loader
Dstv Habarileo  Mobile
China yaahidi kusaidia wavuvi

China yaahidi kusaidia wavuvi

SERIKALI ya China imeahidi kusaidia sekta ya uvuvi kuinua kipato na maisha ya wavuvi nchini.

Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Baraza la Taifa la China, Wang Yi amekaribisha soko la samaki wa

Tanzania kuuzwa moja kwa moja nchini humo.

Alitoa ahadi hizo jana baada ya kutembelea mwalo wa Chato mkoani Geita ambako alipata fursa ya kuangalia shughuli za uvuvi kwa wavuvi wadogo.

“Nimeambiwa wakati wa mvua Tanzania hali inakuwa ngumu sana na pia soko la samaki huko China pia ni kubwa. Kwa hiyo ningependa kutangaza kwamba China inakaribisha samaki kutoka Tanzania na pia tungependa kuwasaidia kuongeza mapato na kuboresha maisha yenu,” alisema Wang ambaye jana alikamilisha ziara yake ya siku mbili nchini.

 Alifurahishwa na kuonana na wavuvi na alitangaza kuwa Ubalozi wa China nchini Tanzania kutoa dola za Marekani 20,000 kwa ajili ya kuwasaidia kununua vifaa vya uvuvi.

“Leo ninayo furaha ya kutembelea hapa na kuonana nanyi. Pia tumembiwa mnazalisha samaki wengi na wazuri sana na wengine wanauzwa China. Mara kwa mara tunapokua Beijing mimi na mwenzangu tunakula samaki katika mghahawa mmoja, lakini tulikuwa hatujui kuwa wanatoka Tanzania, leo tumejua kuwa wanatoka Tanzania,” alisema.

Kuhusu zawadi, alisema, “leo ninyi mmenizawadia samaki wazuri na wakubwa sana, nimefurahi sana na nashukuru sana, kitendo hili kinonesha hisia zenu na urafiki wa kweli.”

“Tanzania na China ni ndugu na marafiki, na sisi tunapenda kusaidia marafiki wa Tanzania katika kuendeleza sekta ya uvuvi ili muweze kupata maisha mazuri zaidi.”

Awali, akitoa taarifa ya sekta ya uvuvi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema Tanzania imejaliwa rasilimali za uvuvi katika maeneo mbalimbali ya maziwa, mito, bahari na maeneo oevu.

Alisema sekta ya uvuvi inatoa mchango mkubwa katika kuwezesha wananchi kupambana na umasikini na imezalisha ajira nyingi za moja kwa moja kwa wavuvi.

Alisema zaidi ya wananchi milioni 4.5 wanajishughulisha na shughuli mbalimbali katika mialo na sekta ya uvuvi inawapatia kipato na lishe wananchi na kuchangia Pato la Taifa.

Ndaki alisema wavuvi hao wanazalisha wastani wa tani 3.5 huku asilimia 85 ya mazao ya uvuvi yakiwamo  yanayosafirishwa nje ya nchi, yanatokana na wavuvi wadogo wadogo ambao hutumia vyombo vidogo vya kuanzia meta tatu hadi meta 10.

“Wengi wao wanashusha mazao yao kwenye mialo midogo kama vile mwalo wa Chato,” alisema na kuongeza kuwa asilimia 75 ya mazao ya uvuvi yanayozalishwa nchini yanavunwa kutoka Ziwa Victoria.

Kwa mujibu wa waziri, Ziwa Victoria huzalisha mazao matatu ya kibiashara ambayo ni samaki aina ya sangara, sato na dagaa. Mazao yatokanayo na sangara yanayojumuisha minofu na mabondo na husafirishwa kwa wingi kwenda kwenye soko la kimataifa ikiwamo China.

“Soko kuu la mazao ya mabondo huuzwa nchini China kwa kupitia Hong Kong. Ni azima ya serikali yetu kuuza zao hili nchini China moja kwa moja,” alisema.

Alisema, “Matarajia yetu ni kuwa tutasaini mkataba kuwezesha kuuza bidhaa hizo moja kwa moja katika soko la China. Tunaomba mheshimiwa waziri (Wang Yi) mara tutakapowasilisha rasmi maombi ya soko la mabondo tuungwe mkono na Serikali ya China.”

Alisema wana imani kufunguliwa kwa soko hilo kutasaidia jitihada za wananchi kujikwamua na umasikini. Alisema Tanzania ina mialo 1,373 ikiwamo mwalo wa Chato.

“Hivyo kupitia kwako (Wang Yi) tunaiomba Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuhamasisha makampuni binafasi kutoka China yaje kuwekeza katika viwanda na miundombinu ya uvuvi ili kuongeza uzalishaji kupunguza upotevu wa rasilimali za uvuvi na kuongeza ubora na usalama wa mazao ya uvuvi,” alisema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wavuvi katika mwalo wa Chato, Kamese Kalima alisema mwalo una changamoto kadhaa ikiwamo inayohusu miundombinu, ambazo wamemuomba kiongozi huyo wa China kuwasaidia.

 Kalima aliomba China kuja kuwekeza viwanda vya kuchakata samaki angalau tani 35 kwa siku.

Akiwa mwaloni, Wang alipata fursa ya kuangalia shughuli za uvuvi zikiendelea na namna mabondo (utumbo) yanavyotolewa katika samaki na kukaushwa. Alishuhudia aina mbalimbali za samaki ambazo wavuvi walimzawadia.

 

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Chato

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi