loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli aiomba China iifutie madeni

Magufuli aiomba China iifutie madeni

RAIS John Magufuli ameiomba Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China isaidie Tanzania katika miradi mikubwa mitatu pamoja na kuwafutia madeni.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo aliposhuhudia utiaji saini wa kampuni za China na Tanzania katika kukamilisha kipande cha tano cha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

Akizungumza baada ya utiaji saini wa mradi huo, Rais Magufuli amesema katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi amepokea salamu kutoka kwa Rais wa China, Xi Jinping, lakini pia amempa waziri huyo salamu zake azifikishe kwa Rais huyo wa China ikiwemo ombi lake la kutaka wamsaidie ujenzi wa miradi mikubwa hapa nchini.

“Nimeomba watusaidie katika miradi mikubwa mitatu, ule wa Hydroelectricity power wa Njombe Rumakali na Luhuji, nimeomba watujengee barabara kuu ya kilometa 148 kule Zanzibar, lakini pia nimeomba watufutia madeni yetu likiwemo lile tulilolibeba wakati tunajenga reli ya TAZARA la dola milioni 15.7,” amesema Rais Magufuli.

Ametaja madeni mengine aliyoomba kufutiwa ni la nyumba za askari, Dola milioni 137, deni lingine ni la kiwanda cha Urafika Dola milioni 15.

“Watufutie tu kwa sababu nchi ya China ni rafiki yetu na ni nchi tajiri, Mheshimiwa waziri amesema atalifikisha hili ombi,” amesema Rais Magufuli.
Ameongeza,  “Watusamehe tu kwa sababu ndani ya miaka kumi tumeshawapa makandarasi wa China trilioni 21, naamini maombi yetu yatakubaliwa.”

Aidha, Rais Magufuli amesema pia amemueleza hali halisi kuwa China ni nchi tajiri na Tanzania ina mazao mengi ambayo yanaweza kupelekwa China.

“China ni nchi tajiri na sisi tuna mazao mengi tunayoweza kuyapeleka China na ndiyo maana katika zawadi zangu nimetoa korosho, majani ya chai na kahawa nikiamini kuwa Wachina wakila tu nusu kilo ya korosho zetu maana yake watakuwa wanakula tani milioni 750 kwa maana sisi tupo watu milioni 64 na wao wapo bilioni 1.5 kwa hiyo wakila korosho za Tanzania zitaisha zote,” amesema na kuwataka Watanzania wachangamkie fursa kwa kuongeza thamani za mazao na kuuza China.

“Kwa ujumla mazungumzo tuliyoyafanya yalikuwa mazuri na nimemhakikishia Tanzania itaendelea kushirikiana na China kwa sababu ni ndugu zetu, sasa ni wakati wa Tanzania na China kujenga uchumi kwa nguvu zote na kuonesha ushirikiano mkubwa,” alisema Rais Magufuli.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi