loader
Kuanza kwa huduma za meli  Ziwa Nyasa kutakuza uchumi

Kuanza kwa huduma za meli Ziwa Nyasa kutakuza uchumi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua meli mpya ya abiria ya MV Mbeya II katika Ziwa Nyasa ambayo itakuwa inahudumia bandari mbalimbali katika ziwa hilo.

Kwa upande wa Tanzania, bandari hizo zipo katika wilaya za Kyela mkoani Mbeya, Ludewa mkoani Njombe na Nyasa mkoani Ruvuma.

Akitoa taarifa ya huduma za bandari katika ziwa Nyasa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko anasema TPA inahudumia jumla ya bandari 15 katika Ziwa Nyasa ambapo katika Mkoa wa Ruvuma, TPA inahudumia bandari sita.

Anazitaja bandari za Ziwa Nyasa katika Mkoani Ruvuma kuwa ni Mbambabay, Liuli, Njambe, Lundu, Mkili na Ndumbi na katika Mkoa wa Njombe TPA pia inahudumia bandari sita ambazo ni  Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde, Lupingu na Manda ambapo katika Mkoa wa Mbeya TPA inahudumia bandari tatu ambazo ni Itungi, Kiwira na Matema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo wa TPA, baadhi ya bandari hizo tayari TPA imeweka miundombinu ya kisasa na zingine zinaendelea kuwekewa miundombinu kwa ajili ya utoaji huduma bora na za kisasa.

Kila bandari anasema inahitaji kuwa na magati kwa ajili ya vyombo vya majini kutua, maghala, yadi za kutunzia mitambo na mizigo na uwepo wa nyumba za kuishi wafanyakazi.

Hayo anasema yanakwenda sambamba na kuweka mifumo ya zimamoto, majisafi, maji taka na mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ili kufanyakazi kwa ufanisi na tija kulingana na maelekezo ya serikali. 

Anasisitiza kuwa katika miaka mitano ijayo TPA imejipanga kukamilisha miundombonu na mifumo yote kwenye bandari zote 15 zilizopo katika Ziwa Nyasa.

Akizungumzia utendaji kazi wa TPA katika ziwa Nyasa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Kakoko anazitaja shehena kuu zilizokuwa zinasafirishwa kuwa ni makaa ya mawe ambayo yalikuwa yanapakiwa kutoka bandari za Ndumbi na Mbambabay na kusafirishwa hadi bandari ya Kiwira iliyoko Kyela mkoani Mbeya.

Anasema katika kipindi hicho, TPA pia iliweza kusafirisha saruji, mabati, dagaa, sukari na shehena zingine ambapo kwa kipindi cha miaka sita TPA ilihusika katika kusafirishwa mizigo ya wastani wa tani 4,500 kwa mwaka.

Anasema kwa ujumla kulikuwa na ongezeko la tani 9,000 ya mizigo kutoka tani 2,233 ya mwaka 2014/2015 hadi tani zaidi ya 11,000 mwaka 2019/2020.

Kakoko anasisitiza kuwa ili kuboresha huduma katika bandari zote za Ziwa Nyasa, TPA inatekeleza mpango kabambe unaoanza mwaka 2021/2022 na unaotarajia kukamilika katika kipindi cha mwaka 2028/2029.

Mpango huo kabambe utaongeza shehena ya mizigo katika ziwa Nyasa kutoka tani zaidi ya 11,000 za sasa hadi kufikia zaidi ya tani 100,000, lengo hili linachochewa na mipango mizuri ya serikali ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Mbambabay, anasema Kakoko.

Anasema kukamilika kwa lami ya Mbinga hadi Mbambabay na kuanza kutoa huduma kwa meli katika Ziwa Nyasa kutafufua uchumi wa mji wa Mbambabay, hivyo kuunganisha Tanzania kupitia ushoroba wa Mtwara na nchi za Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na Zambia.

“Mji wa Mbambabay utafufuka kwa kasi kwani TPA inafanya usanifu wa bandari zote zilizopo katika Ziwa Nyasa na kwa kweli tunashirikiana na nchi jirani ya Malawi ili wakati tunaendeleza bandari za Tanzania, tuendeleze pia bandari za Malawi. Pia tunafanya kampeni za masoko katika nchi za Malawi na Msumbiji," anasema.

Akizungumzia kuhusu kuanza safari kwa meli mpya ya abiria na mizigo katika Ziwa Nyasa, Mkurugenzi huyo wa TPA anasema ziwa Nyasa sasa lina meli tatu zinazomilikiwa na serikali, kati ya hizo meli mbili za MV Njombe na MV Ruvuma ni za mizigo na meli moja ya MV Mbeya II ni ya abiria.

Anasema katika kipindi cha miaka sita iliyopita kwa wastani kwa mwaka kulikuwa na abiria 4,917 lakini kumekuwa na ongezeko la abiria katika mwaka 2019/2020 kutoka abiria 894 mwaka  2018/2019 hadi abiria 3867 mwaka 2019/2020 baada ya kujitokeza meli ya abiria ya MV Chambo ya Msumbiji ambayo iliacha kutoa huduma baada ya kuzuka kwa COVID 19.

Hata hivyo, anasema idadi ya abiria inatarajia kuongezeka katika ziwa Nyasa baada ya kuzinduliwa kwa huduma ya meli ya abiria ya MV Mbeya II ambayo itawezesha kusafirisha abiria zaidi ya 12,000 kila mwezi.

Akizungumzia gharama za meli zote tatu katika ziwa Nyasa, Kakoko anasema zaidi ya shilingi bilioni 20.1 zimetolewa na serikali kujenga meli zote tatu na kwamba meli hizo zimetengenezwa na kampuni ya Songoro Marine inayomilikiwa na Mtanzania.

Anasema meli mbili za mizigo, MV Njombe na MV Ruvuma, kila moja ina uwezo wa kubeba tani 1,000 na kila meli imegharimu shilingi bilioni 5.5 na meli ya abiria ya MV Mbeya II ina uwezo wa kubeba abiria 300 na mizigo tani 200. Imegharimu shilingi bilioni 9.1.

Kwa mujibu wa Kakoko meli ya abiria ya MV Mbeya II imerithi jina la meli ya MV Mbeya I iliyozama eneo la Makonde, Ziwa Nyasa mwaka 1977.

Hata hivyo, anasema meli ya MV Mbeya II baada ya kujengwa iliingizwa majini Septemba 2019 na kwamba kwa kuwa meli ni chombo ambacho kinatakiwa kuwa na usalama wa kutosha ilikaguliwa kimataifa na kupata kibali cha mamlaka inayosimamia usalama wa vyombo vya majini na kuanza safari Oktoba 20, 2020.

Akizungumza baada ya kuzindua meli mpya ya abiria ya MV Mbeya II, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anasema wilaya ya Nyasa sasa imefunguka kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Mbambabay na kuanza rasmi kwa huduma za meli tatu ndani ya Ziwa Nyasa.

Waziri Mkuu anasema serikali imetoa fedha za ujenzi wa meli tatu katika Ziwa Nyasa na kwamba kazi ya kujenga meli ni endelevu na inafanyika katika maziwa yote kwa kuwa bandari ni lango kuu la kukuza uchumi wa Taifa.

Majaliwa anasema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha Watanzania wanafanya biashara katika mazingira rahisi na ndio maana inajenga miundombinu ya usafirishaji ili kuchochea shughuli za uchumi na uzalishaji.

“Ujenzi wa meli ya abiria na uimarishaji wa bandari katika Ziwa Nyasa una lengo la kuimarisha shughuli za kiuchumi hususani biashara na uwekezaji katika ukanda wa Ziwa Nyasa, sisi kama serikali tumepania kuhakikisha watanzania wanaoishi ukanda huu wanafikiwa kwa kujengewa uchumi wenu,” anasisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu anatoa rai kwa watanzania waliopo ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika Wilaya ya Nyasa ambayo miundombinu yake imeboreshwa ikiwemo barabara ya lami, umeme na usafiri wa majini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Nyasa ameipongeza serikali kwa kutoa mabilioni ya fedha kujenga meli tatu mpya zitakazotoa huduma katika Ziwa Nyasa.

Mndeme anasema kukamilika na kuanza safari kwa meli ya abiria ya MV Mbeya II na kukamilika kwa barabara ya lami ya Mbinga hadi Mbambabay kuna ondoa kabisa kero ya usafiri na usafirishaji iliyokuwa inawapata wananchi wa Mkoa wa Ruvuma.

“Sasa mtanzania anaweza kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mbambabay kwa kutumia barabara au meli bila kugusa vumbi.  Huyu ndiye Dk John Magufuli, sasa Mkoa wa Ruvuma unakwenda kuonekana majini, nchi kavu na angani,” anasisitiza Mndeme.

Mndeme anasisitiza kuwa uwepo wa miundombinu hii unakwenda kuchochea shughuli za biashara na utalii kwa sababu Mkoa wa Ruvuma umebarikiwa kuwa na vivutio adimu vya utalii zikiwemo fukwe na visiwa katika Ziwa Nyasa.

Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Stella Manyanya anasema kuboreshwa kwa barabara na uwepo wa meli mpya kutaongeza idadi ya wageni wanaotembelea wilaya ya Nyasa ambayo ni kitovu cha utalii katika Mkoa wa Ruvuma.

 

Mwandishi wa makala ofisi habari wa mkoa wa Ruvuma na mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni baruapepe;albano.midelo@gmail.com

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/9dc299ddbb0d0473e27b1510d7353e18.JPG

HAPA nchini Agosti 23 mwaka ...

foto
Mwandishi: Albano Midelo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi