loader
Dstv Habarileo  Mobile
JPM kuibana wizara hospitali ikamilike

JPM kuibana wizara hospitali ikamilike

RAIS John Magufuli ameitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikamilishe haraka ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato na hataki ijengwe kwa awamu.

Aidha, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amempongeza Rais Magufuli kwa kushughulika na maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya afya.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo mara baada ya mgeni wake Rais Nyusi kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hiyo.

Hospitali hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 700 hadi 1000 kwa siku ikiwa na vitanda zaidi ya 400.

"Sisi Watanzania na wakazi wa kanda hii tunaona ni zawadi kubwa kwa wewe (Rais Nyusi) kuja kuweka jiwe la msingi…kwa sababu nimemleta hapa Rais (Filipe Nyusi) kuweka jiwe la msingi, mmejichongea, hospitali lazima ikamilike, hatuwezi kumleta Rais hapa halafu siku nyingine ananipigia simu vipi ile hospitali niseme bado inajengwa hilo sitakubali."alisema Rais Magufuli na kuongeza;

"Nataka nikuhakikishie mheshimiwa Rais nitawabana kweli kweli wizara ya afya, ili hopitali hii ikamilike mapema, mambo ya kusema awamu ya kwanza, awamu ya pili, awamu ya tatu, hapana nataka ikamilike kwa pamoja”.
 

Baada ya Rais Magufuli kumaliza kuzungumza Rais Nyusi alisema: "Rais Magufuli amenipa kuweka jiwe la msingi, nitamsumbua sana, kila Jumamosi asubuhi nitampigia simu kumuuliza hospitali vipi, mkilala mtafukuzwa maana sitakubali kufedheheshwa," 

Awali akisoma taarifa ya mradi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Dorith Gwajima alisema awamu ya kwanza ya ujenzi imefikia asilimia 90 ikitumia Sh bilioni 14 kati ya Sh bilioni 16 zilizopangwa kutumika.

"Makabidhiano ya miundombinu hiyo ya awamu ya kwanza inatarajiwa kufanyiwa mapema mwezi Machi mwaka huu ambapo pia ujenzi wa nyumba 20 za wafanyakazi umefikia asilimia 85”alisema.

Alisema pia ujenzi wa kilomita 1.4 ya barabara ya lami ya kuzunguka hospitali hiyo utagarimu Sh bilioni 1.6 na inajengwa na (TARURA) huku SUMA JKT wakijenga uzio kwa makadirio ya Sh milioni 400.

Alisema awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo pia itahusisha majengo ya jiolojia, wodi za upasuaji, mifupa na magonjwa ya ndani na kukamilika kwa awamu ya pili kutawezesha jumla ya vitanda vya wagonjwa  201 huku takribani bilioni 14 zikikadiliwa kutumika kwa awamu hiyo.

Awamu ya tatu ya ujenzi itahusisha chumba cha kukufulia, jengo la kuhifadhia maiti na upasuaji.

Akizungumzai ziara ya Rais Nyusi, Rais Magufuli alisema mgeni wake ni kiongozi anayajua maisha ya Watanzania na ni rafiki wa Watanzania.

Magufuli alisema, urafiki wa nchi hizo mbili ni wa muda mrefu tangu enzi za waasisi wa mataifa haya mawili, Mwalimu Nyerere na Samora Machel

Alisema ya serikali ya Tanzania na Msumbiji zina makubaliano ya kufanya kazi pamoja, kushirikiana na kufanya biashara pamoja na kwamba, biashara kati ya nchi hizi kwa mwaka jana imepanda hadi kufikia Sh bilioni 93.6.

"Kuna kampuni za Msumbiji zinafanya kazi hapa, na kampuni za Tanzania zinafanya kazi kule, sisi wote ni wanachama wa SADC yenye wananchi takribani milioni 450 na mwenyekiti wetu ni Filipe Nyusi”alisema na kuongeza;

"Aliniambia nataka kuja Chato tuzungumze masuala ya maendeleo na mimi kwa heshima yake namshukuru sana kukubali kuweka jiwe la msingi”.

Dhana ya kujitengemea

Rais Magufuli alisema dhana ya Tanzania kujitegemea ya mwalimu Julius Nyerere ilianzia Chato Januari 9 mwaka 1967, alifika kufungua kiwanda cha pamba kilichojengwa kwa thamani ya Sh milioni 2, kilichokuwa na uwezo wa kusokota marobota 20,000 kwa mwaka.

 "Alitambua kuwa maeneo haya ni ya wakulima wa pamba, na wakati wa ufunguzi Mwalimu Nyerere alianzisha mchango kwa wananchi waliokuwapo pale ikiwa ni kujenga dhana ya kujitegemea”alisema.

Magufuli alisema Mwalimu Nyerere alichangia paundi 1,000 kwa ajili ya kujenga Bandari ya Nyamirembe kwa lengo la kusafirisha marobota ya pamba, na bandari ambayo mpaka sasa ipo.

"Na baada ya hapo wiki mbili baadaye Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere yaani tarehe 5/2 mwaka 1967 alitangaza Azimio la Arusha likiwa na dhana aya kujitegemea, alianzia hapa Chato kwa kuchangia Sh 2,000, Rais Nyusi umefika hapa malaki ambapo mwali Nyerere alianzisha dhana ya kujitegemea”alisema..

Alisema Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliitangaza Chato kuwa wilaya na Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliizindua wilaya hiyo.

Wakati akizungumzia ziara yake, Rais Nyusi alisema: siku tatu zilizopita alimpigia simu Rais Magufuli na kumuuliza alikuwa wapi.

“Na mara nyingi tunazungumza asubuhi na mapema, akaniambia yuko Chato nyumbani, nikamwambia basi nije huko nyumbani kwako na kuioana shule ya msingi uliyosoma wewe”alisema.

Rais Nyusi amempongeza Rais Magufuli kwa kushughulika na maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya afya.

"Nashukuru kwa kunipa heshima ya kuweka jiwe la msingi katika hospitali hii, hii ni habari nzuri kwenu, kwa sababu serikali inayoangalia afya ya wananchi ni serikali inayowapenda wananchi, unaweza fanya kila kitu lakini bila maisha si kitu."alisema na kuongeza;

"Rais Magufuli anashughulika sana na maisha ya Watanzania, anawahangaikia kwenye nyumba, chakula, maji na afya tena afya bora, kuwekeza kwenye afya ya wananchi ni ustawi mkubwa sana”.

Alisema, nchini Msumbiji wameanza program ya kujenga hospitali kamili katika kila wilaya, na kwamba Tanzania kujenga hospitali kubwa ya kanda ni mfano mzuri kwa sababu itahudumia mikoa mitano, lakini pia iko karibu na Uganda, Rwanda na Kenya kwa maana hiyo hata wananchi wa nchi hizo wataweza kuitumia.

Rais Nyusi alisema mwaka 2014 wakati anaaza safari yake ya kuwania urais wa Mozambique alifika Tanzania na kukutana na Mama Maria ambaye alimpa nasaha za kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga angalau kiwanda kimoja cha dawa.

"Mwaka 2014, nilikuja hapa Tanzania kujiandaa na kampeni yangu ya kwanza, lipofika nilikutana na Mama Maria Nyerer (mjane wa Hayati Julius Nyerere) tulizungumza muda mrefu na alinipikia mbuzi…siku ile alinihusia kitu kimoja na alisema'utakuwa rais ndiyo na nakuombea uwe lakini usisahau kujenga hata kiwanda kimoja tu cha dawa, watu wengi wanakufa katika nchi zetu kwa kukosa hata aspirini, lakini ndugu yangu Magufuli sijui alisikia wapi maana anashughulika na afya ya wananchi.

Akizungumzia mazungumza yao, Rais Nyusi alisema watazungungumzia ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika maeneo ya uchumi na suala la ulinzi na usalama.

"Katika mazungumzo yetu tutazungumzia maendeleo ya nchi zetu na hii si kwa sababu ya mpaka, bali ni kwasababu watu wengi wa Tanzania wako Mozambique na wa Mozambique wengi wako Tanzania, tutazungumzia biashara, pia suala la ulinzi na usalama."alisema.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi