loader
Dstv Habarileo  Mobile
China yakunwa na maendeleo ya Tanzania

China yakunwa na maendeleo ya Tanzania

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Baraza la Taifa la China, Wang Yi ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua za maendeleo.

Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Chato jana, Wang Yi alisema, “tunafurahi kuwapo Chato, tumejiona Tanzania ilivyopiga hatua ya maendeleo, tunawapongeza sana Watanzania.”

Alisema Tanzania ni rafiki mkubwa wa China ukilinganisha na nchi zingine za Afrika.

“Tuna maandishi na maandiko mengi ya habari za kusisimua kuhusu uhusiano wa Tanzania na China. Hatutasahau uhusiano wa muda mrefu uliojengwa na waasisi wa mataifa yetu, Mao na Mwalimu Julius Nyerere na kiongozi wetu alitembelea Tanzania mara 13.

“Na hatutasahau wananchi 15,000 wa China walioshiriki ujenzi wa Tazara na 55 walipoteza maisha wakati wa kutekeleza mradi huo mkubwa na hiyo ni alama kubwa ya ushirikiano wa nchi hizi mbili.”

Alisema nchi hiyo haitasahau jinsi nchi za Afrika na hasa Tanzania zilivyopigania China kuingizwa kwenye Umoja wa Mataifa na Baraza la Ulinzi na pia mchango wa Dk Salim Ahmed Salim akiwa Katibu wa Umoja wa Afrika katika hili na ndio maana mwaka 2019 walimpa zawadi.

Waziri huyo alikumbusha kauli ya Rais wa China, Xi Jinping ambaye alisisitiza ushirikiano wa China na Afrika ujengwe katika msingi wa maslahi ya wote.

Akizungumzia mazungumzo yake na Rais John Magufuli, Wang alisema wamekubaliana kuendelea kuwa na malengo ya pamoja kati ya vyama vya siasa na wizara kwa mipango yenye manufaa kwa pande zote.

Alisema katika mazungumzo hayo pia wamekubaliana kuendela kushirikiana katika masuala ya kimataifa ikiwamo kulinda na kutoingiliwa katika siasa za ndani na kulinda uhuru wa mataifa mengine.

“Nimefanya ziara ya 15 Afrika, nimeona pamoja na magumu inayopitia nchi za Afrika na migogoro iliyopo, lakini China inahakikisha wanaimarisha ushirikiano  na nchi za Afrika kwa kuhakikisha malengo ya kila upande yanafikiwa,” alisema Wang Yi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema lengo la Tanzania ni kuhakikisha bidhaa nyingi za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi inauzwa zaidi China na kampuni zao zinakuja kuwekeza nchini.

Alisema malengo wa Serikali ya Rais John Magufuli ni kujenga Tanzania ya viwanda ili ijitegemee.

“Ili tuwe nchi ya viwanda, tunahitaji miundombinu, tuhitaji nishati na tunahitaji kufanya biashara na mataifa mengine, tumefanya mazungumzo na China kwa sababu tunataka kufanya biashara na China na kuuza na China.

“Tunataka tuuze zaidi China na wao kuwekeza ili kujenga Tanzania kuwa na uchumi imara na inayojiamini na inajitegemea na ili iendelee kutoa mchango zaidi,” alisema Profesa Kabudi.

Alisisitiza, “Msimamo wa Tanzania utakuwa kama ilivyokuwa Nyerere na Salim Ahmed Salim kuwa ni huo huo na kama tuliweza tukiwa taifa masikini, hivyo na sasa tutaweza.”

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Chato

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi