loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

MWAMVITA MAKAMBA: Anayeamini nafasi ya mama katika malezi ya msichana

*Aandika kitabu cha malezi ya msichana

*Kitabu kuuzwa nchi Nigeria, Uganda, Kenya, Zambia

 

KWA kawaida wazo analokuwa nalo mtu na akaamua kulifanyia kazi kwa ufanisi ni lazima lizalishe kitu iwe kikubwa au kidogo na pengi hata miradi yenye kuleta mabadiliko ya maisha katika jamii.

Wazo linaweza kutokana na kitu ambacho mtu amepitia au amesomea na kuamua kutumia uzoefu wake kutekeleza wazo linalokuja kutoa suluhisho juu ya changamoto fulani anayoiona kwenye jamii au anataka isije kutokea kwenye jamii.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Mwamvita Makamba, mwanamke ambaye jina lake siyo geni masikioni mwa watanzania wengine, kwa sasa ni Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom- Afrika Kusini pia ni mjasiriamali anayemiliki kampuni ya uwekezaji inayowakutanisha wawekezaji na taasisi husika za uwekezaji kwenye nchi husika iitwayo MM Connect Africa.

Akiwa na nafasi hizo tatu Mwamvita ameamua kuandika kitabu kiitwacho “Things I tell my Daughter” hapa ndiyo kile nilichoeleza kuwa wazo linakuja kubadilisha, kujenga, kuimarisha maisha ya watu katika jamii lakini wazo hilo linakuwa na namna linavyokuja.

Akiwa mfanyakazi na mjasiriamali nafasi ambazo kwa mujibu wake amekuwa akitumia akili na uwezo wake wote kusimamia, amezifanya kwa ubunifu mkubwa lakini wakati wa likizo ya ya zuio la kutoka kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona akajikuta akipata nafasi kubwa zaidi ya kuwajibika kama mama kwa binti yake aitwaye Malaika(14).

Haina maana ya kuwa muda wote hakufanya majukumu yake kama mama ila kipindi hicho cha corona biashara zilikuwa zinasuasua na wafanyakazi wakitakiwa kufanyia kazi nyumbani, ndipo akajikuta akiwa na muda mwingi zaidi na binti yake huyo.

Mwamvita anasema kuwa siku moja akiwa nyumbani kwake Johannesburg, Afrika Kusini na binti yake huyo ambaye naye shule zilikuwa zimefungwa kutokana na ugonjwa huo, alijikuta akitathmini maisha yake tangu alipoanza shule ya msingi, sekondari, chuo kikuu hadi kuanza kazi.

Anasema akiwa kwenye takafari hiyo alikuwa kila wakati akiona nguvu na nafasi ya mama yake mzazi katika mafanikio yake sasa.

 

Mwamvita anakumbuka kuanzia namna alivyokuwa mkali, usimamizi, ufuatiliaji wa mama yake huyo kuanzia kwenye masomo yake, marafiki zake hadi maisha yake kwa ujumla kama mtoto.

 

Anasema alizikumbuka sauti za mama yake huyo kuanzia akiwa anaanza darasa la kwanza wakati huo akisoma shule mbalimbali za mikoa ya Lindi, Tanga na Morogoro na kuwa mama yake huyo alikuwa mstari wa mbele kuzungumza naye na kumfuatilia katika masuala ya masomo.

 

Hata alipoanza elimu ya sekondari katika shule ya sekondari za Kifungilo kisha Kilakala kidato cha tano kisha cha sita katika shule ya sekondari ya Shaban Robert bado mama yake  alikuwa nyuma yake na alikuwa akizungumza naye na kumuongoza katika masuala mbalimbali kama dada mkubwa.

Mwamvita anasema kuwa alikuwa akikumbuka sauti zote za mama yake hasa alipokuwa akimsihi masuala ya masomo, afya na kujilinda kama mtoto wa kike na muda huo alikuwa dada mkubwa wa kidato cha tano na sita.

 

Kwa mujibu wa Mwamvita alizikumbuka sauti za mama yake na zilivyomsaidia kumfikisha alipo sasa na kati ya mambo yaliyomuumiza kichwa ni kuwatafakari iwapo wamama siku hizi wanazungumza sana na mabinti zao.

Alilinganisha kipindi wakati akiwa msichana mdogo hadi kufikia kuwa mdada mkubwa haikuwepo mitandao ya kijamii ambayo hivi sasa inapatikana kwa wingi tena hadi katika simu za mikononi.

Mitandao hiyo anaeleza imekuwa ina mazuri na mabaya kwa malezi ya watoto sasa kwa kuwa watoto hao wanaweza kujifunza mazuri na mabaya kupitia simu na swali ni je,  wazazi wanalionaje hilo na kwa kiasa gani wanalinda watoto wao dhidi ya mabaya hayo yanayopatikana kwenye mitandao.

Anasema maswali hayo kwa siku hiyo yalimnyima usingizi huku akimwangalia binti yake huyo na kuona kuwa kama yeye anayo ya kuzungumza naye na amekuwa akizungumza naye kuhusiana na maisha kwa ujumla, ni kwa nini asizungumze na watoto wengine.

Hapo ndipo likaja wazo la yeye kuandika kitabu hicho cha “Things I tell my Daughter” kitabu ambacho ndani yake amejumuisha yale yote ambayo huzungumza na binti yake huyo ili yatumiwe na wazazi na mabinti kujifunza kitu.

Lakini pia ndani yake amegusia malezi kwa ujumla kutokana na yale ambayo amejifunza katika maisha yake akiwa kama mwanamke aliyewahi kupitia usichana,  udada na sasa mama.

Akizungumzia zaidi kitabu hicho Mwamvita anasema kuwa baada ya kupata wazo la kukiandika ili kuwasaidia walezi, wazazi na wasichana akaanza kazi ya kukiandika huku akiweka ubunifu zaidi ili kisiwe kama kitabu cha kawaida chenye kurasa zilizojaa maneno.

Anasema ubunifu huo umelenga kuwasaidia wasomaji kukisoma na kukielewa kwa haraka  na kila kurasa kuna nukuu ya kiingereza na kiswahili.

 

“Yaani kwangu huu ni kama mchango wangu kwa jamii za Tanzania, Afrika na naweza kusema dunia nzima kwa ujumla hasa nikitoa mtazamo wangu kuhusiana na malezi ya mtoto wa kike. Nimeangalia siye tulivyokuwa na mama zetu na je,  watoto wa sasa wanapaswa kulelewa vipi na mama zao.

“Sina maana ya kuwa mimi ninajua sana malezi ila nimeshirikisha yale ambayo ninayaona kuwa yanapaswa kufanywa na wasichana wenyewe katika maisha lakini pia kinaweza kuwa mwongozo kwa wazazi katika kuwalea watoto hasa kipindi hiki cha mitandao ya kijamii ikiwa imepamba moto,” anasema.

Wasichana wengi wamekuwa wakipata malezi kutoka mitandaoni au kupitia vipindi mbalimbali vya televisheni na zimekuwepo jumbe mbalimbali kutoka kwa watu wakizungumzia kuhusiana na malezi pia.

 Kuna ujumbe mzuri na pengine pia kumekuwa na ujumbe ambao sio nzuri hasa kutokana na tofauti za malezi, mila na desturi za nchi na nchi au jamii na jamii lakini vyote vinawekwa pamoja katika mitandao hiyo.

Kati ya mambo ambayo Mwamvita anayaamini katika malezi bora ya wazazi au walezi kwa mtoto ni pamoja na kujenga utamaduni wa kuwapongeza au kuwasifia pale wanapofanya mambo mazuri.

Anasema kwa kuwasifia inasaidia zaidi kuwajengea hali ya kujiamini, kujithamini kama watoto na kujiamini ni silaha kubwa kwa watoto hasa mtoto wa kike. 

Kitabu hicho kimewasihi wasichana kuhusiana na kupenda dini kwa maana ya namna ya kumshirikisha Mungu katika mambo yao ya kila siku, pia wamegusiwa suala la kuwa na utu kwa watu na umuhimu wa kuziishi na kutimiza ndoto zao.

Anabainisha  kuwa kitakuwa kinapatikana katika maktaba zote nchini, katika migahawa, maduka na sehemu mbalimbali ambazo wazazi au walezi wanafika na kitakuwa kikiuzwa Sh 35,000.

Mwamvita anasema kuwa kitabu hicho kinatarajiwa kuuzwa nchi za Kenya, Uganda, Zambia na Nigeria kwa kuwa kimeandikwa kwa lugha ya kiingereza na kiswahili na kuwa ni muda muafaka wa kukiingiza kwenye nchi hizo ili kuendeleza malezi ya mtoto wa kike.

Kuhusiana na dhana ya msichana kujiamini anasema inaanza kujengwa tangu akiwa kwenye ngazi ya kifamilia, kwake imekuwa msaada mkubwa hadi kufikia hatua ya kupatiwa cheo katika kampuni ya Vodacom Makao Makuu.

Anasema yeye amesoma hapa hapa nchini Tanzania kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu na elimu ya Chuo Kikuu amesoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alichukua Shahada ya Sayansi ya Siasa na Utawala. Pia amesoma Shahada ya Uzamili ya Masuala ya Mahusiano ya Kimataifa.

Mwanamvita anasema kuwa kujiamini na kufanya kazi kwa ufanisi, umakini na kutoendekeza mzaha ndio kumemuwezesha kupata nafasi za juu katika kampuni ya Vodacom Tanzania na kuhamishiwa nchini Afrika Kusini.

Anasema akiwa nchini humo na binti yake aliamua kuanzisha kampuni ya MM Connect Africa ambayo inaendelea vema kufanya kazi katika nchi mbalimbali za Afrika.

evance ngingo <evancengingo@gmail.com>

Mbali na maisha yake ya kiujasiriamali, kazi na malezi Mwamvita anasema kuwa anapenda kutumia muda wake mwingi kukaa mwenyewe akifanya shughuli zake, pia anapenda zaidi kusafiri sehemu mbalimbali huku akikutana na watu wapya wenye mawazo mapya.

Mwanadada huyu ambaye pia anasifika kwa kupenda kuvaa, kila wakati akionekana ni lazima anakuwa amevalia nadhifu na anajua kupangilia mavazi yake.

Mwamvita wakati akiwa anafanya kazi Vodacom Tanzania alikuwa akishiriki kikamilifu katika kuendeleza tasnia za ubunifu wa mavazi kwa kuhakikisha wabunifu wanapata udhamini wa maonesho yao.

Lakini pia hata yeye mwenyewe anasema kuwa akiwa kama mjasiriamali mwonekano ni kitu muhimu ili kuwashawishi na kupata wateja mbalimbali na kuwa anapenda kuonekana nadhifu muda wote.

Mwamvita anapenda muziki hasa muziki wa Afrika wa aina zote kuanzia muziki wa Bongo Fleva, Zhouk, Rhumba na hasa anapendelea kwenda kwenye matamasha mbalimbali ya muziki.

Akiwa nyumbani mbali na kumwangalia binti yake huyo wa pekee, huwa ni mtu wa kufanya shughuli kama mama wa kiafrika kma vile usafi, kupika na  hakosi kusoma vitabu na kusikiliza muziki.

Anapongeza serikali kwa jitihada zake za kuendeleza sanaa, utamaduni, michezo na masuala mengine ya maendeleo hasa kumsaidia mtoto wa kike kupata elimu bora na kumlinda.

Mwamvita ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini Yusuph Makamba na mama Josephine.

WANAWAKE wamekuwa ni chachu kubwa ya ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi