo kingine cha urafiki wa China, Afrika

Chuo cha Uongozi na Itikadi cha Mwalimu Nyerere Kielelezo kingine cha urafiki wa China, Afrika

“SOMENI barabara historia ukiielewa barabara historia utaepuka vikwazo na dhambi za ubeberu na ubaguzi wa rangi.”

 

Hayo ni maneno ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na maneno hayo ndiyo kaulimbiu ya Chuo cha Uongozi na Itikadi cha Mwalimu Nyerere kinachojengwa Kwa Mfipa wilayani Kibaha mkoani Pwani.

 

Kinajengwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na kimepewa jina la Mwalimu Julius Nyerere ili kuenzi jitihada zake za mapambano dhidi ya unyonyaji. Chuo hicho kinasimamiwa na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kimekamilika kwa sasa.

 

Kutokana na urafiki uliopo baina ya Tanzania na China, umeinufaisha Tanzania ambapo urafiki huo umezaa matunda ya baadhi ya miradi mikubwa na ya kihistoria ikiwamo ujenzi wa Chuo cha Uongozi na Itikadi ambacho kinajengwa na nchi hiyo ikiwa ni matunda ya urafiki huo.

 

Chuo hicho kinachojengwa na China ni sehemu ya vyombo vya uongozi wa siasa vikiwemo vyama vya kisiasa huku vyama rafiki vilivyoshiriki kwenye kwenye chuo hicho ni CCM, ANC cha Afrika Kusini, SWAPO cha Namibia, ASPLA cha Angola, ZANU PF cha Zimbabwe, na FRELIMO cha Msumbiji, vikiwa na mahusiano na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).

 

Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo hicho Julai 16, 2018, Rais John Magufuli alisema kitakuwa mkombozi kwa viongozi watakaopata mafunzo hapo juu ya kuwaletea maendeleo wananchi. Mradi huo una thamani ya Sh bilioni 100.

 

Rais Magufuli alisema kwa kuwa viongozi watapikwa hapo itasaidia kuwa na viongozi ambao watakuwa na maadili hivyo kuwa viongozi bora watakaowaletea maendeleo wananchi wa nchi za kusini na Afrika nzima.

 

“Tumeona vyama vingi havina itikadi hivyo kuanizishwa kwa chuo hichi ni mkombozi kwa wananchi kwani watapata viongozi ambao watakuwa wameandaliwa kwa kuwa na maadili mema,” alisema Rais Magufuli.

 

Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa aliwataka makatibu wakuu wa vyama hivyo kukamilisha taratibu zikiwamo wanafunzi watakaosoma na malipo ya watumishi na wakufunzi, na kuwapongeza kukiita jina la mwasisi wa Taifa la Tanzania akiamini watazalishwa watu wa aina yake wengi.

 

Alitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na Chama cha Kikomunisti kinachotawala nchini China (CPC) kwa kusaidia kufanikisha kujengwa kwa chuo hicho kwani kimeonesha urafiki kwa vyama hivyo vya ukombozi Kusini mwa Afrika.

 

Aliwataka makatibu wakuu wa vyama sita ambavyo vinashirikiana kuweka mipango mizuri ikiwemo mitaala na kuwapata wakufunzi kukamilisha taratibu mapema kabla ujenzi haujakamilika.

 

Akitoa salamu za Chama cha Kikomunisti cha China, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Kimataifa cha CPC, Song Tao alisema wamekuwa wakipambana na ukoloni na ubeberu na kuziletea maendeleo nchi za kijamaa.

 

Song alisema lengo ni kuwaletea maendeleo wananchi wa nchi zinazoendelea kwa kuwa na ushirikiano wa kimaendeleo kupitia vyama vya ukombozi.

 

Makatibu wa vyama hivyo walikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuweka utaratibu wa uongozi kwani tangu harakati za kujikomboa kwa nchi za Kusini mwa Afrika, Mwalimu Nyerere aliwakaribisha viongozi wenzake na kuzikomboa nchi hizo.

 

Naye Balozi wa China nchini, Wang Ke alisema chuo hicho ni kama jukwaa la ujenzi wa uwezo wa uongozi na itikadi kwa vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika na misingi ya ushirikiano kati ya China na chama tawala cha Kikomunisti cha CPC na CCM.

 

Alisema misingi minne ni muhimu ni pamoja na uhuru wa kujiendesha kama taifa huru, usawa wa mahusiano bila kujali ukubwa wa Taifa na wananchi wake na heshima baina ya nchi zao na kutoingilia mambo ya ndani ya nchi.

 

Alisema misingi hiyo minne inaongoza ushirikiano uliopo CCM na CPC na Taifa la Tanzania ambao urafiki huo ulianza tangu enzi za utawala wa Rais wa Kwanza wa China, Mao Tse Tung na Mwalimu Julius Nyerere.

 

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema ujenzi wa chuo hicho utasaidia viongozi kuwa na uelewa wa mambo na kuwa na utambuzi kwani licha ya nchi za Afrika kuwa na rasilimali nyingi lakini bado ni maskini na tegemezi.

 

Akielezea kuhusu harakati za nchi za Afrika kujikomboa, alisema Desemba 14, 1960 Baraza la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuzikubali nchi za kikoloni na wananchi waliokuwa chini ya ukoloni kuwa wanastahili kuwa huru na ni azimio muhimu kwa ukombozi wa nchi za Afrika.

 

“Kikao hicho namba 15 azimio lake linajulikana kama Azimio Namba 1,524 ambapo nchi zilizokuwa kwenye baraza hilo zilipigwa kura ambapo nchi za Afrika zilikuwa hazijapata uhuru ikiwemo Tanzania na zilikuwa zikiendelea na mapambano ya kupata uhuru na nchi 89 ziliunga mkono azimio hilo huku nchi tisa hazikuunga mkono azimio ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini iliyokuwa na uhuru bandia hazikukataa wa kukubali bali hazikupiga kura,”alisema Dk Bashiru.

 

Alisema miongoni mwa mataifa makubwa ambayo hayakuunga mkono ndiyo mabingwa na walimu pia ni mapolisi wa dunia kuhusu uhuru na haki za binadamu kwani azimio hilo lilitamka bayana kwamba dunia ya mwaka 1960 haikustahili kuendesha siasa za kimataifa wakati nchi nyingine ziko chini ya ukoloni zinastahili kuwa huru na Urusi iliweka msukumo kwenye azimio hilo.

 

“Azimio hilo lilisema kuwa haiwezekani kuendesha siasa za kimataifa huku nchi nyingine ziko chini ya ubaguzi wa rangi zinatawaliwa, rasilimali zake bado zinaporwa watu wake wanadhulumiwa na kunyimwa haki zao, lilikuwa azimio la aina yake.

 

“Hivyo tarehe 14 Desemba ni siku muhimu sana kusherehekea azimio la Umoja wa Mataifa kutambua kwamba ukoloni ilikuwa ni unyama kutimiza miaka 60 baada ya azimio hilo nchi zilikuwa huru na lisingepitishwa nchi isingeweza kupiga kura,” aliongeza.

 

Alisema kaulimbiu ya chuo hicho ilitolewa na Mwalimu Nyerere kuwa ukijifunza barabara historia utakuwa na uwezo na ujuzi wa kukabiliana na dhambi na maafa ya ubeberu na ubaguzi wa rangi ni hekima ya Mwalimu na falsafa muhimu.

 

Aliongeza kuwa chuo hicho hakijaitwa jina lake kwa bahati mbaya kwani alikuwa mwalimu mzuri, mwanafalsafa mzuri na alikuwa kiongozi bora na mwanasiasa bora Afrika na dunia, mchango na falsafa ya Nyerere kupitia chuo hicho itakuwa nyenzo ya kujifunzia.

 

Alibainisha kampuni iliyojenga chuo hicho ya CRJE, imejenga miradi ya kihistoria nchini ikiwamo Reli ya Tazara maarufu Reli ya Uhuru, Daraja la Mwalimu Nyerere, Kigamboni na Nyerere Square.

 

“Natoa pongezi kwa Rais Mstaafu, Dk Jakaya Kikwete, na Katibu mkuu mstaafu, Kanali Abdulrahman Kinana kwani wao ndiyo walijadili kwenye vikao vya chama na vyama vingine rafiki na kuanzisha mchakato wa majadiliano na alikabidhiwa nyaraka za ujenzi wa chuo hicho. Wazo hilo ni zuri kuwa na vyuo vya itikadi kwa ajili ya kujenga Taifa,” alisema Dk Bashiru.

 

Mratibu wa ujenzi wa chuo hicho, Emanuella Kaganda alisema ulianza mwaka 2018 na umekamilika licha ya kuchelewa kidogo kutokana hali ya mvua na ugonjwa wa Covid-19. Alisema ujenzi huo ulipaswa kukamilika Julai mwaka jana.

 

Alisema kutokana na changamoto hizo, baadhi ya vifaa kutoka China vilishindwa kuingizwa nchini hivyo kufanya baadhi ya malighafi kukosekana na kusababisha kuchelewa huko kwa ujenzi.

 

Alibainisha kuwa manufaa yaliyopatikana ni pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 3,000 ikiwa ni pamoja na mafundi na vibarua huku akina mama zaidi ya 30 wajasiriamali walikuwa wakitoa huduma za vyakula kwa mafundi.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/c9d7bf29add983da644cd53a1bc889b4.JPG

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: John Gagarini

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi